Habari za Punde

Mkutano wa wasaidizi wa sheria wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC)

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Khamis Juma Mwalim akifungua mkutano wa siku mbili wa wasaidizi wa sheria wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) katika ukumbi wa Hotel ya Zanzibar Beach Resort nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
Baadhi ya washiriki wa mkutano wa wasaidizi wa sheria wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) wakifuatilia kwa makini mkutano huo
Baadhi ya washiriki wa mkutano wa wasaidizi wa sheria wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) wakifuatilia kwa makini mkutano huo


Na Raya Hamad 

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania(SMT) na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) zimejidhatiti kwa pamoja  kuunga mkono wasaidizi wa sheria kutokana na umuhimu walionao katika kuwafikia walengwa.

 

Hayo yalisemwa na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Khamis Juma Mwalim wakati akifungua mkutano wa siku mbili wa wasaidizi wa sheria wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) katika ukumbi wa Hotel ya Zanzibar Beach Resort nje kidogo ya mji wa Zanzibar.

 

Waziri  Khamis  alisema Serikali mbili hizo zinawaunga mkono wasaidizi wa kisheria kutokana na njia muhimu ya kufikia maendeleo endelevu ya dunia (SDG).

Alisema ushirikiano wa wasaidizi wa kisheria katika  nchi za SADC  utaweza kuwasaidia wananchi wenye uwezo mdogo kupata haki yao ya msingi kutokana na matatizo wanayokumbana nayo.

“Serikali zetu mbili za SMT na SMZ imejidhatii kuhakikisha inawaunga mkono kikamilifu wasaidizi wa kisheria katika kutatua matatizo na kuwaletea mataendeleo wananchi wanyonge,”alisema.

Waziri Khamis alisema Zanzibar imefanikiwa kupitisha Sheria ya  Msaada wa kisheria mwaka 2018 kutokana na umuhimu uliokuwepo  wa kulizungumzia hilo kutokana na baadhi ya wananchi hawajui umuhimu wa kuwepo kwa wasaidizi hao.

Hivyo aliwaomba wananchi wa Zanzibar kuitumia Idara ya Msaada wa Kisheria kwani ipo kwa ajili yao na imejipangia mikakati ya kuwafikia wananchi wote kwa kuweka ofisi kwenye Wilaya zote ili kuwafikia wananchi wake.

Waziri Khamis amewashukuru waandaji wa mkutano huo pamoja na waliofanikisha kufanyika kutokana na umuhimu wake kwa maendeleo endelevu ya nchi na kwamba huduma za kisheria zinahitaka kumfikia kila raia.

Nae Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Profesa Sifuni Mchome alisema mwaka 2017 SMT imepitisha sheria ya kuwatambua na kwa sasa wamesambaa nchi nzima .

Alisema tayari wasaidizi wa kisheria Tanzania Bara wanatambulika kisheria na wamekua wakitoa msaada mkubwa kwa wananchi wenye mahitaji hayo katika maeneo mbali mbali.

“Wasaidizi wa kisheria Tanzania Bara wanafanya kazi vizuri na wanatambuliwa na Serikali lakini changamoto kubwa zinazowakabili ni ukosefu wa fedha pamoja na uelewa mdogo miongoni mwa wananchi,”alifafanua.

Akizungumza kabla ya ufunguzi wa mkutano huo, Mkurugenzi wa Idara ya Msaada wa Kisheria Hanifa Ramadhan Said alisema mkutano huo umefanyika wakati muafaka kwa kubadilishana uzoefu na kuendeleza mbele huduma za kisheria kwa wananchi hususan maskini na wenye mahitaji maalum vijijini.

Mkutano huo ulitarajiwa kufanyika mwezi wa sita mwaka huu, kutokana na kuzuka kwa maradhi ya homa kali ya mapafu inayotokana na virusi vya corona  na umefanyika leo ambapo baadhi ya wanachama wa shiriki wa jumuiya hiyo ambao hawajaweza kufika wanahudhuria mkutano huo kwa njia ya mtandao wa kijamii wa Zoom.

Mkutano huo umedhaminiwa na Shirika la Legal Services Facility (LSF) ambapo Afisa Mtendaji Mkuu , Lulu Ng'wanakilala  amesema wamekuwa wakifanya kazi kwa karibu na Wizara ya Katiba na Sheria kwa Serikali zote mbili ya SMT na SMZ katika kuwezesha upatikanaji wa haki nchini kwa kupitia watoa huduma za msaada wa kisheria nchini, Tanzania bara na Zanzibar. Kuwezesha kufanyika mkutano huu ni mwendelezo wa dhamira ya LSF ya kuleta mapinduzi katika upatikanaji wa haki katika nchi za SADC

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.