Habari za Punde

Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Mhe.Dk Ali Mohamed Shein Amuombea Kura Mgombea Urais wa Zanzibar Kwa Tiketi ya CCM Mhe.Dk. Hussein Mwinyi Kwa Wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja leo.

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar ambae pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein akihutubia katika mkutano wa kampeni ya Mgombea Urais wa Zanzibar Mhe.Dk. Hussein Mwinyi uliofanyika katika viwanja vya Sisi kwa Sisi Bumbwini Wilaya ya Kaskazini "B" Unguja.

MAKAMO Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa uchaguzi ujao wa Zanzibar utaendeshwa kwa fedha za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na hakutohitajika msaada kutoka nje ya nchi.

Dk. Shein ameyasema hayo leo huko Bumbwini Makoba, Wilaya ya Kaskazini B, Mkoa wa Kaskazini Unguja katika Mkutano wa Kampeni za CCM zinazoendelea kote nchini.

Alisema kuwa Zanzibar iko tayari kuingia katika uchaguzi mnamo Oktoba 28 mwaka huu wa 2020 ikiwa inajitegemea wenyewe kwa kuendesha uchaguzi wake bila ya kutegemea msaada kutoka nje ya nchi.

Makamo Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar alisema kuwa Mwenyezi Mungu kaipa uwezo Zanzibar ya kufanya baadhi ya mambo yake na yapo mambo ya kusaidiawa, lakini si uchaguzi.

“Watuwachie wenyewe tunayaweza, na kwa saabau kasha kwua Waziri wakati wa uongozi wangu anayajua yote mambo ya Muungano”,alisema Dk. Shein.

Alisema kuwa hakuna wa kuja kuitawala Zanzibar na badala yake Zanzibar itatawaliwa na Wazanzibari wenyewe.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa CCM akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ali Hassan Mwinyi, Spika wa Baraza la Wawakilishi na viongozi wengine wa chama hicho.

Akieleza historia ya Zanzibar, Makamo Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar alisema kuwa Marais wote waliopita awamu wka awamu waliindeleza historia ya Zanzibar pamoja na kuyaendeleza na kuyaenzi Mapinduzi ya Zanzibar.

Alisema kuwa zaidi ya karne nne, Zanzibar ilitawaliwa lakini kabla ya hapo Zanzibar ilikuwa huru na kuanzia mwaka 1957 mpaka 1964 chama cha ASP kilipigania uhuru wa wanyonge na hatimae ikaamua kufanya Mapinduzi Matukufu ya Januari 1964 kwani demokrasia haikufanya kazi.

Alisema kuwa Mapinduzi yamefanyika kwa lengo la kuondosha dhulma kwani wazee walikataa kudharauliwa, kutawaliwa, kunyanyaswa na kupuzwa na ndipo Marehemu Mzee Abeid Karume na viongozi wenzike wakafanya Mapinduzi.

Alisema kuwa wapo wanayoyabeza na kuyakashifu Mapinduzi hivyo, aliwataka wanaCCM kuachana nao.”Mapinduzi daima ina maana kuwa ni lazima Mapinduzi tutayaenzi, tutayadumisha na tuyatunze”,alisisitiza Dk. Shein.

Alisema kuwa iwapo Dk. Hussein atapata ridhaa ya wananchi kuiongoza Zanzibar ataendeleza heshima na utu wa Mzanzibari kwani atakuwa imara kukataa kutawaliwa na kudharauliwa na kunyanyaswa na wanaCCM na wapenzi wa maendeleo watamuunga mkono. “Mimi nikiuka anaingia Dk. Hussein Ali Hassan Mwinyi”alisema Dk. Shein.

Katika hotuba yake kwa wanaCCM na wananchi Makamo Mwenyekiti huo wa CCM aliwataka wananchi kutowachagua viongozi wabaguzi na wanayoyapinga Mapinduzi ya Januari 12, 1964 na badala yake wawachague viongozi wenye nia safi na uwezo wa kuiongoza Zanzibar.

Aidha, aliwataka wanaCCM, kumchagua Dk. Hussein Mwinyi kwani yeye ndie atakaouendeleza atakaoutunza na kuuenzi Muungano uliopo.

Rais Dk. Shein alisisitiza kuwa njia pekee ya kuingia Ikulu ni demokrasia pekee, na si vyenginevyo.

Alieleza kuwa vipo baadhi ya vyama vya upinzani ambavyo havikuwa na Ilani ya Uchaguzi na vimezindua Ilani baada ya kuingia katika Kampeni jambo ambalo ni vichekesho “Sisi tunajua hawana mpya na wanakopia tu yale tunayoyasema”,alisisitiza Rais Dk. Shein.

Makamo Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar alisema kuwa CCM iliizindua kampeni zake rasmi mnamo tarehe 29.8.2020, ilizindua Kampeni pamoja na kuizindua Ilani ya CCM.

Aliongeza kuwa Dk. Hussein ana sifa zote za kisiasa na zile za kielimu kwani ni bingwa aliyebobea katika fani ya utibabu ambaye pia ni kiongozi muadilifu.

Pia, Dk. Shein alisema kuwa Dk. Hussein ni mbunifu kwani ameibua mambo mengi katika uongozi wake ndani ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pia ,ni mstaahamilifu na mvumilivu na ndio maana CCM ikamchagua kuwa mgombea wa CCM Zanzibar.

Aliwataka wanaCCM na wananchi kumpokea Dk. Hussein Mwinyi huku akiwaahidikwua Dk. Hussein atashinda kwa kishindo kura zisizo na mfano ambapo pia alimuombea kura Dk. Magufuli pamoja na mgombea wake mwenza Samia Suluhu Hassan, Dk. Hussein Mwinyi, Wabunge, Wawakilishi pamoja na Madiwani wote wa CCM.

Nae Dk. Hussein Mwinyi alimpongeza Rais Dk. Shein kwa Utekelezaji Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa upande wa Zanzibar na kueleza kuwa ahadi zote ambazo Rais Dk. Shein aliahidi katika Baraza la Idd al Hajj lililofanyika Bumbwini kwa ajili ya Bumbwini yeye atazitekeleza.

Akianzia ombi la Hospitali ya Wilaya katika eneo la Bumbwini, alitoa shukurani kwa Awamu ya Saba kwa kutekeleza sekta ya afya na kuahidi kwamba Awamu ya Nane itajenga miundombinu ya kutoa huduma ya afya, nyumba za madaktari, kuongeza bajeti na vifaa tiba ili huduma za afya ziwe bora pamoja na kuajiri wafanyakazi wa afya ili kupunguza uhaba.

Alisema kuwa ni matarajio yake kwamba huduma zitakuwa nzuri na itapunguza wananchi kwenda katika Wilaya  nyengine ama kuzifuata huduma hizo mjini.

Aliongeza kuwa barabara ya Bumbwini hadi Mahoda itakayounganisha  Mashariki na Mgharibi itajenwga na kwa vile kutajengwa bandari ya mafuta na gesi barabara hiyo itakupunguza mzungumko ambao watu wengi wanaupata hivi sasa jambo ambalo atalipa kipaumbele.

Aliongeza kuwa, ujenzi wa daraja ambalo linahitajika katika mto wa Zingwezingwe litajenwga ambalo litakuwa la kisasa na kuwezesha watu kupita huku akisisitiza kwamba iwapo barabara hiyo na daraja hilo litajengwa hospitali ya kisasa pia, itajengwa katika eneo la Pangatupu.

Alisema kuwa ujenzi wa miundombinu hiyo itabadilisha hali ya uchumi wa watu wa Kaskazini B, kwani utakuwa ni uchumi wa kisasa utakaoleta maendeleo sambamba na ajira kwa vijana.

Pia, aliahidi kuitekeleza ahadi ya ujenzi wa barabara ya Makoba hadi Kiongwe, iliyoahidiwa na Awamu ya Saba ili kuwapa urahisi wananachi wa eneo hilo katika kutekeleza shughuli zao za kiuchumi.

Sambamba na hayo, mgombea huyo aliahidi kujengwa kwa skuli ya ghorofa huko Bumbini Gongoni kwani kuna uhaba wa madarasa huku akiadi kuwa mbali ya skuli hiyo ya ghorofa pia katika uongozi wake kutajengwa mabweni, ili kuweza kusaidia wanafunzi wanaotoka maeneo ya mbali.

Kuhusu changamoto ya wizi wa mifugo, Dk. Hussein Mwinyi alisema kuwa wizi wa ngombe umekithiri na wafugaji wameacha na kupelekea kutopatikana kwa maziwa hivyo katika uongozi wake atahakikisha hilo linapigwa vita kwani tayari kiwanda kipo, hivyo ni lazima kuondokana na wizi ili wananchi wafaidike.

Alisisitiza haja ya kuweka hatua madhubuti katika kuhakikisha sekta ya maziwa inawaongezea kipato.

Na kwa upande wa mradi wa bandari ya mafuta na gesi, mradi huo ni moja ya kipambelee cha Serikali ijayo kwani itahakikisha kunajengwa bandari ya kisasa na kubwa huko Mangapwani, Wilaya ya Kaskazini B, kwa lengo la kuongeza uchumi wa Zanzibar.

Alisema kuwa Wilaya hiyo imepata bahati ya kujengwa kwa mradi huo mkubwa wa bandari ambao utakuwa ni kitovu cha uchumi wa Zanzibar ambayo itatoa ajira nyingi sana.

Aliongeza kuwa ajira laki tatu alizoziahidi miongoni mwao zitatoka katika bandari hiyo ambayo haitoathiri shughuli za wananchi huku akisema kuwa hatua zitachukuwa kwa wajasiriamali za kuwatafutia eneo maalum la kufanya shughuli zao wakiqwemo wavuvi wadogo wadogo na waanika dagaa.

Alisema kuwa lengo lake ni kuhakikisha wajasiriamali wanawezeshwa na kipaumbele zaidi kitaelekezwa katika utoaji wa mafunzo ili waweze kufanya shughuli zao kitaalamu pamoja na kuwapa nyenzo, mitaji na mikopo yenye masharti nafuu pamoja na kuwatafutia masoko.

Kwa upande wa huduma ya maji safi na salama alisema kuwa hasa kwa wale walio mbali na barabara ambao bado hawajapata maji alisema kuwa pale ilipofikia Serikali ya Awamu ya Saba ni pakubwa na palipobaki ni padogo ambapo Serikali atakayoiongoza itamalizia.

Akilitaja eneo jengine alisema kuwa kipaumbele alisema ni suala la viwanda , ambapo Zanzibar ya viwanda itatoa ajira kwa viajana, soko la uhakika la bidhaa zinazozalishwa pamoja na kuhakikisha kunawekwa programu maalum za uzalishaiji wa maziwa hasa kwa wananchi ambao nao wanatakiwa kufaidika.

Alisema kuwa kwa upande wa uchumi wa buluu kipaumbele kitawekwa katika uvuvi wa bandari kuu sambamba na kutafuta masoko kwa bidhaa za wakulima mbali mbali nchini.

Kwa upande wa utalii, alisema kuwa bado sekta hiyo itakuwa na umuhimu hivyo, itapewa kipaumbele kwani ndio inayofaidisha nchi, ambapo utalii utaendelezwa kwa lengo la kuwanufaisha wananchi wa maeneo husika kwa upande wa bidhaa zao pamoja na kuwataka wawekezaji kuchangia katika maeneo wanayoekeza.

Aliongeza kuwa kipaumbele kitawekwa kwa vijana ili waweze kuajirika ambapo pia, wawekezaji watatakiwa kila kitu kinachozalishwa nchini ambacho kitasaidia katika kuendeleza sekta hiyo kinanunuliwa hapa na hakitoagizwa nje ya Zanzibar.

Alieleza kuwa juhudi zitafanywa katika kuzuia athari zinazotokana na utalii huku akieleza kuwa kuhusu dawa za kulevya mapambano ya dawa za kulevya yatapewa kipaumbele ili kuondoa athari ya matumizi kwa vijana.

Sambamba na hayo, kwa upande wa  miradi ya ufugaji wa samaki, Dk. Hussein aliahidi kuwa yatatolewa mafunzo na kutakuwa na utaratibu maalum wa kuhakikisha wanakijita ili kuhakikisha wananchi wa maeneo hayo yananufaika ili kuwaondolea umasikini..

Alisisitiza haja ya kuendeleza amani na utulivu nchini na kumuombea kura Rais Magufuli na mgombea mwenza wake, alijiombea kura yeye mwenywe, Wabunge, Wawakilishi na Madiwani wa CCM.

Mapema Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdalla Juma Mabodi alipongeza hatua anazozichukua mgombea urasi kwa tiketi ya CCM kuwa anatekeleza kwa vitendo agizo la Kamati Kuu ya CCM kwa kwenda mtaa kwa mtaa, kijiwe kwa kijiwe, makundi kwa makundi na  mtu kwa mtu kuomba kura.

Alisema kuwa CCM imetekeleza Ilani zake kwa asilimia mia na kuipongeza sana Awamu ya Saba pamoja na kumpongeza Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli kwa kufanya mazuri mengi yaliotukuka.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja Idd Ali Ame, alimpongeza Rais Dk. Shein kwa kutekeleza Ilani ya CCM ya mwaka 2015-2020, kwa kufanya mengi mazuri ikiwa ni pamoja na kujenga vituo vya afya, huduma za maji, umeme, elimu, barabara pamoja na kuimarisha sekta nyengine za maendeleo.

Nao wagombea wa Uwakilishi, Ubunge na Udiwani wa Wilaya ya Kaskazini B walitoa pongezi kwa Rais Dk. Shein kwa kujenga bandari ya mafuta katika eneo la Mangapwani katika Mkoa huo kwani hatua hiyo itaimarisha uchumi na kuleta ajira kwa vijana.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.