Habari za Punde

Tasaf Yafadhili Miradi ya Ujenzi wa Madarasa na Jengo la Utawala Skuli ya Sekondari Mahonda

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi  na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {Tasaf} Nd. Ladislaus Mwamanga wakifungua pazi kuashiria kuweka Jiwe la Msingi la Ofisi ya Utawala  pamoja na Jengo la Madasa Matatu la Skuli ya Sekondari ya Mahonda.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibare Mhe.Balozi Seif Ali Iddi akitoa maelezo kwa Wasimamizi wa Mradi wa Ujenzi wa Jengo la Utawala la Skuli ya Sekondari ya  Mahonda mara baada ya kuliwekea Jiwe la Msingi Jengo hilo pamoja na lile na  Madarasa Matatu.
Mkurugenzi wa Uratibu wa Shughuli za Serikali ya Mapinduz ya Zanzibar anayesimamia  Mradi wa Tasaf Zanzibar Nd. Khalid Bakar Amran akitoa maelezo ya ujenzi wa Miradi ya Elimu kwa Skuli ya Sekondari ya Mahonda inayosimamiwa na Mafuko wa Tasaf.
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania Ndugu Ladislaus Mwamanga akitoa maelezo ya Tasaf ilivyojipanga katika kuwahudumia Wananchi wa Kaya Maskini ndani ya Awamu ya Tatu ya Kipindi cha Pili cha Mfuko huo.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Shaaban Seif Mohamed akiwasisitiza Wananchi kuhakikisha Miradi wanayoianzisha katika maeneo yao wanaisamia wenyewe ili ilete tija.
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania Ndugu Ladislaus Mwamanga Kulia na Mkurugenzi wa Uratibu wa Shughuli za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar anayesimamia  Mradi wa Tasaf Zanzibar Nd. Khalid Bakar Amran Kushoto wakiteta kutafakari Hotuba ya Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akizungumza na Wananchi, Walimu na Wanafunzi wa Shehia za Mahonda na Mkataleni kwenye hafla ya Uwekaji wa Mawe ya Msingi ya Mradi wa Ujenzi wa Jnego la Madara Matatu na lile la Utawala la Skuli ya Sekondari ya Mahonda.
 Baadhi ya Wana Kamati ya Kusimamia Miradi ya Kijamii inayoibuliwa ndani ya Shehia za Mhaonda na Mkataleni wakifuatilia hafla ya uwekaji wa Mawe ka Msingi ya Ujenzi wa Majengo ya Darasa na Ofisi ya Utawala ya Skuli ya Sekondari ya Mahonda.Picha na – OMPR – ZNZ.  

Na.Othman Khamis.OMPR.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {Tasaf} umeonyesha muelekeo mzuri wa ufanisi mkubwa unaopatikana katika Utekelezaji wa Miradi ya Jamii tokea ulipoanzishwa ndani ya Awamu ya Tatu ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alisema Viongozi wa Wilaya, Halmashauri, Majimbo, Wadi pamoja na Shehia wana wajibu na jukumu la kuwasimamia vyema Wananchi katika kuona Miradi wanayoiibua katika Maeneo yao inaendelea kupata ufanisi kama inavyojidhihirisha hivi sasa katika mpango huo unaosaidia kustawisha Jamii.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na Wananchi wa Shehia za Mkataleni na Mahonda, Walimu na Wanafunzi mara baada ya kuweka Mawe ya Msingi ya Ujenzi wa Jengo la Madarasa Matatu pamoja na Jengo la Utawala la Skuli ya Sekondari ya Mahonda  Miradi inayofadhiliwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Yanzania {Tasaf}.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ililazimika kufanya mabadiliko katika ngazi ya Utawala kwenye Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tasaf  kwa upande wa Zanzibar ili kuona Taasisi hiyo ya Kijamii inatekeleza wajibu wake katika misingi iliyopangiwa ya kuunga mkono jitihada za Jamii kwenye Miradi yao ya Maendeleo.

Balozi Seif alibainisha wazi kwamba wapo baadhi ya Watendaji wa Tasaf  katika kipindi kilichopita walikuwa wakizorotesha kazi kwa kufikiria zaidi maslahi yao binafsi bila ya kujali kwamba chombo hicho kimeanzishwa kwa lengo la kuwakomboa Wananchi Kiuchumi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alielezea faraja yake kutokana na Uzalendo mkubwa wa Watendaji na Viongozi wa Mfuko huo  na kuwapongeza jinsi walivyojizatiti katika kusimamia Utekelezaji wa Miradi iliyobuniwa na Jamii inayokwenda kwa kasi katika maeneo mbali mbali Nchini.

“ Ni kiri kwa dhati Kwamba Majengo haya niliyoyawekea Mawe ya msingi hivi punde  yanaendelea kujengwa katika ubora unaokubalika katika fani ya Ujenzi na uharaka wake uliyofikia huwezi kuamini kama ni ya Mwezi Mmoja”. Alisisitiza Balozi Seif.

Alifahamisha kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Sera yake ya Elimu imejizatiti katika kuona Wanafunzi wote wa Visiwa vya Unguja na Pemba wanapata Taaluma katika mazingira bora na kiwango kinachokubalika Kitaifa na Kimataifa.

Akigusia Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Wiki chache zijazo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambae pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa aliwatahadharisha Wana CCM na Wananchi wote Nchini kujiepusha kuingia katika mtego wa kuuza Vitambulisho vyao vya kupigia Kura.

Balozi Seif alisema kitendo hicho ambacho mbali ya kumnyima  Mwananchi Haki yake ya Kidemokrasia kwa kuchagua Kiongozi anayefaa kumsimamia katika Maendeleo na kuuza Utu wake lakini baya zaidi ni kujihusisha na usaliti wa Taifa lake linalomtegemea wakati wote alilinde.

Mapema akisoma Risala ya Wanajamii wa  Shehia za Mahonda na Mkataleni Mjumbe wa Kamati ya usimamizi wa Ujenzi wa Majengo hayo Mawili ya Madarasa Matatu na Ofisi ya Utawala Nd. Madaraka Suleiman Haroun alisema ushiriki wa Wananchi katika Ujenzi huo umeleta faraja kubwa  licha ya kuwepo baadhi yao kuona mradi huo hauwahusu.

Nd. Madaraka alisema kukamilika kwa Miradi hiyo miwili kutasaidia kupunguza msongamano wa Wanafunzi na hata Walimu jambo ambalo litaongeza fursa za Masomo zitakazokwenda sambamba na ufaulu mkubwa utakaosaidia kurejesha Heshima ya Skuli hiyo.

Wakitoa Taarifa ya Utekelezaji wa Miradi ya Tasaf Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania Nd. Ladislaus Mwamanga na Mkurugenzi Uratibu wa Shughuli za Serikali Zanzibar anayesimamia Tasaf Zanzibar Nd. Khalid Bakari Amran walisema Zanzibar imepangiwa kupata Shilingi Bilioni 112 katika Kipindi cha Miaka Minne ijayo.

Walisema inafurahisha kuona  kwamba Zanzibar inaongoza katika Utekelezaji wa Miradi ya Tasaf Tanzania hasa kipindi hichi kilichoanza cha Tasaf  Awamu ya Tatu Kipindi cha Pili cha kuimarisha Kaya Maskini inayokwenda kwa kasi ya ajabu na kusababisha hata baadhi ya Mataifa ya kigeni yenye Miradi ya Kijamii kufika Zanzibar kujifunza mafanikio hayo.

Wakurgenzi hao walieleza kwamba hatua hiyo ya haraka ya ajabu inatokana na ushirikishwaji wa moja kwa moja wa Jamii inayopewa fursa ya kubuni na hatimae kuibua Miradi wanayoweza kuitekeleza bila ya vikwazo au changamoto zinazojichomoza mbele yao.

Walifahamisha kwamba Utekelezaji wa Mradi wowote wa Tasaf hupangiwa kukamilika ndani ya kipindi kisichozidi Miezi 12 lakini itashangaza kuona Miradi inayotekelezwa ndani ya Zanzibar haizidi katika kipindi cha Miezi Minne ikiwa ni mfano bora.

Ndugu Mwamanga na Nd. Khalid walieleza kwamba Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {Tasaf} umekuwa ukijibu kero za Wananchi katika maeneo yao na kuamini kwamba changamoto zote zinazojichomoza zitamalizika endapo ushirikiano wa pamoja utazingatiwa kwa pande zote husika.

Akimkaribisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwenye hafla hiyo ya Kijamii, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Shaaban Seif Mohamed aliwakumbusha Wananchi lazima wajizatiti katika kuisimamia Miradi yao.

Katibu Mkuu Shaaban alisema wao ndio dhamana wa Mradi yao waliyoianzisha huku wakielewa kwamba Watendaji wa Tasaf na wale wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar jukumu lao ni kuratibu mtiririko mzima wa Miradi hiyo katika kujiridhisha inatekelezwa na kukamilika.

Alitanabahisha kwamba Wapo Wananchi katika baadhi ya sehemu wamekuwa wakihitaji Miradi kama hiyo lakini bahati mbaya huchukuwa kipindi kirefu kuwafikia.

Mradi wa Ujenzi wa Jengo la Madarasa Matatu ya Skuli ya Sekondari Mahonda limepangia kugharimu zaidi ya Shilingi Milioni Sabini ya Saba Nukta Saba wakati lile Jengo la Utawala limetengewa kugharimu jumla ya Shilingi Milioni 78 Nukta Nane.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.