Habari za Punde

TCRA Kanda ya Kaskazini Kutoa Semina ya Uchaguzi Kwa Kundi la Wenye Mahitaji Maalum Kuaza Octoba 19.

Na Hamida Kamchalla, TANGA.

MAMLAKA ya udhibiti wa mawasiliano  nchini (TCRA) kanda ya kaskazini imejipanga kutoa semina kuhusu uchaguzi  mkuu wa mwaka huu kwa makundi ya watu wenye mahitaji maalumu katika mikoa yote ya kanda hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi jijini Tanga kwenye semina iliyowashirikisha waandishi wa habari wa kanda hiyo, mkuu wa Tcra kanda ya kaskazini Imelda Salum alisema kuwa mamlaka hiyo inawahusu wadau wote wa mawasiliano nchini bila kujali wako kwenye kundi la aina gani.

Alieleza kwamba kwa watu wenye mahitaji maalumu wa aina mbalimbali, mamlaka huwa inaandaa semina ambayo inawalenga wao pekee ili kuwajengea uwezo kwa kuwapa nafasi nzuri ya uelewa na hata kueleza changamoto zinazowakumba katika kipindi cha uchaguzi kutokana na uhalisia wao.

"Sisi kama mamlaka huwa tunaandaa semina ambazo zinawalenga wale wenye makundi maalumu pekee ili kuwajengea uwezo kwasababu tunafahamu kwamba sisi wengine ambao hatuna changamoto za kimaumbile tunapata nafasi nzuri zaidi ya kupata habari" alisema.

"Mamlaka imeandaa semina kuanzia wiki ijayo tarehe 19 kwa wasioona kwenye mikoa yote ya kanda yetu ya kaskazini, lengo ni kuhakikisha kuwa wenzetu wanapata fursa ya kipekee hata kama watapata taarifa kwenye vyanzo vingine huko kwenye jamii lakini tunapokuwa na semina au mikutano inayohusu makundi hayo pekee inakuwa ni nafasi yao nzuri kupokea zile taarifa na kueleza changamoto zao" aliongeza.

Aidha alibainisha kwamba mamlaka inatoa semina kwa vyombo vya habari ili kuhakikisha kwamba vinatunza ba kulinda amani, umoja na mshikamano wa nchi katika kipindi hiki ambacho kampeni zinamalizika, katika uchaguzi na hata kwenye kutangaziwa matokeo ya uchaguzi.

Alifafanua kwamba vyombo vya habari vimekuwa vikishirikiana  na taasisi nyingine mbalimbali katika kulinda amani nchini na mamlaka imetoa semina hiyo ili kuwajengea uwezo wanaotoa habari katika harakati za kuiweka na kulinda amani hiyo wakati huu na hata baada ya matokeo ya uchaguzi.

"Mamlaka inahakikisha kwamba vyombo vya habari vinahusika kwa namna chanya kwenye mchakato wa uchaguzi, kusiwepo na namna yoyote ambayo chombo cha habari kimetumika kwenye kupelekea taarifa ambazo zitaleta mtafaruku ama migongano kwenye jamii, alifafanua.

Hata hivyo alibainisha kwamba mojawapo ya malengo ya mamlaka kwa kutoa semina hiyo ni kuwakumbusha waandishi wa habari kuhusu kanuni mpya ya uchaguzi ya mwaka 2020 ambayo kwa namna moja au nyingine kupata au kutoa taarifa zenye mizania na zitakazolinda maslahi ya Taifa kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.