Habari za Punde

Waziri wa Katiba na Sheria Zanzibar Azindua Baraza la Nne la Ulamaa.

Waziri wa Katiba na Sheria Khamis Juma Maalim akitoa nasaha kwa maulamaa walioteuliwa kuwa wajumbe wa  Baraza la Ulamaa  Zanzibar huko  katika  Ukumbi  wa Wizara ya Katiba na Sheria Mazizini Zanzibar .
Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi akizungumza  na Wajumbe wa Baraza la Maulamaa (kushoto  )Waziri wa Katiba na Sheria Khamis Juma Maalim huko katika ukumbi wa Wizara ya Katiba na Sheria Mazizini Zanzibar .
Sheikh Jamal Mohammed akitoa neno la shukurani kwa niaba ya wajumbe wa Baraza la Ulamaa waliohudhuria katika uzinduzi wa Baraza la Nne la Ulamaa Zanzibar uliofanyika ukumbi wa Wizara ya Katiba na Sheria Mazizini Zanzibar .

Waziri wa Katiba na Sheria Khamis Juma Maalim akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe  wa Baraza la Nne la  ulamaa Zanzibar.
PICHA NA FAUZIA MUSSA/MAELEZO ZANZIBAR.

Na Khadija Khamis –Maelezo Zanzibar 18/10/2020

Waziri wa Katiba na Sheria Khamis Juma Maalim amewataka  Maulamaa walioteuliwa kuwa Wajumbe wa  Baraza la ulamaa Zanzibar  kufanya kazi kwa mashirikiano katika misingi ya dini ya kiislamu na kuweza kutoa haki na fatwa.

 

Ametoa kauli hiyo huko katika  Ukumbi wa Wizara ya Katiba na Sheria Mazizini, wakati wa Uzinduzi wa  Baraza la Nne la Ulamaa Zanzibar, amesema mashirikiano ya pamoja na upendo katika utendaji wa kazi ni jambo la msingi ambalo litasaidia kutekeleza majukumu yao.

 

Alifahamisha kuwa Ulamaa ni kazi nzito ambayo inahitaji hikma na busara kwa kuweza kujadili na kutatua migogoro pamoja na kuleta fatwa ambayo itaondosha mifarakano na kupata usuluhishi katika jamii .

 

Waziri huyo aliwataka Maulamaa kurithisha elimu ya dini ya kiislamu kwa vizazi vijavyo ili isipotee na kuisambaza kupitia vyombo vya habari pamoja na kuandika vitabu vya  dini iweze kuenea kwa jamii nzima.

 

Nae Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi alisema fatwa haitaki papara inahitaji fikra na busara katika kuamua jambo pindi likijitokeza jambo jipya ulimwenguni na kukosa  mfano wake katika vitabu na kurani, jambo hilo huhitaji kutatuliwa kwa kutumia hekma na busara pamoja na mazingatio makubwa.

 

“Suala la kutoa fatwa halihitaji hasira kwani pindipo kadhia  utaitoa bila ya kuzingatia jukumu lote litakuwa la mwenye kutoa fatwa”, alifahamisha Shekh Kabi .

 

Aidha aliwataka waulamaa hao kuliombea dua taifa liweze kuwa na amani na utuluivu hasa katika kipindi hichi cha uchaguzi mkuu .

 

Katibu wa Mufti Zanzibar Khalid Ali Mfaume alisema uwepo wa Baraza la Ulamaa kwa mujibu wa matakwa ya  sheria  ya Ofisi ya Mufti, kazi yake  kubwa  ni kumshauri Mufti  wa Zanzibar katika masuala mbali mbali yanayofikishwa kwake aidha kutolewa fatwa kutatua migogoro au usuluhisho na mengine yanayohusiana na uislamu .

 

Alieleza kuwa Baraza la Ulamaa lina kazi kubwa ya kutoa miongozo mbali mbali kwa misingi ya dini ya kiislamu yanayojitokeza katika jamii ili kuweza kusuluhisha na kutoa haki .

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.