Baadhi ya Wataalamu wa maradhi ya kisukari pamoja na waandishi wa habari wakimsikiliza Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa Mnazimmoja Ali Abdalla Ali (katikati) kuhusu vichocheo vya maradhi ya kisukari ambavyo hupata watoto ,vijana pamoja na watu wazima katika Maadhimisho ya Siku ya Kisukari Duniani huko Ukumbi wa Dodoma Mnazimmoja .
PICHA ZOTE NA KHADIJA KHAMIS MAELEZO ZANZIBAR .
Na Khadija Khamis – Maelezo Zanzibar
Mkurugenzi wa Hospitali ya Mnazimmoja Dk.Ali Salum Ali amesema hali ya maradhi ya kisukari inatisha kutokana na ongezeko kubwa la wagonjwa wapya.
Akizungumza katika kilele cha siku ya Kisukari Duniani katika ukumbi wa Hospitali ya Rufaa Mnazimmoja amesema kumekuwa na ongezeko la wagonjwa wapya wa kisukari 300 kila mwaka hapa Zanzibar kwa mujibu wa utafiti uliofanywa mwaka 2011 ambapo hivi sasa idadi imekuwa kubwa zaidi .
Aliwashauri wananchi kuwa na utamaduni wa kupima afya na kufanya mazowezi pamoja na kupata mlo kamili ikiwa ni pamoja na mbogamboga kwa wingi matunda na uwanga kidogo .
Aidha aliwashauri wananchi wenye maradhi ya kisukari kuacha tabia ya kutumia dawa za miti shamba ambazo hazina viwango na hazijathibitishwa.
Daktari Bigwa wa Magonjwa ya Kisukari Dk Faidha Kassim Suleiman amesema ongezeko la watoto wanaogunduliwa na kisukari ni watoto saba hadi kumi kwa mwezi na mtoto mmoja aligudulika na ugonjwa huo mara baada ya kuzaliwa.
Amesema takwimu inaonyesha kwa wauguzi 274 walifanyiwa vipimo hivi karibuni vinaonyesha asilimia 63..4 ya wauguzi hao wanauzito mkubwa 3.2 wanaviashiria vya sukari, 10.2 wanapresha na 30.3 wenye matatizo ya macho.
Nae Katibu wa Jumuiya ya Maradhi ya Kisukari Ali Zuber Juma alisema Jumuiya ya umoja wanaoishi na maradhi ya kisukari iliosajiliwa Zanzibar Novemba 26,2006 kwa lengo la kuwainua wagonjwa wa maradhi ya kisukari.
Pia jumuiya hiyo inatoa elimu kwa walioathirika na maradhi yasioambukiza pamoja na jamii juu ya namna ya kujikinga na maradhi ya kisukari na kuwapa njia sahihi ya matumizi ya chakula ikiwemo mboga mboga na matunda
Kila ifikapo Novemba 14 ya kila mwaka ni siku ya Kisukari duniani ujumbe wa mwaka huu ni Kauli mbiu ya mwaka huu ni “KISUKARI NA WAUGUZI”
No comments:
Post a Comment