Habari za Punde

Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Wapata Semina Elekezi

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) akiwaslisha Mada kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, wakati wa semina ya mafunzo Elekezi kwa Wajumbe ikuhusu mbinu ya Uwasilishaji wa Mijadala kwa njia ya mazungumzo, liofanyika katika ukumbi mdogo wa Baraza Chukwani Jijini Zanzibar. 
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Zanzibar Profesa Mohammed Makame Haji akiwasilisha Mada kuhusiana na Dhana ya Uwajibikaji wa Serikali mbele ya Baraza la Wawakilishi, wakati wa semina elekezi kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar iliofanyika katika ukumbi mdogo wa Baraza Chuwani Zanzibar. 
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar wakifuatila Mada mbalimbali zinazowakilishwa na Watoa Mada katika semina elekezi ya Majukumu ya Mjumbe wa Baraza wakati wa Kikao cha Baraza, iliofanyika katika ukumbi mdogo 

Na. Mwandishi Wetu.

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Zanzibar  Profesa  Mohammed Makame Haji amesema Uimara wa Baraza la Wawakilishi katika kusimamia  uwajibikaji utapelekea matatizo mengi yaliyozoeleka  kuyasikia kutokomezwa katika jamii na taifa kwa ujumla.

Amesema Baraza la Wawakilishi linadhima kubwa ya kutetea maslahi ya wananchi, hivyo  kuna  haja ya kila mjumbe wa Baraza hilo  kujitambua na kutimiza wajibu wake wa kikatiba kwa misingi ya uadilifu, uaminifu na usawa.

Baraza la Wawakilishi limebeba dhima kubwa ya kutetea na kusimamia maslahi ya kila mwananchi na kuhakikisha kuwa serikali pamoja wale wote waliopewa nyadhifa au madaraka ya kiutendaji wanatimiza wajibu wao kama ambavyo wanatakiwa kufanya. “ Alisisitiza.

“Ingawa uwajibikaji madhubuti sio suluhisho la kutatua changamoto zote ambazo serikali inakabiliwa nazo katika mazingira magumu, inaweza kuiboresha serikali kwa kiasi kikubwa katika utekelezaji wa kazi zake. “ Alisisitiza Profesa Makame.

Profesa Makameamesema hayo leo na wakati akitoa mada inayohusu dhana ya uwajibikaji wa Serikali mbele ya Baraza la Wawakilishi  katika Semina elekezi kwa wajumbe hao inayoendelea katika ukumbi wa Baraza hilo Chukwani.

Amesema mfumo sahihi wa uwajibikaji, utasaidia kwa kiasi kikubwa kuondokana na malamiko ya vitendo vya rushwa, ukiukwaji wa maadili na matumizi mabaya ya mabaraka.

Aidha Profesa Makame amesema wananchi kupitia Wawakilishi wao  wanawajibika kutoa maoni yao na kupatiwa maelezo kuhusu utendaji kazi wa maafisa wa maafisa wa kuchaguliwa na wasiochaguliwa na inapobidi wanashauri hatua za kuchukuliwa kwa maofisa wanaoshindwa kutekeleza majukumu yao kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji.

Wakati huo huo Profesa Makame amewashauri wawakilishi hao kutekeleza mkataba wao na wananchi kwa kujipanga kutimiza ahadi walizokubalina  ili kuepusha manunguniko watakaporudi tena kuomba ridhaa kwa wananchi kipindi chengine.

Katika hatua nyengine Wajumbe hao wa Baraza la Wawakilishi wamehimizwa kuwa na uteuzi mzuri  na sahihi wa maneno ili kujiepusha na makosa mbali yanayofanywa katika matumizi ya lugha ya Kiswahili.

Akiwasilisha mada inayohusu Mbinu za Uwasilishaji wa Mjadala kwa njia ya lugha ya Mazungumzo Mhadhir kutoka Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar Maalim Amour Khamis amesema ni vyema mijadala ya wajumbe hao ikajikita katika kujenga umoja na mshikamano na sio kuibua chuki na mipasuko ndani ya jamii.

Imetolewa na

Divisheni ya Itifaki na Uhusiano, BLW

November 14, 2020

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.