Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla Azungumza na Mwakilishi wa Kampuni ya Arena

Mwakilishi wa Kampuni ya Kimataifa ya Arena yenye Makao Makao Makuu yake Nchini Ujerumani inayojishughulisha na Miradi ya Uwekezaji katika Sekta ya Nishati ya Umeme Bwana Souheil Freich Kushoto akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla alipofika kuwasilisha hisia zake za kutaka kuwekeza Nchini.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdallah akizihakikishia Taasisi za Uwekezaji za ndani na nje ya Nchini kutumia fursa ya Uwekezaji inayosisitizwa na Serikali Kuu.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Na.Othman Khamis OMPR.

Uongozi wa Kampuni ya Kimataifa ya Arena yenye Makao Makao Makuu yake Nchini Ujerumani inayojishughulisha na Miradi ya Uwekezaji katika Sekta ya Nishati ya Umeme imeonyesha nia ya kutaka kuwekeza Miradi yake Visiwani Zanzibar baada ya kuridhika na mazingira mazuri yaliyopo ya Uwekezaji.

Mwakilishi wa Kampuni hiyo Bwana Souheil Freich aliyeambatana na Uongozi wa Kampuni ya Flagfin yenye Makao Makuu yake Jijini Dar es salaam alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdalla hapo Vuga Mjini Zanzibar.

Bwana Souheil Freich alisema alikuwa akifuatilia harakati za Sera na Ilani za Uchaguzi Mkuu uliopita na kuridhika nazo kitendo kilichoipa ushawishi Kampuni yake kutaka kuitumia nafasi ya Uwekezaji ndani ya ardhi ya Tanzania.

Alisema uwepo wake umemthibitishia kwamba mazingira ya Uwekezaji yaliyopo Tanzania Bara na Zanzibar yanastahiki kutumiwa na Wawekezaji wenye nia thabiti ya kutaka kuzisaidia Jamii katika maeneo husika kulingana na Miradi itakayoanzishwa.

Mwakilishi huyo wa Kampuni ya Kimataifa ya Arena alimueleza Mh. Hemed kwamba Taasisi yake ya uwekeza tayari imeshabobea katika fani ya Uwekezaji kwenye masuala ya Nishati ya Umeme wa jua pamoja na Taaluma ya utengenezaji wa Mbolea ambayo inaweza kuifaidisha Zanzibar endapo itapata fursa ya kutoa mchango wake.

Akitoa nasaha zake kwa Uongozi wa Kampuni hiyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdalla alisema ujio wa Wawekezaji tofauti Nchini ni ishara ya kuunga mkono kasi ya Serikali katika Mipango yake ya Kuimarisha Uchumi.

Mh. Hemed aliuhakikishia Uongozi huo kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inahitaji utaratibu na Sheria katika kuona Wawekezaji hao wanakamilisha maombi yao kwa vile kamwe hakutakuwa na ubabaishaji ili kuona kasi ya Uwekezaji inaimarika Zaidi kwa kuondosha urasimu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alibainisha kwamba wapo baadhi ya Wawekezaji waliowahi kuonyesha nia ya kutaka kuwekeza Miradi yao Nchini lakini wakakata tamaa baada ya usumbufu walioupata uliosababishwa na ubinafsi wa baadhi ya Watendaji wa Taasisi za Umma.

Mheshimiwa Hemed alieleza kwamba Uwekezaji ndio eneo sahihi lenye nguvu kubwa ya kuongeza fursa za Ajira hasa kwa Vijana waliomaliza masomo zinazokwenda  sambamba na kuimarika kwa mapato yatakayofaidisha Taifa na Wawekezaji wanaohusika.

Aliuomba Uongozi wa Makampuni yao ya Uwekezaji kutoka Ujerumani na Dar es salaam kwa Taaluma zao kuangalia zaidi Miradi wanayoweza kuianzisha akitolea mfano ile iliyomo katika Sekta ya Viwanda vidogo vidogo na vikubwa pamoja na huduma za Maji safi na salama.

Kampuni ya Kimataifa ya Arena tayari imeshatia saini moja ya Mikataba ya kuendesha shughuli za Mgodi ikiwa njiani kuweka saini Mkataba mwengine hivi karibuni katika jitihada za kuwekeza Miradi yake Nchini Tanzania.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.