Habari za Punde

Mawaziri wa SMZ Waahidi Utekelezaji wa Majukumu ya Kazi Zao Kwa Wananchi

 
MAWAZIRI wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, wameahidi kutekeleza kwa vitendo Ilani ya Uchaguzi wa CCM ya 2020-2025, ahadi zilizotolewa na Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi wakati wa kampeni pamoja na maelekezo  yaliomo katika hotuba aliyoitowa katika ufunguzi wa Baraza la Wawakilishi;  Novemba 11, mwaka huu.

Wakizungumza na vyombo mbali mbali vya habari, baada ya hafla ya kuapishwa Ikulu jijini Zanzibar, Mawaziri hao wamesema wataweka mikakati imara na kuwa wabunifu katika usimamizi wa majukumu hayo, ili kuimarisha uchumi pamoja na kuwandolea kero wananchi, hususan katika suala la upatikanaji wa huduma.

Waziri wa Nchi (OR) Katiba,Sheria,Utumishi na Utawala Bora Haroun Ali Suleiman alisema ataendeleza juhudi zilizoanzishwa katika Serikali ya Awamu ya saba ili kufanikisha mapambano dhidi ya rushwa.

Aidha, Waziri wa Nchi (OR) Fedha na Mipango Jamal Kassim Ali alisema ataweka mikakati mizuri katika ukusanyaji wa mapato pamoja na kusimamia matumizi mazuri ya fedha za Serikali.

Nae, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais Sera,Uratibu na Baraza la Wawakilishi Dk. Khalid Salum Mohamed alisema atahakikisha Fedha za mfuko wa Maendeleo ya Jimbo zinatumika vyema na kwa utaratibu uliowekwa ili ziweze kuleta tija katika mqendeleo ya wananchi.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Simai Mohamed Said alieleza kuwa atatumia uwezo wote alionao pamoja na ubunifu katika kukabiliana na changamoto mbali mbali ndnai ya sekta hiyo, ikiwemo uhaba wa madarasa ya kusomea pamoja na kuwataka wazazi na walezi kusimamia maendeleo ya elimu ya watoto wao.

Katika hatua nyengine, Waziri wa Nchi (OR) Tawala za Mikoa na Idara maalum za SMZ Masoud Ali Mohamed alisema huu ni wakati muafaka kwa Vikosi vya Serikali ya Zanzibar kufanya kazi zaidi za uzalishaji mali, akibainisha kuwepo kwa ardhi ya kutosha itakayoweza kufanikisha azma hiyo.  

Aidha, Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Riziki Pembe Juma, akabainisha namna Wizara hiyo itakavyoandaa mikakati madhubuti katika kuliendeleza eneo la ardhi lilioko Bagamoyo Mkoa wa Pwani, linaloimilikiwa na Serikali ya Zanzibar.

“Nitasimamia mikakati katika kuimarisha sekta ya Utalii kisiwani Pemba kwa kutumia vyanzo mbali mbali vya utalii, kama kilivyoainishwa katika Dira ya 2020-2050”, alisema Lela Mohamed Mussa, Waziri wa Utalii na mambo ya kale.

 

Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 

 E-mail: abdya062@gmail.com

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.