Habari za Punde

Naibu Katibu Mkuu Fedha na Mipango Zanzibar Aahidi Mabadiliko Makubwa na Huduma Bora kwa Kutumia Teknolojia ya TEHAMA

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa   Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (kushoto) akimuapisha Nd.Rashid Said Rashid   kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango anayeshuhulikia masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika hafla iliyofanyika  leo ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Hussein Ali Hassan Mwinyi leo amemuapisha Rashid Said Rashid kuwa Naibu Katibu Mkuu anaeshughulikia mifumo ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) katika Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango.

Hafla ya kuapishwa kiongozi huyo ilifanyika Ikulu Jijini  Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar akiwemo Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Jamal Kassim Ali, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Dk. Mwinyi Talib Haji,  Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee na Makatibu Wakuu. 

Wengine ni Naibu Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh  Hassan Othman Ngwali, Katibu wa Mufti Sheikh Khalid Ali Mfaume, Mkuu wa  Wilaya ya Mjini Marin Joel Thomas, Wakuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama pamoja na viongozi wengine wa Serikali na wanafamilia.

Katika maelezo yake mara baada ya kula kiapo Naibu katibu Mkuu huyo alieleza ambaye pia atakuwa anashughulikia masuala ya fedha na kodi alisema kwamba wananchi wanamatumaini makubwa na mabadiliko kwani wanahitaji kupata huduma nzuri na zilizo bora zaidi.

Alisisitiza kwamba teknolojia ya TEHAMA haitokuwa kwenye kodi pekee yake na badala yake itakwenda kwenye kila sekta ikiwemo uchumi wa buluu, huduma za afya, elimu na nyenginezo.

Aidha, alisema kuwa ipo haja ya kutumia teknolojia katika kutatua matatizo ya walimu na kusema kwamba Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kina uwezo mkubwa wa kufanya hivyo lakini kwa kuanzia alisema kuwa hatua hiyo itaanza katika ukusanyaji wa kodi kama alivyosisitiza Rais Dk. Mwinyi.

Alisema kwamba lengo la Serikali ni kuhakikisha wananchi walipe kwa urahisi zaidi na kuepuka wananchi kwenda kulipa benki na kukaa muda mrefu ni lazima iondolewe ikiwa ni pamoja na kupata wepesi katika kufuatia masuala ya vyeti vya kuzaliwa.

Aliongeza kwamba Serikali itajipanga katika kuhakikisha wahitimu wa vyuo vya Zanzibar wanapata muelekeo kwa kuwatumia hapa hapa nchini na hakuna haja ya kuwaita wataalamu kutoka nje jambo ambalo litafanywa haraka iwezekenavyo ili kuondoa tatizo la walimu hasa wa sayansi.

Naibu Katibu Mkuu huyo alitangazwa siku ya Jumanne ya tarehe 22 Novemba 2020 ambapo Rais Dk. Mwinyi alifanya uteuzi huo kwa mujibu wa kifungu cha 50(4) cha katiba ya Zanzibar.

Kabla ya uteuzi huo Naibu Katibu Mkuu huyo alikuwa Mkurugenzi wa Mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika benki kuu ya Tanzania, ambapo uteuzi wake ulianza rasmi Novemba 23 mwaka huu.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.