Habari za Punde

Watu Milioni 15 hufa kwa maradhi yasiyoambukiza kila mwaka duniani

Na Khadija Khamis /Maelezo Zanzibar.

Zaidi ya Watu milioni 15 Wenye umri kati ya miaka 30 hadi 69 wanakufa kila mwaka Duniani kutokana na maradhi yasioambukiza.

 

 Akifungua mafunzo ya siku moja kwa Waandishi wa Habari katika Ukumbi wa malaria Mwanakwerekwe, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maradhi Yasioambukiza, Dk. Said Gharib Bilali amesema vifo hivyo vinachangiwa na  mfumo wa kileo wa utumiaji wa vyakula katika jamii.

 

“Ni muhimu jamii kuyatambua maradhi yasioambukiza na visababishi vyake,njia ya kuyaepuka na kutumia mfumo sahihi wa ulaji wetu,  na tuwe na desturi ya kufanye mazowezi angalau kwa dakika 30 kwa kila siku,”alisema Dkt Said .

 

Amesema wakati umefika kwa jamii kutambua uwepo wa Maradhi yanayoambukiza na yasiyoambukiza na uwiano wa  maradhi hayo ambayo huathiri zaidi jamii kutokana na  kushuka kwa kiwango cha kinga mwilini.

 

Akiwasilisha Mada juu ya  Maradhi yasiombukiza,Mkuu wa Idara ya Maradhi ya Watu Wazima  Dr. Yussuf Ameir Haji kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja alisema Maradhi Yasioambukiza  hayana dalili husika pindi yanapompata mwanaadamu na hupelekea kuwepo na vichocheo vingi vya upatikanaji wa Maradhi hayo.

 

Amefahamisha kuwa ni vyema jamii kuyapa kipaumbele Maradhi hayo kwa kuwepo kwa utamaduni wa upimaji wa Afya ili kuweza kutambua mwenendo wa Afya pamoja na kuchukua hatua madhubuti ya kuyadhibiti.

 

Meneja kutoka Kitengo cha Maradhi Yasioambukiza  Nd. Omar Abdulla  amesisitiza ulaji wa mlo kamili kwa kupunguza matumizi ya Uwanga kwa wingi.

 

Alifahamisha kuwa  Maradhi Yasiombukiza husababishwa kwa asilimia 99 kutokana na ulaji wa uwanga wingi ,na kuathiri waliowengi kwa kupoteza maisha na kupoteza viungo mbali mbali vya mwili ikiwemo kupofua macho.

 

“Maradhi ya Kisukari na Saratani humuweka mtu katika hatari ya kupoteza viungo vya mwili ikiwemo presha ambayo husababisha ugonjwa wa kupooza”

 

Dkt Omar alifahamisha kuwa  Maradhi yasioambukiza huchukua muda mrefu kuugua wala Hayatibiki Bali hupatiwa matibabu ya kupunguza kasi ya Maradhi Hayo.

 

Nae Mwandishi  wa Habari Mwandamizi Bw. Ali Sultani amevitaka vyombo vya Habari kutoa elimu stahiki juu ya maradhi hayo kwa jamii ili wapate uwelewa wa kujinusuru kuingia katikam hatari ya maradhi yasioambukiza .

 

Alisema jamii ikipata uwelewa wa matumizi bora ya ulaji wataweza kubadilisha mfumo wa maisha yao kwa kutumia mboga mboga na matunda kwa wingi na uwanga kidogo kwa kujinusuru na hatari ya kupaa maradhi hayo .

 

Hata hivyo aliwataka Waandishi hao kufanya kazi kwa kufuata maadili ya uwandishi ikiwemo kuandika taarifa sahihi na zenye data za uhakika ambazo zimetolewa na  Taasisi husika zenye mamlaka ya kutoa taarifa .

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.