Habari za Punde

WIZARA YA ARDHI YAWASHUKIA WASIOENDELEZA VIWANJA NA KULIPIA KODI YA ARDHI

Mkuu wa Kitengo cha Kodi Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Denis Masami (katikati) na Afisa kutoka kitengo cha Kodi Wizarani Kija Duda (kulia) wakiagana na mmoja wa wamiliki wa ardhi katika eneo la Chidachi Faustine Mwakalinga wakati wa zoezi la kupita nyumba kwa nyumba  kuhamasisha ulipaji kodi ya pango la ardhi mwishoni mwa wiki.

Wataalamu wa sekta ya ardhi katika ofisi za ardhi za mkoa na jiji la Dodoma wakiingia mitaani kuanza zoezi la kupita nyumba kwa nyumba katika mtaa wa Chidachi jijini Dodoma kuhamasisha ulipaji kodi ya pango la ardhi mwishoni mwa wiki.

Mkuu wa Kitengo cha Kodi Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Denis Masami (kulia) na wataalamu wengine wakichukua mawasiliano kutoka kwa kijana aliyemkuta katika nyumba iliyopo eneo la Chidachi jijini Dodoma wakati wa zoezi la kupita nyumba kwa nyumba kuhamasisha ulipaji kodi ya pango la ardhi mwishoni mwa wiki.

Wataalamu wa sekta ya ardhi katika ofisi za ardhi za mkoa na jiji la Dodoma wakiingia katika gari kuanza zoezi la kupita nyumba kwa nyumba katika mtaa wa Chidachi jijini Dodoma kuhamasisha ulipaji kodi ya pango la ardhi mwishoni mwa wiki.

 


Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA

Wizara ya ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imetoa rai kwa wamiliki wote wa ardhi walio na viwanja visivyoendelezwa na kulipiwa kodi ya pango la ardhi kuhakikisha wanalipia viwanja vyao ndani ya siku kumi na nne baada ya kupokea ankara ya madai na wasipotekeleza watanyanganywa viwanja vyao na kupatiwa watu wengine.

 

Rai hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki na Mkuu wa Kitengo cha Kodi Wizara ya Ardhi Denis Masami wakati wa zoezi la kuhamasisha ulipaji kodi ya pango la ardhi katika mtaa wa Chidachi jijini Dodoma ikiwa ni Mkakati wa Wizara kuhakikisha wamiliki wote wa ardhi wanalipa kodi ya pango la ardhi kwa wakati.

 

Alisema, Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia ofisi zake za ardhi za mikoa imeanzisha utaratibu wa kuwatembelea wamiliki wa ardhi kila mwisho wa wiki kwa lengo la kuhamasisha ulipaji kodi na kutoa elimu ili kuwawezesha wamiliki wa ardhi nchini kutekeleza jukumu hilo bila shuruti.

 

‘’Maeneo mengi nchini yana viwanja visivyoendelezwa na wakati huo wamiliki wake hawavilipii kodi ya pango la ardhi jambo linaikosesha mapato serikali, baada ya siku kumi na nne tutaanza utaratibu wa kuzitwaa, kuvinadi ili kufidia deni na kumilikishwa kwa watu wengine’’ alisema Masami.

 

Mkuu huyo wa Kitengo cha Kodi Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliongeza kwa kusema, Wizara ya Ardhi inatekeleza mkakati wake wa kuhamasisha ukusanyaji kodi ya pango la ardhi kwa kushirikisha wataalamu wa sekta ya ardhi na Makamishna Wasaidizi wa ardhi katika mikoa kwa kupita nyumba kwa nyumba na kuwapelekea wadaiwa Ankara za madai ya ulipaji kodi ya pango la ardhi na maduhuli mengine yatokanayo na sekta ya ardhi ili waweze kulipa.

 

Akiwa eneo la Chidachi jijini Dodoma na timu yake, Masami alibaini maeneo kadhaa yasiyoendelezwa na wamiliki wake kudaiwa kodi ya pango la ardhi sambamba na ukubwa wa eneo la shule ya St Merys Dodoma kuonesha kuwa na ukubwa wa Square mita 900 wakati uhalisia ni hekta 3.5 jambo alilolieleza kuwa limeifanya shule hiyo kulipia kiasi kidogo cha kodi ya pango la ardhi.

 

Kwa upande wake Afisa Ardhi wa Jiji la Dodoma Ruta Rwechugura alisema, wakati wa zoezi la kuwafuatilia wadaiwa wa kodi ya pango la ardhi walibaini kukiukwa kwa baadhi ya taratibu na wamiliki wa ardhi na kutolea mfano ubadilishaji matumizi ya umiliki sambamba na baadhi ya wananchi kuuziana viwanja bila kubadilisha jina.

 

Aliwataka wamiliki wote wa ardhi walionunua viwanja kwenye maeneo mbalimbali nchini kuhakikisha wanabadilisha umiliki kwa kufika ofisi za ardhi katika halmashauri husika ili kuiweka ardhi yao salama na kuwasisitizia wamiliki kutobadili matumizi ya kiwanja vyao bila kufuata taratibu.

 

Hata hivyo, wakati wa zoezi la kuwafikia wadaiwa wa kodi ya ardhi mmoja wa wananchi aliyefikiwa na zoezi hilo Faustine Mwakalinga aliipongeza Wizara Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa uamuzi wake wa kuwafikia wamiliki wa ardhi kwa lengo la kutoa elimu na kuhamasisha ulipaji kodi ya ardhi na kuuelezea kuwa utaratibu huo unapaswa kuigwa na watendaji wengine wa  serikali katika kudai kodi kwani ni utaratibu ulio rafiki na unamhamasisha mdaiwa kulipa badala ya kuogopa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.