Habari za Punde

Maendeleo ya Michezo Yatafikiwa Kuwepo na Udhamini -Dk.Mwinyi.

 


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ameitaka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kuhakikisha Vyama vya Michezo vinakuwa na utaratibu maalum utakaowezesha wafanyabaishara kujitokeza na kudhamini michezo hiyo.

Dk. Mwinyi amesema hayo Ikulu Jijini Zanzibar, katika hafla ya makabidhiano ya fedha zilizotolewa na Wafanyabiashara watano wa Zanzibar kwa ajili ya ushiriki wa Timu ya Mlandege, kuelekea mchezo wa marudiano dhidi ya Timu ya CS Sfaxien ya Tunisia.

Alisema maendeleo ya michezo hapa nchini yatafikiwa kwa kuwepo udhamini  wa uhakika utakaozinufaisha pande zote mbili kati ya wafanyabaishara na vilabu.

Aliwataka wafanyabiashara kote nchini kujitokeza kusaidia maendeleeo ya michezo, ikiwemo soka ili kurejesha hadhi ya mchezo huo iliyopotea.

Alisema kwa njia yoyote ile Taifa lina dhima ya kuhakikisha michezo inaimarika na kubainisha kuwa kamwe jambo hilo haliwezi kufikiwa bila ya kuwepo ufadhili ambapo  Makampuni kwa utaratibu maalum yataweka fedha katika bajeti zao.

Dk. Mwinyi alisitiza umuhimu wa Wizara hiyo kusimamia  mashindnao mbali mbali, akisema jambo hilo lina faida kubwa katika maendeleo ya michezo, kwa kigezo kuwa huongeza hamasa, kuinua kipato pamoja na kukuza utalii nchini.

Aidha, aliitaka Wizara hiyo kuendelea na juhudi za kutengeneza viwanja kila mahali, ili kuondokana na utaratibu wa timu kupokezana viwanja.

Dk. Mwinyi alisisitiza azma ya vyama vya michezo kukaa na wadau, ili kujenga mashirikiano na maelewano kati ya vyama vya michezo na vilabu pamoja na wadau kwa ujumla.

Alisema hivi sasa maelewano kati ya Viongozi wa ZFF na vilabu Unguja na Pemba hayako sawa, sambamba na kuwepo tatizo kubwa la ukosefu wa fedha za kuendeshea mashindano.

Dk. Mwinyi aliwashukuru wafanyabiashara hao kutoka kampuni mbali mbali hapa Zanzibar kwa uzalendo wao wa kusaidia fedha zitakazoiwezesha timu ya Mlandege kugharamia safari ya kuelekea nchini Tunisia.

“……..nawashukuru kwa kuokoa hili jahazi……….hili jambo mlilolifanya ni la kizalendo sana…………”, alisema.

Mapema, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Tabia Mwita Maulid aliahidi kukaa na wadau ili kuimarisha maendeleo ya michezo nchini pamoja na maandalizi ya kufanikisha Kombe la Mapinduzi la 2021, kwa dhamira ya kurejesha hamasa na imani kwa wananchi.

Nae, Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Omar Hassan Omar ‘King’ aliishukuru Serikali kwa wito wake wa kuitaka Wizara hiyo kuwakutanisha na wadau wa michezo ili kufanikisha safari ya Timu ya Mlendege kuelekea nchini Tunisia.

Pamoja na mambo mengine, akigusia kushuka kwa michezo nchini, alisema  kwa kipindi kirefu Zanzibar imekuwa ikikabiliwa na changmoto ya miundombinu ya michezo na ndio maana  Chama cha Mapinduzi katika Ilani yake ikaazimia  umuhimu wa  kujenga viwanja katika Wialaya zote Unguja na Pemba.

Alisema mfumo wa uendeshaji wa mpira wa miguu nchini nao uligubikwa na changamoto kubwa ya kuwa na idadi kubwa ya timu zinazoshiriki katika Ligi Kuu ya Zanzibar, jambo lisiloendana na maelekezo ya Shirikisho la Soka Afrika  (CAF).

Alisema kuwepo kwa timu 36 zinazoshiriki Ligi Kuu ya Zanzibar, hakuwezi kuwashajiisha wadhamini kuwekeza katika mpira   hapa nchini.

Aidha,  King alisema kuna changamoto ya mfumo wa   kiutawala  katika uendeshaji wa vyama vya michezo ikiwemo  ZFF ambapo katiba yake inapswa kuwa na sifa zinazoendana na vyama vya soka vya nchi nyengine zilizo wanachama wa FIFA.

Nao, wafanyabiashara waliofadhili fedha hizo, walisema kuna umuhimu mkubwa wa kuwashirikisha wadau wa michezo katika kila hatua ili kufanikisha maendeleo ya michezo nchini, ikiwemo soka.

Walisema  mchezo wa soka uliopata umaarufu  mkubwa hapa nchini katika miaka iliopita, umepoteza hadhi na hamasa kutokana an sababu mbali mbali, ikiwemo kutokuwepo ushirikishwaji wa wadau pamoja na mfumo mbaya wa uendeshaji.

Walisema moja ya changamoto kubwa inayokwaza maendeleo ya soka nchini ni kwa Shirikisho la mchezo huo nchini (ZFF) kushindwa kukaa pamoja na vilabu  na kushirikiana katika masuala mbali mbali ya kuendeleza mchezo huo pamoja na utatuzi wa changamoto ziliopo.

Aidha, walisema  miongoni mwa matatizo makubwa yanayovikabili vilabu kote nchini, hususan vile vilivyoko daraja la kwanza ni ukosefu wa viwanja vya mazoezi.

“Vilabu vina matatizo mengi, pamoja na Mlandege kuwa na historia nzuri ya kuchukua makombe, haina kiwanja chake”, alisema mmoja wa wafanyabiashara hao.

Waliomba Serikali kuweka utaratibu mzuri wa matumizi ya viwanja vyake, ili kila timu iweze kupata fursa ya kuvitumia kwa mazoezi badala ya kuhodhiwa na timu maalum kama milki yake.

Aidha, walieleza haja ya ZFF  kuangalia uwezekano wa kubadili mfumo wa uendeshaji ligi kwa timu za Vikosi kwa kuwa na timu moja, hatua itakayoziinua timu za kiraia ambazo ndio zenye mashabiki wengi.

Walisema ushiriki wa timu za kiraia, kama ilivyo sasa katika michuano ya ‘ndondo na yamle yamle’ utaibua hamasa na kuleta ushindani mkubwa kama ilivyokuwa miaka iliyopita.

Wafanyabiashara hao waliahidi kuendelea kushirikiana na Serikali na vyama vya michezo ili kuendeleza michezo mbali mbali nchini, wakibainisha hatua hiyo itawaweka vijana katika maadili mema na kuondokana na vitendo viovu, ikiwemo utumiaji wa dawa za kulevya.

Walimuomba Waziri anaehusika na michezo kuendelea kushirikiana nao na kubainisha utayari wao katika kusaidia maendeleo ya michezo mbali mbali nchini.

Aidha, akitoa shukrani, Mkurugenzi wa Klabu ya Mlandege Ali Khatibu Dai  aliwashukuru wafanyabiashara hao kwa kujitolea  kufanikisha safari ya Timu hiyo kuelekea nchini Tunisia katika pambano la marudiano dhidi ya timu ya CS Sfaxien.

Alisema miongoni mwa athari kubwa ambayo Klabu ya Mlandege  ingekabiliana nayo  kwa kushindwa kushiriki katika mchezo huo wa marudiano ni kufungiwa na CAF, na hivyo kuliletea aibu Taifa.

Jumla ya US Dola 34, 000 zimechangwa na wafanyabaishara hao watano kutoka Zanzibar.

Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 

 E-mail: abdya062@gmail.com

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.