STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS
SECRETARY
PRESS
RELEASE
Zanzibar Disemba 02, 2020.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ameitaka Wizara ya Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo kuhakikisha Vyama vya Michezo vinakuwa na utaratibu maalum
utakaowezesha wafanyabaishara kujitokeza na kudhamini michezo hiyo.
Dk. Mwinyi amesema hayo
Ikulu Jijini Zanzibar, katika hafla ya makabidhiano ya fedha zilizotolewa na
Wafanyabiashara watano wa Zanzibar kwa ajili ya ushiriki wa Timu ya Mlandege,
kuelekea mchezo wa marudiano dhidi ya Timu ya CS Sfaxien ya Tunisia.
Alisema maendeleo ya michezo hapa
nchini yatafikiwa kwa kuwepo udhamini wa
uhakika utakaozinufaisha pande zote mbili kati ya wafanyabaishara na vilabu.
Aliwataka wafanyabiashara kote nchini
kujitokeza kusaidia maendeleeo ya michezo, ikiwemo soka ili kurejesha hadhi ya
mchezo huo iliyopotea.
Alisema kwa njia yoyote ile Taifa lina
dhima ya kuhakikisha michezo inaimarika na kubainisha kuwa kamwe jambo hilo
haliwezi kufikiwa bila ya kuwepo ufadhili ambapo Makampuni kwa utaratibu maalum yataweka fedha
katika bajeti zao.
Dk. Mwinyi alisitiza umuhimu wa Wizara
hiyo kusimamia mashindnao mbali mbali,
akisema jambo hilo lina faida kubwa katika maendeleo ya michezo, kwa kigezo
kuwa huongeza hamasa, kuinua kipato pamoja na kukuza utalii nchini.
Aidha, aliitaka Wizara hiyo kuendelea
na juhudi za kutengeneza viwanja kila mahali, ili kuondokana na utaratibu wa
timu kupokezana viwanja.
Dk. Mwinyi alisisitiza azma ya vyama
vya michezo kukaa na wadau, ili kujenga mashirikiano na maelewano kati ya vyama
vya michezo na vilabu pamoja na wadau kwa ujumla.
Alisema hivi sasa maelewano kati ya
Viongozi wa ZFF na vilabu Unguja na Pemba hayako sawa, sambamba na kuwepo
tatizo kubwa la ukosefu wa fedha za kuendeshea mashindano.
Dk. Mwinyi aliwashukuru
wafanyabiashara hao kutoka kampuni mbali mbali hapa Zanzibar kwa uzalendo wao
wa kusaidia fedha zitakazoiwezesha timu ya Mlandege kugharamia safari ya
kuelekea nchini Tunisia.
“……..nawashukuru kwa kuokoa hili
jahazi……….hili jambo mlilolifanya ni la kizalendo sana…………”, alisema.
Mapema, Waziri wa Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo Tabia Mwita Maulid aliahidi kukaa na wadau ili kuimarisha
maendeleo ya michezo nchini pamoja na maandalizi ya kufanikisha Kombe la
Mapinduzi la 2021, kwa dhamira ya kurejesha hamasa na imani kwa wananchi.
Nae, Katibu Mkuu Wizara ya Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo Omar Hassan Omar ‘King’ aliishukuru Serikali kwa
wito wake wa kuitaka Wizara hiyo kuwakutanisha na wadau wa michezo ili
kufanikisha safari ya Timu ya Mlendege kuelekea nchini Tunisia.
Pamoja na mambo mengine, akigusia kushuka
kwa michezo nchini, alisema kwa kipindi
kirefu Zanzibar imekuwa ikikabiliwa na changmoto ya miundombinu ya michezo na
ndio maana Chama cha Mapinduzi katika
Ilani yake ikaazimia umuhimu wa kujenga viwanja katika Wialaya zote Unguja na
Pemba.
Alisema mfumo wa uendeshaji wa mpira
wa miguu nchini nao uligubikwa na changamoto kubwa ya kuwa na idadi kubwa ya timu
zinazoshiriki katika Ligi Kuu ya Zanzibar, jambo lisiloendana na maelekezo ya
Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Alisema kuwepo kwa timu 36 zinazoshiriki
Ligi Kuu ya Zanzibar, hakuwezi kuwashajiisha wadhamini kuwekeza katika mpira hapa nchini.
Aidha,
King alisema kuna changamoto ya mfumo wa
kiutawala katika uendeshaji wa vyama vya michezo ikiwemo ZFF ambapo katiba yake inapswa kuwa na sifa
zinazoendana na vyama vya soka vya nchi nyengine zilizo wanachama wa FIFA.
Nao, wafanyabiashara waliofadhili
fedha hizo, walisema kuna umuhimu mkubwa wa kuwashirikisha wadau wa michezo
katika kila hatua ili kufanikisha maendeleo ya michezo nchini, ikiwemo soka.
Walisema mchezo wa soka uliopata umaarufu mkubwa hapa nchini katika miaka iliopita,
umepoteza hadhi na hamasa kutokana an sababu mbali mbali, ikiwemo kutokuwepo
ushirikishwaji wa wadau pamoja na mfumo mbaya wa uendeshaji.
Walisema moja ya changamoto kubwa inayokwaza
maendeleo ya soka nchini ni kwa Shirikisho la mchezo huo nchini (ZFF) kushindwa
kukaa pamoja na vilabu na kushirikiana
katika masuala mbali mbali ya kuendeleza mchezo huo pamoja na utatuzi wa
changamoto ziliopo.
Aidha, walisema miongoni mwa matatizo makubwa yanayovikabili
vilabu kote nchini, hususan vile vilivyoko daraja la kwanza ni ukosefu wa viwanja
vya mazoezi.
“Vilabu vina matatizo mengi, pamoja na
Mlandege kuwa na historia nzuri ya kuchukua makombe, haina kiwanja chake”,
alisema mmoja wa wafanyabiashara hao.
Waliomba Serikali kuweka utaratibu
mzuri wa matumizi ya viwanja vyake, ili kila timu iweze kupata fursa ya
kuvitumia kwa mazoezi badala ya kuhodhiwa na timu maalum kama milki yake.
Aidha, walieleza haja ya ZFF kuangalia uwezekano wa kubadili mfumo wa
uendeshaji ligi kwa timu za Vikosi kwa kuwa na timu moja, hatua itakayoziinua
timu za kiraia ambazo ndio zenye mashabiki wengi.
Walisema ushiriki wa timu za kiraia,
kama ilivyo sasa katika michuano ya ‘ndondo na yamle yamle’ utaibua hamasa na
kuleta ushindani mkubwa kama ilivyokuwa miaka iliyopita.
Wafanyabiashara hao waliahidi
kuendelea kushirikiana na Serikali na vyama vya michezo ili kuendeleza michezo
mbali mbali nchini, wakibainisha hatua hiyo itawaweka vijana katika maadili
mema na kuondokana na vitendo viovu, ikiwemo utumiaji wa dawa za kulevya.
Walimuomba Waziri anaehusika na
michezo kuendelea kushirikiana nao na kubainisha utayari wao katika kusaidia
maendeleo ya michezo mbali mbali nchini.
Aidha, akitoa shukrani, Mkurugenzi wa
Klabu ya Mlandege Ali Khatibu Dai aliwashukuru wafanyabiashara hao kwa kujitolea kufanikisha safari ya Timu hiyo kuelekea
nchini Tunisia katika pambano la marudiano dhidi ya timu ya CS Sfaxien.
Alisema miongoni mwa athari kubwa
ambayo Klabu ya Mlandege ingekabiliana
nayo kwa kushindwa kushiriki katika
mchezo huo wa marudiano ni kufungiwa na CAF, na hivyo kuliletea aibu Taifa.
Jumla ya US Dola 34, 000 zimechangwa
na wafanyabaishara hao watano kutoka Zanzibar.
Abdi
Shamna, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422
Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822
E-mail:
abdya062@gmail.com
No comments:
Post a Comment