Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais akutana na Uongozi wa Chama cha Wasanii wa Kizazi Kipya {ZFU}

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla Akizungumza na Uongozi wa Chama cha Wasanii wa Kizazi Kipya {ZFU} waliofika Afisini kwake Vuga kujitambulisha.
Mwenyekiti wa Bodi ya Chama cha Wasanii wa Kizazi Kipya Zanzibar Makame Mshimba Mbarouk akielezea malengo la Chama chao katika kushirikiana na Taifa kwenye masuala mbali mbali yanayopangwa kufikishwa Ujumbe kwa Wananchi kupitia Sanaa.
Rais wa Chama cha Wasanii wa Kizazi Kipya Mohamed Abdulla Laki akiipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa uamuzi wake  maalum wa kuwashirikisha Wasanii na Wanamichezo kwenye Sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar za Mwaka huu zilizofikia Kilele chake katika Uwanja wa Mnazi Mmoja.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla akiwahakikishia Wasanii dhamira ya Serikali katika kuimarisha Sanaa kwa lengo la kudumisha Utamaduni wake.

Picha na – OMPR – ZNZ.


Na Othman Khamis, OMPR


Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inalazimika kuendelea kuwaheshimu Wasanii Nchini kutokana na mchango wao mkubwa wanaoendelea kuutoa kwa Jamii na Taifa kwa jumla katika suala zima la kufikisha Ujumbe, Elimu  sambamba na burdani.

Akizungumza na Uongozi wa Chama cha Wasanii wa Kizazi Kipya {ZFU} waliofika Afisini kwake Vuga kujitambulisha, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla alisema Zanzibar kipindi hichi inapaswa kurejea katika hadhi yake ya kuibua Wasanii waliobobea katika anga za Kimataifa.

Alisema wapo Wasanii na hata Wawakilishi wa Taasisi za Sanaa katika baadhi ya Mataifa Duniani yaliyotumia umahiri wa Sanaa ya Zanzibar ulioenea Dunia katika Miaka ya nyumna na hatimae kushawishika kuja kujifunza Sanaa hiyo iliyoshiba Utamaduni wa kuwapenda wageni.

Mheshimiwa Hemed Suleiman alisema Serikali imedhamiria kuimarisha Sanaa kwa lengo la kudumisha Utamaduni wake ili ufikie wakati Taifa na hata Jamii husika iridhike na vipaji walivyobarikiwa kuwa navyo Wasanii wa Zanzibar ambavyo vinastahiki kulelewa.

Kwa mnasaba huo Mheshimiwa Hemed alitanabahisha wazi kuwa Serikali kupitia Wizara ya Habari, Vijana na Utamaduni itabeba jukumu la kuwaendeleza Wasanii wake kwa kuwapatia fursa za Kielimu na  mafunzo mengine muhimu yatakayowajengea uwezo mkubwa utakaowasaidia kufikia kiwango cha Kitaifa na Kimataifa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kupitia Uongozi huo wa Chama cha Wasanii wa Kizazi Kipya amewatoa hofu Wasanii Nchini kwamba wajiandae kushirikishwa katika shughuli zozote za Kitaifa wakati zinapofanyika iwe Mjini au Vijijini na wakat mwengine hata Tanzania Bara jambo ambalo huwa likifanyika.

Mheshimiwa Hemed amemuagiza Waziri anayesimamia Wizara inayohusika na masuala ya Wasanii katika Mikutano na vikao vyake atenge muda wa Kukutana na Wasanii kupitia Uongozi wake ili kujadili masuala yanayoleta changamoto katika shughuli zao za kila siku.

Alishukuru na kuwapongeza Wasanii wote Nchini kwa ushiriki wao mkubwa wakati Taifa likiwa katika Kampeni za Uchaguzi Mkuu ambapo Wasanii walitumia vipaji vyao katika kutoa Burdani zilizotuliza nyoyo za Kundi kubwa la Vijana na kuepuka kujiingiza katika Vitendo viovu na hatimae kuisaidia Nchi kuendelea kubakia katika hali ya  Amani na Utulivu.

Mapema Mwenyekiti wa Bodi ya Chama cha Wasanii wa Kizazi Kipya anzibar Makame Mshimba Mbarouk alisema Wasanii wachanga Nchini wameomba kupewa fursa ya kuvitumia vipaji vyao katika kufikisha Ujumbe na kutoa Burdani kwa Jamii mahala popote watakapopangiwa.

Mwenyekiti Makame Mshimba alisema Wasanii kupitia Chama chao wamekuwa na Programu nzuri zinazotekelezeka lakini kinachowakwaza kwao ni ukosefu ya ufadhili hasa pale wanapopata fursa za kuzitumia Nyanja za Kimataifa.

Naye kwa upande wake Rais wa Chama cha Wasanii wa Kizazi Kipya Mohamed Abdulla Laki ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa uamuzi wake  maalum wa kuwashirikisha Wasanii na Wanamichezo kwenye Sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar za Mwaka huu zilizofikia Kilele chake katika Uwanja wa Mnazi Mmoja.

Laki alisema wakati umefika kwa Serikali kuwatumia Zaidi Wasanii hao katika masuala mbali mbali kwa vile wako tayari wameshajikubalisha kufanyakazi za Kitaifa kwa kufikisha Ujumbe kupitia Sanaa zao.

Alisema wakati umefika kwa Wizara ya Habari, Vijana na Utamaduni kuanzisha Mfuko Maalum wa Utamaduni utakaosaidia Wasanii kutatua baadhi ya changamoto zinazowakabili katika harakati zao za Kazi za kila mara.

 

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.