Habari za Punde

Wateja wa Tigo Zanzibar kulipa bili za maji kwa Tigo Pesa


 Waziri wa maji nishati na madini Zanzibar Suleiman Makame, katikati akifafanua jambo ambapo wameingia makubaliano na Tigo Pesa kwamba wateja wa maji wa ZAWA wataanza kulipia bili zao kupitia Tigo Pesa kushoto ni Mkurugenzi Mkuu-ZAWA- Mussa Ramadhan Haji na kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Fedha Tigo pesa Angelica Pesha

Na Mwandishi wetu


MAMLAKA ya Maji Visiwani Zanzibar (ZAWA), kwa kushirikiana na Kampuni ya Simu za Mkononi, wameingia makubaliano ambapo wateja wataanza kulipa bili za maji kwa kupitia Tigo Pesa.

Akizungumza Visiwani hapa, Kaimu Afisa Mkuu wa Kitengo cha Tigo Pesa, Angelica Pesha, alisema kuwa lengo la kampuni hiyo ni kuhakikisha watu wanabadilisisha maisha na kuishi kidijitali kwa kutumia Tigo Pesa kupata huduma mbalimbali ikiwemo kulipa bili kirahisi.

“Tumejikita katika kuhakikisha wateja wanaishi maisha ya kidijitali kupitia Tigo Pesa katika kupata huduma za mahitaji ya kila siku. Kwa kuingia makubaliano haya na ZAWA, ni hatua nyingine itakayowasaidia wateja wetu kulipa bili zao kirahisi,” alisema Angelica.

Aliongeza: "Hapo awali wateja walikuwa wakilazimika kufika katika ofisi za ZAWA na wale waliochelewa kulipa bili walikuwa wakikatiwa huduma, kwa sasa kupitia simu yako ya mkononi una uhakika wa kulipa bili za maji kwa kutumia Tigo Pesa.”

Mkurugenzi wa ZAWA, Mussa Ramadhan, ameishukuru Tigo kwa kuchukua hatua hiyo Visiwani Zanzibar ambapo wateja wataanza kuliba bili zao kirahisi na kuendele kupata huduma ya maji.

“Mikakati yetu ni kuendeleza na kurahisisha huduma ya maji kwa wateja wetu, hivyo Tigo Pesa itarahisisha ukusanyanyaji wa bili kwa haraka kupitia simu za mkononi," alisema.

Alisema kuwa suluhisho hilo linatarajiwa kuharakisha ufanisi katika ukusanyaji wa mapato kwa mamlaka na hivyo kuongeza uwezo wake kwenye utoaji wa huduma ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya maji na kupanua wigo wake ndani ya Visiwa hivyo.

Alisema maji ni moja ya rasilimali muhimu katika kuendesha shughuli za nyumbani na za kiuchumi.

 Mamlaka ya Maji ya Zanzibar ina jukumu kubwa la kusimamia huduma za usambazaji maji kwa zaidi ya walengwa 1,161,915 katika Visiwa hivyo.

Kulipa bili mteja atatakiwa kupiga *150*01# alafu anachagua namba 4 Kulipa Bili, atabonyeza namba 3 na kuingiza namba za biashara (123569), kisha zitafuatiwa na namba za akaunti ya ZAHA baadaye namba ya siri ya Tigo Pesa kwa uthibitisho na moja kwa moja atapokea ujumbe mfupi wa maneno.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.