Habari za Punde

Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi ajumuika na waislamu katika sala ya Ijumaa Masjid Rahma Nungwi

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi akiwasalimia na kuzungumza na Wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja baada ya kumaliza kwa Sala ya Ijumaa iliofanyika katika Masjid Rahma Nungwi.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi akiitikia dua baada ya kumaliza kuzungumza na kuwasalimia Wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja wakati wa kumaliza kwa Sala ya Ijumaa iliofanyika leo katika Masjid Rahma Nungwi, ikisomwa na Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh, Saleh Omar Kabi (kulia kwa Rais) na (kushoto kwa Rais) Katibu wa Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khalid Ali Mfaume na Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mhe. Ayoub Mohammed Mahmoud.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi , akisalimiana na kuagana na Wananchi baada ya kumalizika kwa Sala ya Ijumaa iliofanyika katika Masjid Rahma Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja leo.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la MapinduziAlhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi ameendelea kuwasisitiza viongozi aliowateua kwenda kuwasikiliza wananchi changamoto walizonazo.

Alhaj Dk. Hussein Mwinyi ameyasema hayo leo wakati akitoa salamu zake kwa wananchi wa kijiji cha Nungwi mara baada ya kuungana nao katika sala ya Ijumaa huko katika Masjid Rahman iliyopo Nungwi, Wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Katika salamu zake hizo, Alhaj Dk. Mwinyi alisema kuwa kuna kila sababu kwa viongozi wake wakiwemo Wakuu wa Wilaya na Mikoa kwenda kuwasikiliza wananchi changamoto zao ili ziweze kupatiwa ufumbuzi.

Alisema kuwa amegombea nafasi ya Urais kwa ajili ya kuwatumikia wananchi kwa kuwasikiliza matatizo yao, kero zao zikiwemo huduma za jamii kama vile afya, elimu, maji na nyenginezo ambapo hivi sasa amekuwa akifanya mikutano kadhaa na wadau wa sekta hizo kwa azma ya kutatua changamoto zilizopo.

Alisema kuwa changamoto hizo zinashughulikiwa na kusisitiza kwamba tayari alishawaambia wateule wake  wakati akiwaapisha kwamba washuke chini wakawashughulikie wananchi changamoto zao za ardhi, kuondoa dhulma na changamoto nyenginezo.

Aliwapa maagizo Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja na Mkuu wa Wilaya Kaskazini A, wakutane na uongozi kwa ajili ya kusikiliza changamoto za wananchi wa kijiji cha Nungwi na kuwataka wakatatue na yale yaliyo chini ya uwezo wao wamjuulishe ili ayafanyie utatuzi.

Alisema kuwa anadhima ya kuhakikisha anatenda haki kwa wananchi wote bila ya kujali uwezo wao kifedha, itikadi zao za kisiasa kwani yeye ni Rais wa Zanzibar na ana wajibu wa kuwatumikia wananchi wote bila ya kujali matabaka, rangi, dini wala kabila.

“Nnaomba muendelee kuniombea dua ili Mwenyezi Mungu aniwezeshe kwa dhamira yangu njema niweze kutekeleza yale ninayokusudia katika kuwaletea wananchi maendeleo, niweze kuondoa dhulma na kuweza kuwatendea haki wananchi wote wa Zanzibar”,alisema Dk. Mwinyi. 

Aliwaomba wananchi wote wa Zanzibar kuendeleza amani iliyopo kwani hakuwezi kupatikana maendeleo iwapo amani itatoweka kwanii mekuwa ni utamaduni kwamba kila ikikaribia uchaguzi amani hutetereka.

Alisema kuwa jambo hilo linaathirisana kidugu, kidini na kimaendeleo na kusema kwamba wananchi na viongozi wa dini waliombwa kuiombea nchi amani.

Alisema kuwa kwa kiwango kikubwa hivi sasa nchi ina amani, hivyo ni wajibu wa wananchi wote kuiendeleza Amani iliyopo.

Kwa upande wa umoja, Alhaj Dk. Mwinyi alisema kuwa ni kawaida kwamba umoja hutetereka kutokana na kutokuwepo kwake kutokana na itikadi za kisiasa.

Aliongeza kwamba baada ya uchaguzi viongozi waliamua kukaa pamoja na kuridhiana na kuwaunganisha Wazanzibari ili kuondokana na mitafaruku iliyokuwepo kwani dini inataka watu waishi pamoja na inatakataa mifarakano.

Alisema kuwa ilifikia wakati watu walikuwa hawazikani, walipeana talaka kwenye ndoa kwa sababu ya kisiasa, hivyo ikaonekana hayo hayapaswi kuendelezwa.

Kutokana na hali hiyo, ikaonekana hilo haliwezekani na ndipo viongozi walikaa na kuzungumza juu ya suala hilo ambapo safari hii hakukuwa na mtu kutoka nje kwa ajili ya kuwaunganisha wala kukaa Kamati kubwa kubwa za chama ama serikali bali walikaa viongozi wenyewe wa vyama vyao wakajadiliana pamoja.

Alisema kuwa kwa makusudi walikubaliana kuwaunganisha wananchi kwa kuanzia kwenye vyama vyao, kuunda serikali ya umoja wa kitaifa, na tayari imeshaundwa na mategemeo yake kwamba wananchi nao wataungana katika kuunga mkono juhudi hizo.

Alisisitiza kurudi katika umoja, mafundisho ya dini ya Kiislamu yanayosisitiza umoja na amani licha ya kuwepo wachache waliokuwa hawajakubaliana na hali hiyo.

Alisisitiza haja ya kuendelea kuelemishana kwamba umoja una umuhimu mkubwa katika Taifa lolote duniani.

Alisema kuwa baada ya kuwa na amani na umoja kinachofuata ni kuwaletea wananchi maendeleo wanayoyataka.

Alhaj Dk. Mwinyi alisema kuwa matarajio ya wananchi ni makubwa sana katika kuwaletea maendeleo na kuondosha dhulma na kufanikisha mambo wanayoyahitaji.

Mapema Sheikh Hassan Jani Masoud akisoma khutba ya sala ya Ijumaa alisema kuwa wananchi wa Nungwi wataendelea kumuombea dua Rais Dk. Mwinyi usiku na mchana ili Mwenyezi Munguc amlinde hasa kutokana na kazi kubwa anazozifanya za kuwapigania wanyonge.

Sheikh Hassan alisema kuwa wananchi wana matumaini makubwa ya kiongozi wao huyo katika kupigania haki na wanampongeza kwa jitihada zake hizo.

Sambamba na hayo, kwa niaba ya wananchi wa Nungwi Sheikh Hassan aliomba uongozi wa serikali kukutana na viongozi wa kijiji chao kwa lengo la kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazowakabili.

Sheikh Hassan alisisitiza haja ya kuendeleza maadili ya Kiislamu, kulinda amani pamoja na kusimamia haki za wanyonge.

Wakati huohuo,Rais Dk. Mwinyi alimtembelea Rais Mstaafu wa Awamu ya Sita Alhaj Dk. Aman Abeid Karume huko nyumbani kwake Mbweni nje kidogo ya Jiji la Zanzibar.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.