Habari za Punde

Jamii yaaswa kujenga tabia ya kupima afya mara kwa mara

Baadhi ya Waandishi wa Habari wakimsikiliza Meneja wa Kitengo cha Maradhi yasioambukiza cha Wizara ya Afya Omar Abdulla Ali (hayupo pichani) akieleza ongezeko la Maradhi yasiyoambukiza yanavyoiathiri jamii huko katika Ukumbi wa Jumuiya ya Watu Wanaoishi na Maradhi yasiyoambukiza, Mpendae Zanzibar .

 Meneja wa Kitengo cha Maradhi yasioambukiza cha Wizara ya Afya Omar Abdulla Ali  akitoa mada ya Maradhi ya Saratani kwa waandishi wa habari katika Ukumbi wa Jumuiya ya Watu Wanaoishi na Maradhi yasiyoambukiza, Mpendae Zanzibar.

Na Khadija khamis –Maelezo Zanzibar  

 Jamii inapaswa kujenga tabia ya kupima afya mara kwa mara ili kugundua hatua za awali za maradhi mbali mbali hasa maradhi yasiyoambukiza.

 

Akizungumza na Waandishi wa Habari Meneja wa Kitengo cha Maradhi yasioambukiza cha Wizara ya Afya Omar Abdullah Ali amesema kwa vile dalili za maradhi ya yasiyoambukiza haziko wazi ni vyema wananchi kuangalia afya zao ili kupatiwa tiba mapema.

 

Alisema hivi sasa Zanzibar maradhi yasiyoambukiza hasa Saratani ya shingo ya kizazi, saratani ya matiti kwa wanawake na tenzi dume inayowapata wanaume ndizo zinazoongoza kuathiri wananchi wengi.

 

Aliwaeleza waandishi wa habari katika Ofisi za Jumuiya ya Maradhi yasioambukiza Mpendae kuwa katika uchunguzi uliofanyika Novemba mwaka jana umeonyesha jumla ya wanawake 112 wanaviashiria vya saratani kati yao 45 wamegundulika kuwa na saratani ya matiti na kupatiwa matibabu.

 

Alifahamisha kuwa saratani ni chembe chembe asi za kwenye mwili zinazoua chembe hai na hatimae kusababisha uvimbe ndani ya mwili wa binaadamu

 

Chanzo cha maradhi ya Saratani hakiko wazi lakini inaweza kumpata binadamu kwa njia ya urithi, matumizi ya dawa kwa muda mrefu bila mpango, umri mkubwa pamoja na mionzi.

 

Aidha aliwataka akinamama kujifanyia uchunguzi kwenye matiti baada ya kumaliza hedhi zao na wakibaini uvimbe wakimbilie vituo vya afya

 

Aliwashauri akinamama wenye umri kuanzia miaka 20 hadi 39 kuhudhuria katika vituo vya afya kufanyiwa uchunguzi wa matiti kila baada ya miezi mitatu

 

Meneja wa Jumuiya ya watu wanaoishi na maradhi yasioambukiza Zanzibar Haji Khamis Fundi amesema  kutokana na ongezeko la maradhi yasiyoambukiza, juhudi zaidi inapaswa kuchukuliwa kupambana nayo.

 

Serikali na Jumuiya zisizo za serikali wanatarajia kufanya uchunguzi wa saratani ya matiti katika hospitali ya Wete Pemba na watakaogundulika watapatiwa tiba ikiwa ni wiki ya maadhimisho ya siku ya saratani duniani kila ifikapo Febuari 4 ya kila mwaka  . 


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.