Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi Ameshiriki Matembezi ya Mazoezi ya Kitaifa ya Viungo Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akishiriki katika Tamasha la Matembezi ya Mazoezi ya Viungo lililofanyika Zanzibar Kitaifa leo 1-1-2021, hufanyika kila mwaka ifikapo Januari Mosi na (kulia kwake) Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe.Maalum Seif Sharif Hamad na Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe.Zuberi Ali Maulid na (kushoto kwake) Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla na Waziri wa Vijana Habari Utamatuni na Michezo Zanzibar Mhe. Tabia Maulid Mwita, wakimalizia matembezi hayo katika Uwanja wa Amaan Jijini Zanzibar kwa ajili ya mazoezi ya pamoja.  

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la MapinduziDk. Hussein Ali Mwinyi amewataka wananchi kufanya mazoezi kwa lengo la kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza.

Rais Dk. Hussein Mwinyi aliyasema hayo leo katika hotuba yake aliyoitoa huko uwanja wa Amaan Jijini Zanzibar ikiwa ni maadhimisho ya Siku ya Mazoezi ya Viungo Kitaifa yaliyoanzia kiwanja cha Mapinduzi Square Michenzani na kuishia Uwanja wa Amaan ambapo Rais Dk. Hussein Mwinyi alishiriki kikamilifu pamoja na viongozi wengine akiwemo Mkewe Mama Mariam Mwinyi.

Viongozi wengine walioshiriki ni Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, Makamo wa Pili wa Rais Hemed Suleiman Abdulla pamoja na Mkewe Mama Sharifa, Spika wa Baraza na Wawakilishi Zubeir Ali Maulid, Mkuu wa Mkoa Idrisa Mustafa Kitwana, Mawaziri, vikundi vya mazoezi pamoja na wananchi.

Alisema kuwa mazoezi ni jambo lolote linalohusisha misuli na kuongezeka kwa mapigo ya moyo na kasi ya kupumua kwani kiwango cha mazoezi kinacholeta faida ni mazoezi yasiyopungua dakika 30 kwa siku angau tatu kwa wiki na kumfanya mtu kutoka jasho.

Rais Dk. Mwinyi aliwataka wananchi hasa wale wanaofanya kazi maofisini kuongeza bidii ya kufanya mazoezi na wale wanaotumia magari wanapaswa kupanga shughuli ambazo zitawafanya kila siku watembee kwa miguu.

Kwa upande wa waajiri aliwashauri kuimarisha mazingira ya kazi kwa kuhakikisha watumishi wao wanashiriki katika michezo na kufanya mazoezi hata katika sehemu zao za kazi kwa kuanzisha timu za michezo pamoja na kutenga siku maalum katika mwezi kwa ajili ya mabonanza ya michezo.

Alisisitiza kuwa Mazingira rafiki ya kufanya mazoezi kazini ni kutenga  vyumba vya mazoezi na kununua vifaa vya michezo hatua ambayo itaimarisha afya ya watumishi na kupunguza kharama za matibabu katika taasisi husika.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa ili kufanya mazoezi kuwa endelevu Maofisa Michezo wa Mikoa na Wilaya wanawajibu wa kuongeza uhamasishaji na uundaji wa vikundi vya mazoezi vya pamoja katika maeneo yao.

Aliongeza kuwa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa pamoja na Wizara ya Ardhi na Makaazi zina mamlaka ya kusimamia na kuweka mazingira bora ya watu kufanya mazoezi kwa kuendelea kutenga viwanja vya michezo na kuzuia uuzaji wa maeneo ya wazi.

Dk. Mwinyi alisema kuwa Matamasha ya michezo na utamaduni yanatakiwa kuwa kichocheo cha kushirikisha vitu vingi ikiwemo michezo ya jadi na mashirndano ya basikeli katika maeneo mbali mbali ambayo yana mchango mkubwa katika  kutunza afya za washiriki wa michezo hiyo.

Alisema kuwa katika matamasha hayo ni vyema wananchi wakahamasishwa kupima afya zao ili kuongeza hamasa ya wananchi huku upimaji huo ni vyema ukawa bure.

Aidha, alisema kuwa bonanza hilo linapelekea watu kujuana na kubadilishana mawazo huku akieleza dhamira ya wazi ya Serikali ya Awamu ya Nane katika kuimaisha michezo ikiwemo Bonanza la Michezo na vikundi vya mazoezi linalofanywa kila tarehe mosi ya Januari ya kila mwaka.

Pia, alieleza azma ya Serikali ya kuhamaisha michezo ya asili ya Zanbzibar ikiwemo mashindano ya resi za ngalawa, bao, karata, mchezo wa ngombe na mengineyo ambapo pia, watu wenye ulemavu watahamasishwa na kupatiwa vifaa.

Alisema kuwa michezo ni nyenzo madhubuti katika kulinda avya za wanaadamu na kuwajengea uimara na ustahamilivu ambapo Sera ya michezo inatambua umuhimu wa michezo ikiwemo kuhamasisha uma wa Wazanzibari kushiriki katika michezo na mazoezi ya viungo.

Aliongeza kuwa Serikali itawezesha kupatikana viwanja na michezo na vifaa vya michezo vilivyobora na vya kutosha kwa ajili ya kuimarisha maendeleo ya mic hezo nchini.

Rais Dk. Mwinyi alitoa ushauri kwa wananchi katika maeneo yao nchini kushiriki kufanya mazoezi ambayo ni sehemu ya michezo.

Alieleza kuwa ili utaratibu wa kufanya mazoezi uwe endelevu  aliagiwaagiza Wakuu wa Mikoa kuwa na siku maalum ya mazoezi kwa afya za wananchi huku akiwaasa wananchi kufanya mazoezi na kuahidi kwamba serikali itaweka mazingira mazuri ya kufanya mazoezi.

Alisema kuwa moja wapo ya vitu vinavyoshirikisha watu wengi kujiunga na kufanya mazoezi ni kuwa na matamasha ya michezo ambayo yanalenga kuhamasisha wananchi kushiriki katika michezo ikiwa ni pamoja na kufanya mazoezi ya viungo ili kuepuka magonjwa  yasiyoambukiza ambayo yanaongezeka kwa kasi nchini.

Alisema kuwa magonjwa hayo yanatokana na mitindo isiyofaa ya maisha  kama matumizi ya tumbaku, lishe duni, matumizi ya pombe kupita kiasi pamoja na kutofanya mazoezi ya viungo mara kwa mara ambapo magonjwa kama kisukari, shinikizo la damu, magonjwa ya moyo na mishipa ni miongoni ya magonjwa hayo ambayo yasipodhibitiwa huwa sugu na yanagharama katika kuyatibu.

Alitoa pongeza kwa Chama cha (ZABESA) pamoja na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo pamoja na kwa jitihada zao katika kuwaunganisha na kuwaweka pamoja wanavikundi pamoja na kuandaa bonanza hilo huku akiwapongeza Benki ya NMB na Mamlaka ya bandari ambao wamefanikisha kwa kutoa michango yao.

Nae Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Tabia Mwita Maulid alitoa shukurani na pongezi kwa Rais Dk. Mwinyi kwa kushiriki kikamilifu katika mazoezi hayo ambapo wananchi waliowengi wamemuunga mkono.

Alieleza kuwa Wizara anayoiongoza itaendelea kutekeleza Sera ya Michezo ambayo imekuwa inahamasisha ufanyaji wa mazoezi kutokana na umuhimu wake mkubwa katika afya ya mwanaadamu.

Mapema  Mwenyekiti wa Chama cha Mazoezi ya Viungo Zanzibar (ZABESA) Said Suleiman kwa niaba ya chama hicho alimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mweyekiti wa Baraza la Mapinduzi na kuahidi kuendelea kushirikiana nae.

Walieleza matumaini yao kwa Rais Dk. Mwinyi kutokana na kasi aliyonayo ya kutaka kuwatumikia wananchi na kuahidi kumuunga mkono katika kujenga nchi yao.

Pia, Mwenyekiti huyo wa (ZABESA) alitumia fursa hiyo kumpongeza Maalim Seif Sharif Hamad kwa kuteuliwa kuwa Makamo wa Kwanza wa Rais Zanzibar na kueleza jinsi hapo siku za nyuma alivyoweza kuunga mkono mazoezi hayo huku akipomgeza Hemed Suleiman Abdulla kwa kuteuliwa kuwa Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Mwenyekiti huyo alieleza mafanikio ya Chama hicho yaliyopatikana ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa vikundi kutoka 17 walivgyoanza navyo na kufikia 80 hivi sasa sambamba na ushiriki wa vikundi kutoka Pemba na Tanzania Bara ambapo pia alitumia fursa hiyo kueleza baadhi ya changamoto walizonazo.  

Katika hotuba yake alieleza matumaini ya chama hicho kwamba Rais Dk. Mwinyi ataendelea kushirikiana nao katika miaka mingine ijayo kwenye tukio kama hilo huku akieleza kauli mbiu ya mwaka huu kuwa “Kuimarisha Uchumi wa Buluu, afya bora kwanza”.

Katika Tamasha hilo, Rais Dk. Mwinyi alitoa vyeti maalum kwa washiriki wa Tamasha hilo kutoka Unguja, Pemba na Tanzania Bara ambapo mapema wanamazoezi hao walipita mbele ya jukwa kuu alilokaa Rais huku wakionesha umahiri wao wa mazoezi.

Sambamba na hayo Wanamazoezi hao walionesha namna ya ufanyaji wa mazoezi wakiongozwa na walimu wao mahiri wa mazoezi ambapo walionesha ufundi na hamasa kubwa ya ufanyaji wa mazoezi.

KwamujibuwaKatibuMkuuWizarayaHabari, Vijana, UtamaduninaMichezo Omar Hassan King jumlayavikundi 97  vimeshirikikatika Bonanza hilovikiwemo 60 kutokaUnguja, 20 kutoka Pemba na 17 kutoka Tanzania Bara.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.