Habari za Punde

ZSSF Kuhakikisha Amana Zote za Wanachama Zinasimamiwa Ipasavyo.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akiwahutubia Wananchi wa Pemba katika viwanja vya Tibirinzi Chakechake Pemba wakati wa hafla ya Ufunguzi wa Jengo la Ofisi ya ZSSF la Hifadhi Building Tibirinzi Pemba, ikiwa ni shamrashamra za  kusherehekea Miaka 57 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyiamesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane itaendelea kufanya kazi kwa karibu na uongozi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) katika kuhakikisha amana zote za wananchama zinasimamiwa ipasavyo.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo katika hotuba yake ya ufunguzi wa jengo jipya la “Hifadhi Building” la (ZSSF)lililoko Tibirinzi, Wilaya ya Chake Chake , Mkoa wa Kusini Pemba, ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra za sherehe za miaka 57 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964 ambapo pia, Makamo wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad  alihudhuria.

Katika hotuba hiyo Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa ni jukumu la Serikali kuhakikisha inachukua hatua zionazofaa na kwa wakati katika kuhakikisha Mfuko huo unaendelea kuimarika, unaongozwa na kusimamiwa na viongozi walio makini na wanaojiepusha na vitendo vya ubadhirifu, rushwa na wizi.

Alisisitiza kwamba Serikali itahakikisha wanachama wa Mfuko huo wanaishi bila ya kuwa na wasiwasi wa hatma ya amana wanayowekeza ambayo mara nyingi huwa nitegemeo kubwa katika maisha ya wafanyakazi baada ya kustaafu.

Alisema kuwa ni lazima viongozi wa (ZSSF) wahakikishe kwamba utekelezaji wa dhamira njema ya kutumia amana ya wanachama wa Mfuko wanayokusanya iambatane na mipango imara ya kusimamia uwekezaji huo.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi aliwataka viongozi kuhakikisha kwamba fedha inayowekezwa inazalisha na shughuli zote za uendeshaji wa taasisi hiyo zinafanywa kwa weledi, umahiri na umakini mkubwa.

Rais Dk. Mwinyi alisisitiza kwamba uongozi nilazima kila wakati uhakikishe kwamba idadi ya fedha zinazohitajika kulipa stahiki za wananchama wanaostaafu na mafao mbali mbali zinakuwepo kila wakati bila ya nendda rudi na usambufu wa aina yoyote ile.

Alisema kuwa kuwepo kwa majengo ya ofisi za kisasa ni hatua muhimu katika juhudi hizo za kuvutia wawekezaji kisiwani Pemba.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa kazi kubwa imefanywa na Serikali ya Awamu ya Saba ya kuimarisha mazingira ya kufanya kazi kisiwani Pemba  ambapo majengo mengi ya serikali yamejengwa na mengine yamefanyiwa matengenezo makubwa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.

Katika hotuba yake hiyo, Rais Dk. Mwinyi aliwahimiza viongozi wa (ZSSF)kuhakikisha taratibu za ukodishaji wa maduka yaliyomo katika maduka mapya ya Michenzani Mall na jengo la Thabit Kombo kwani ni kipindi kirefu tangu majengo hayo yalipozinduliwa rasmin.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alitoa pongezi kwa wakandarasi wa ujenzi wa jengo hilo Kampuni ya kizalendo ya Quality Building Contractor pamoja na kampuni ya Arqes Africa kwa kazi kubwa waliyoifanya.

Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kutoa pongezi za dhati kwa uongozi wa Wizara ya Fedha, uongozi wa ZSSF pamoja na Kamati ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa kwa maandalizi mazuri ya shughuli hiyo na kwa kumualikakuwa mgeni rasmi.

Alisisitiza kwamba ni jukumu la kila mwananchi wa Zanzibar kuendelea na kudumisha fikra njema za waasisi wa nchi wakiongozwa na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais  Fedha na Mipango Jamal Kassim Ali alisema kuwa kukamilikakwa ujenzi huoni mafanikio makubwa kwani itaongeza ufanisi na mapato.

Alisema kuwa kukamilikakwa jeno hilo kunatokana na mashirikiano ya Mfuko wa ZSSF, Wizara na Bodi ya Mfuko huo sambamba na ushauri mkubwa uliokuwa ukitolewa na Rais juu ya Mfuko huo huku akieleza haja kwa taasisi za Serikali kuwa makinikatika kutekeleza miradi kama hiyo ikiwa ni pamoja na kufanya tathmini ya miradi kabla ya ujenzi wake.

Alieleza kwamba fedha zliozotumika ni michago ya wanachama wa ZSSF hivyo, ni vyema zikarudi na kupata tija kwa wanachama wa Mfuko huo huku akiwataka wale wote watakaokodi jengo hilo wanapaswa kulipa fedha zinazotakiwa.

Nae Katibu Mkuu Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Khamis Mussa Omar alisema kuwa  kwa bahati mbaya ZSSF Tawi la Pemba awali ilikuwa ikitoa huduma zake katika maeneo ya kukodi katika majengo ya watu binafsi, Ofisi za kudumu zilianzishwa mwaka 2004 katika jengo lake la Kituo cha Mikutano (Pemba Conference Centre) ambalo pia, linatoa huduma za malazi afisi ambayoilikuwa ndogo sana.

Hivyo, ZSSF iliamua kujenga jengo hilo jipya la kisasa linaloendana na mahitaji ya sasa na hapo baadae  ambapo mkataba wa ujenzi ulitiwa saini tarehe 4 Julai 2009 baina ya ZSSF na Kampuni ya Kizalendo ya Quality Building Contractors baada ya Kampuni hiyo kuwa mshindi wa zabuni.

Kufuatia kusainiwa kwa mkataba huo, ujenzi ulianza rasmi tarehe 1 Agosti 2019 ambao ni mradi uliokuwawa miezi 12 na ulitarajiwa kukamilika tarehe 31 Julai,2020 lakini kutokana na changamoto zilizobainika wakati wa ujenzi na athari ya maradhi ya COVID 19 lakini hata hivyo,ujenzi ulikamilika rasmi Oktoba 2020.

Mapema Rais Dk. Mwinyi mara baada ya kulifungua jengo hilo alipata fursa ya kulitembelea na kupata maelezo kutoka kwa uongozi wa ZSSF pamoja na maelezo kutoka kwa Mkandarasi wa jengo hilo Khamis Ali kutoka Kampuni ya Quality Building Contractor Limited.

Kwa maelezo ya uongozi wa ZSSF Jengo hilo la ghorofa tatu limegharimu jumla ya TZS Bilioni 7.9 zimetarajiwa kutumika katika ujenzi wa jengo hilo ambapo hadi hivi sasa jumla ya TZS Bilioni 5.3 ameshalipwa mjenzi huku mjenzi huyo mzalendo akitoa shukurani kwa Rais kwa Dk. Mwinyi kuwapa kipaumbele wajenzi wazalendo.

 

Wakati huo huo, Rais Dk. Mwinyi aliitembelea ujenzi wa barabara unaoelekea katika maeneo huru ya vitegauchumi Micheweni na kufika eneo la Maziwangombe na kuwaeleza wananchi wa Micheweni kwamba fursa za ajira zitakapoanza wao watapewa kipambele.

 

Aliwataka wakuuwa Mikoa na Wilaya kwa kila Wilaya kutafuta maeneo ya uwekezaji huku akisisitiza kwamba kuna haja ya eneo hilola Micheweni kuweka viwanda vinavyohusiana na uchumi wa buluu zaidi kutokana na mazingira yake.

 

Rais Dk. Mwinyi alieleza haja ya kusogezwa wka huduma nyengine muhimu zikiwemo maji na umeme ili kufikia malengo yaliyokusudiwa ya kurahisisha uwekezaji katika eneo hilo na kuwataka Wizara husika kupanga na kuweka fedha kwa ajili ya mchakato huo.

 

Alisema miezi minane kwa barabara ya kilomita 2.8 iliyoelezwa na wajenzi wa barabara hiyo kutoka uongozi wa Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi ni mingi sana na kuutaka wapunguze ili shughuli ziweze kuendelea

 

Alisisitiza kwamba ahadi zote zilizotolewa wakati wa Kampeni zitafanyiwa kazi huku akieleza haja ya kujengwa barabara yote badala ya kujengwa eneo hiyo ya ambayo ujenzi wake unaendelea hivi sasa.

 

Alieleza azma ya Serikali ya kuweka viwanda katika eneo hilo kwa ajili ya kupata ajira zikiwemo zile ajira 300,000 zilizoelezwa katika Ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2020-2025 ili nyengine zitoke katika eneo hilo huku akiwapongeza wananchi wa Micheweni kwa kuupokea mradi huo.

 

Mapema Mkurugenzi waUwezeshaji na Maendeleo ya Uwekezaji ZIPA, Shariff Ali Shariff alimueleza Rais Dk. Mwinyi mipango na mikakati iliyowekwa  na ZIPA juu ya eneo hilo la uwekezaji.

 

Nae Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Salama  Mbarouk Khatib kwa niaba ya wananchi wa Micheweni alitoa shukurani kwa Rais Dk. Mwinyi kwa uwamuzi wake wa kuijenga barabara hiyo na kusema kwamba wananchi wamefarajika

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.