NA BAHATI HABIBU / MAELEZO 10/02/2021
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo amewataka wafanyakazi wa sekta ya habari kufanya kazi kwa ufanisi na mashirikiano ili kufikia malengo yaliyokusudiwa na Serikali ya kuwaletea maendeleo wananchi.
Ameyasema hayo alipofanya ziara ya kujitambulisha na kuzungumza na wafanyakazi wa sekta ya hiyo huko ukumbi wa Sanaa uliopo Rahaleo mjini Zanzibar.
Amesema ili sekta hiyo ifanye kazi kwa ufanisi kila mfanyakazi atekeleze vyema majukumu yake kutokana na nafasi yake aliyopangiwa bila ya kujali changamoto zitakazojitokeza katika utendaji wa kazi zao.
Katibu huyo amewataka viongozi wa taasisi hizo kufanya usawa kwa wafanyakazi na kuacha tabia ya ubaguzi ili kuepuka mizozo na migogoro kwa kuwapatia stahiki zao bila ya upendeleo.
Aidha amewasisitiza wafanyakazi kuwa na ushirikiano katika utendaji wa kazi zao na kuondoa makundi, ubaguzi na majungu ili kuweza kufanya kazi kwa kuleta maendeleo katika sekta hiyo.
“Ubaguzi, majungu na makundi katika utendaji wa kazi hurudisha nyuma utendaji wa kazi na kurudisha nyuma maendeleo ya nchi ni vizuri kushirikiana na kupendana ili kuleta maendeleo ya nchi” alisema Katibu Mkuu.
Nae Naibu Katibu Mkuu Khamis Abdalla Said amesema atahakikisha kwamba anazitafutia ufumbuzi changamoto zote zinazowakabili wafanyakazi wa sekta ya habari ikiwa pamoja na kuboresha maslahi ya wafanyakazi.
Hata hivyo amekemea matumizi mabaya ya fedha za umma kwa baadhi ya watendeji kutumia kwa maslahi yao binafsi au kwa wachache jambo ambalo linarudisha nyuma maendeleo ya taifa.
“Hatutakubali kuona fedha zilizochumwa kwa jasho la wanyonge zinatumika kwa maslahi ya watu wachache tutahakikisha kila fedha inayoingia inatumika kwa malengo yaliyokusudiwa”, alisema Naibu Katibu.
Akitoa neno la shukrani Katibu Mtendaji wa Tume ya Utangazaji Omar Said ameiomba serikali kuboresha maslahi ya wafanyakazi wa sekta ya Habari kutokana na mazingira magumu wanayokabiliana nayo ili kuweza kutoa huduma nzuri kwa jamii.
No comments:
Post a Comment