Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais aakhirisha Mkutano wa pili wa BLW



Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akisoma hotuba yake wakati akiakhairisha Mkutano wa Pili wa baraza la kumi huku akisisitiza juu ya azma ya serikali ya awamu ya nane katika kutatua migogoro ya ardhi kwa kuwapatia haki wananchi wanyonge.
Wajumbe wa Baraza la wawakilishi wakifuatilia kwa karibu hotuba ya Makamu wa Pili wa Rais alioitoa wakati akiakhirisha Mkutano wa pili wa baraza la kumi la wawakilishi.  
Wajumbe wa Baraza la wawakilishi wakifuatilia kwa karibu hotuba ya Makamu wa Pili wa Rais alioitoa wakati akiakhirisha Mkutano wa pili wa baraza la kumi la wawakilishi.  
 

Na Kassim Abdi 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameuagiza uongozi wa Wizara ya ardhi na maendeleo ya makaazi kufuatilia na kuharakisha utatuzi wa kesi za migogoro ya ardhi sambamba na kuwachukulia hatua kali watendaji wote wanaohusika katika migogoro hiyo.

Mhe. Hemed alilieza hayo wakati akiakhirisha mkutano wa pili wa baraza la kumi (10) ulionza vikao vyake Februari 10, mwaka huu katika ukumbi wa baraza la wawakilishi chukwani nje kidogo ya jiji la Zanzibar.

Alieleza kuwa kuwepo kwa migogoro hiyo kunasababishwa na baadhi ya viogozi na watendaji wasiokuwa waaminifu kwa kutenda vitendo viovu, hivyo alitanabahisha kwa wasimamizi na viongozi hao kuacha mara moja tabia hiyo kwani serikali haitomvumilia mtendaji yoyote atakaejihusisha na vitendo hivyo.

Makamu wa Pili alifafanua kwamba mbali na kero ya uwepo wa migogoro ya ardhi lakini pia kumekuwepo na muendelezo wa vitendo viovu vya rushwa katika upatikanaji wa haki ndani ya taasisi na katika jamii kwa ujumla.

Alisema kutokana kukithiri kwa changamoto hizo serikali ya awamu ya nane imeamua kuimarisha utawala bora unaosiamamia sheria kwa kuhakikisha inazipatia ufumbuzi changamoto hizo kwa kuanzisha mahakama maalum kwa kesi zinazohusiana na rushwa pamoja na uhujumu wa uchumi wa nchi.

Akigusia tatizo la masuala ya udhalilishaji Mhe. Hemed alieleza bado jamii inaendelea kukumbwa na vitendo hivyo akitolea mfano kukithiri kwa matukio ya ubakaji wa wanawake na watoto, matukio ya kupigwa na kuumizwa kwa wanawake na watoto pamoja na ushirikishwaji wa watoto katika biashara haramu za madawa ya kulevya.

“inathikitisha na kufedhehesha kwa vitendo hivi kutendwa na watu wazima wanaonekana wastaarabu na wenye hekima” alieleza Makamu wa Pili.

Makamu huyo wa Pili wa Rais alisema katika kuipatia ufumbuzi changamoto hiyo serikali itaendendelea kusimamia utekelezaji wa sheria na kuzifanyia marekebisho huku akitumia fursa hiyo kumpongeza Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa baraza la mapinduzi kwa uwamuzi wake wa kuanzisha mahakama maalum ya kushughulikia kesi za masuala ya udhalilishaji.

Akigusia juu ya suala zima la uimarishaji wa uchumi wa nchi Mhe. Hemed alisema serikali imedhamiria kuongeza uwezo wa ukusanyaji wa mapato kwa kuchukua hatua madhubuti za kupanua wigo kwa kuanzisha mifumo ya kieletroniki ya ukusanyaji mapato ya serikali, kudhibiti mianya ya uvujaji wa mapato pamoja na kuwasisitiza wananchi kutoa au kudai risiti kila wanapouza au wanaponunua bidhaa au kupatiwa huduma.

“Katika kuimarisha mifumo hiyo pia serikali itahakikisha kwamba inasimamia vyema matumizi ya fedha za umma, kufuata taratibu na sheria zilizowekwa” Alifafanua Mhe. Hemed

Alieleza kuwa, kwa vile Zanzibar pato lake linategemea sekta utalii, wizara ya utalii na mambo ya kale lazima isimamie kwa karibu uimarikaji wa makusanyo wa mapato yake.

Alisema kumekuwepo kwa baadhi ya wageni wanaofika nchini kukwepa sheria na taratibu za serikali kwa kuacha kufikia katika nyumba za kulala wageni na kuamua kulala katika maeneo yasiokuwa rasmi (Guest Bubu) hali inayosababisha serikali kukosa mapato.

Pia, Makamu wa Pili wa Rais aliiagiza wizra ya utalii na mambo ya kale, wamiliki wa mahoteli pamoja na watembezaji wageni kuchukua jitihada za makusudi kwa kuwaelimisha wageni wanaoingia nchini juu ya kuhifdhi mila na silka za kizanzibar kwa kuvaa mavazi yatayowasitiri badala ya hali ya ilivyo sasa kwa kuonekana kukiuka silka na desturi za nchi yetu.

Kwa upande wa kisiwa cha Pemba Mhe. Hemed alisema serikali inayoongozwa na Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi imedhamiria kueka kipaumbele maalum kwa uwekezaji ili kuleta uwiano katika visiwa viwili kwa kuifanya Pemba kuwa eneo la mkakati la uwekezaji lenye vivutio vitakavyowavutia na kuwashajihisha wawekezaji kujitokeza kwa wingi kwa kuanzisha na kuendesha miradi mikubwa ya kiuchumi kisiwani  humo.

“Niseme tu hali hii itasaidia sana kuinua na kuimarisha miundombinu ya kiuchumi pamoja na kunyanyua hali za maisha za wananchi kwa ujumla” Alifafanua Mhe. Hemed

Alieleza Serikali imeamua kupanua wigo kwa kutilia mkazo “Uchumi wa Buluu” ambao unahusisha sekta ya utalii, uvuvi, kilimo, mafuta na gesi, katika kutilia mkazo jambo hilo serikali imechukua hatua madhubuti kwa kuunda wizara maalum inayoshughulikia sekta hiyo.

Akitolea mfano kitendo cha serikali kutia saini hati ya maelewano (Memorundum of Understanding) kwa ujenzi wa bandari ya uvuvi na bandari ya mafuta na gesi ni mingoni mwa jitihada za  serikali inayongozwa na dk. Huseein Mwinyi katika kuimarisha uchumi wake.

Akilezea juu mapambano dhidi ya maradhi mbali mbali, Zanzibar ikiwa ni sehemu ya dunia aliwaomba waanchi kuendelea kushirikiana na watalamu wa Afya kwa kufuata maelekezo na miongozo katika kujikinga maradhi mbali mbali yanayoambukiza na yasioambukiza.

Mkutano wa Pili wa baraza la Kumi ulipokea, na kujadili miswada mbali mbali ikiwemo ripoti ya utekelezaji wa kazi za tume ya maadili ya viongozi wa umma, Ripoti ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa serikali kwa wizara na mashirika, Ripoti ya jitihada za kuzuwia rushwa na uhujumu uchumi Zanzibar pamoja na miswa mengine mbali mbali.

Baraza la wawakilishi limeakhirishwa hadi Jumatano ya tarehe 05 Mei 2021 Majira ya saa Tatu kamili za Asubuhi (3:00).

 

……………………………

Kassim Abdi

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

25/02/2021.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.