Habari za Punde

Serikali yatoa Tahadhari juu ya Virusi vya Corona na Maradhi ya Homa ya Mapafu

 SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR

AFISI YA MAKAMU WA PILI WA RAIS SERA,              URATIBU NA BARAZA LA WAWAKILISHI


TAARIFA KWA UMMA KUHUSIANA NA TAHADHARI JUU YA KINGA YA UGONJWA WA SHIDA YA KUPUMUA NA MARADHI                 MENGINE YA KUAMBUKIZA 


Ndugu Wananchi;

Kama tunavyofahamu kuwa dunia imeendelea kuathiriwa na miripuko mbalimbali ya maradhi yakiwemo maradhi ya homa ya mapafu, homa kali, shida ya kupumua na maradhi yanayosabishwa na virusi vya Corona (Covid – 19); hali hii inapelekea haja ya kuchukua tahadhari kwa ajili ya kulinda maisha ya wananchi wetu. Kwa hapa kwetu Zanzibar, hivi karibuni pia kumejitokeza wananchi wenzetu wengi kusumbuliwa na maradhi ya homa ya mapafu, homa kali na shida ya kupumua. Serikali inalielewa jambo hili na inalifuatilia kwa karibu sambamba na kuchukua jitihada kubwa sana kupitia wataalamu wetu ili kudhibiti hali hiyo.


Ndugu Wananchi;

Wakati serikali inaendelea na jitihada hizo, tunahitajika kuchukua tahadhari za kujilinda na maradhi haya sisi wenyewe na jamii inayotuzunguka. Ili kupunguza maambukizi ya maradhi yanayoambukiza katika jamii, kila mmoja wetu anatakiwa kuzingatia mambo yafuatayo: -


1) Tudumishe usafi wa mikono kwa kunawa mara kwa mara kwa maji tiririka na sabuni au vitakasa mikono (sanitizers);

2) Maeneo yote yanayotoa huduma kwa watu wengi ni vyema wahusika wakaweka sehemu na vifaa vya kunawia mikono kwa maji tiririka na sabuni au vitakasa mikono;

3) Tuepuke mikusanyiko isiyo ya lazima muda wote na pale tunapolazimika kukaa watu wengi kwa pamoja tukae kwa masafa ya angalau mita moja baina ya mtu na mtu; 

4) Wakati wote tunapotoka nje ya nyumba zetu hasa tunapokuwa katika mikusanyiko na watu tuvae barakoa hasa zile zilizotengenezwa kwa vitambaa hapa hapa nchini. Aidha inasisitizwa barakoa hizo zifuliwe kwa maji na sabuni kabla ya kutumia tena; 

5) Tunapokohoa au kupiga chafya tufuate masharti ya kiafya ikiwemo kufunika mdomo kwa kutumia kitambaa safi au kiwiko cha mkono; 

6) Kwa wale wenye dalili za kukohoa, mafua makali au shida ya kupumua tunatakiwa kuripoti Kituo cha Afya kilicho karibu ili kupata ushauri unaostahiki;

7) Tuwe na utaratibu wa kula chakula bora ikiwemo matunda na mboga mboga pamoja na kufanya mazoezi;

8) Wamiliki wa vyombo vya usafiri wa anga, baharini na nchi kavu wanapaswa kuwaongoza abiria na wafanyakazi wao kuchukua tahadhari zote za kiafya kama zinavyotolewa na wataalamu wetu wa afya kila mara;     

9) Taasisi zote za Serikali na zisizo za kiserikali zinasisitizwa kuweka mazingira mazuri ya kutekeleza masharti ya kiafya ili kujilinda na maradhi haya, ikiwemo kuweka vitakasa mikono katika maeneo mbalimbali, kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima na kuelimishana juu ya kinga ya maradhi ya kuambukiza katika maeneo ya kazi.


Ndugu wananchi;

Katika kukabiliana na tatizo hili, tunashauriwa kuendelea kutumia dawa zetu za kiasili kwa ajili ya kinga na tiba ya maradhi mbalimbali yanayotukabili. Aidha, tunawaomba wananchi waendelee kutulia na kusikiliza maelekezo ya wataalamu yatakayokuwa yakitolewa kupitia Wizara ya Afya au Taasisi nyengine za kiserikali. Ndugu wananchi tunaombwa tuendelee kumuomba Mwenyezi Mungu kwa kupitia imani zetu mbalimbali ili Taifa letu libaki salama kutokana na maradhi na majanga yanayoikumba dunia hivi sasa.  KILA MMOJA WETU AMUHIMIZE MWENZAKE. 


KUMBUKA: KINGA NI BORA KULIKO TIBA

MUNGU IBARIKI ZANZIBAR, MUNGU IBARIKA TANZANIA

AHSANTENI KWA KUNISIKILIZA


-------------------------------------------

Dkt Khalid Salum Mohamed  

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa 

Pili wa Rais Sera Uratibu na BLW

 


 Tarehe: 22 Februari, 2021

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.