Habari za Punde

Tamwa Zanzibar yaandaa mafunzo ya siku moja kujadili changamoto wanazokabiliana nazo wanawake wanapogombea nafasi za uongozi

Miongoni mwa washiriki wa majadiliano ya siku moja Thuwayba Jeni Pandu akitoa ushuhuda jinsi wanawake wanavyokabiliwa na changamoto wanapogombea nafasi za uongozi.
Miongoni mwa washiriki wa majadiliano ya siku moja yaliolenga kujadiliana namna bora ya kuwawezesha wanawake wa Zanzibar kushika nafasi mbali mbali za uongozi.
Afisa utafiti na tathmini kutoka TAMWA-Zanzibar Mohamed Khatib akitoa nenoa la shukrani kwa washiriki wa mafunzo ya siku moja yanayolenda kutafuta njia bora za kuwawezesha  wanawaek wa Zanzibar kushika nafasi za uongozi.


Na Muhammed Khamis,TAMWA

Hofu dhidi ya wanawake wasomi inaelezwa kuwa miongoni mwa vikwazo vikuu vinavyowakabili wanawake kushika nafasi za uongozi Zanzibar kupitia chaguzi mbali mbali zinazofanyika kila baada ya miaka mitano visiwani hapa.

 

Hayo yamelezwa na Thuwayba Jeni  Pandu katika mafunzo ya siku moja yalioandaliwa na TAMWA-Zanzibar yenye lengo la kutoa fursa za majadiliano na kujenga misingi bora kuwawezesha wanawake kushika nafasi za uongozi chini ya ufadhili wa shirika la umoja wa mataifa linalojihusisha na maswala ya wanawake (UN Woman)

 

Amesema kuibuka kwa wanawake wengi waliosoma na wenye uwezo katika maeneo mbali mbali Zanzibar ambao hushiriki kwenye kuwania nafasi za uongozi imeleta  hofu kubwa kwa baadhi ya wanasiasa wakongwe na kuhisi kuwa wanataka kuchukuliwa nafasi zao jambo ambalo lilipaswa kuwa wazi na kuona kuwa kila mtu ana haki sawa.

 

‘’Kwa mazingira haya wasomi wengi wenye jinsia ya kike hushindwa kufikia malengo yao na pia kuinyima jamii fursa ya kupata watumishi wazuri’’alifafanua.

 

Sambamba na hilo mshiriki huyo alizungumzia kuhusu changamoto ya ukosefu wa kifedha unaowakabili wanawake na kueleza kuwa kuna mfumo mbovu kwenye jamii ambao umezoeleka ikiwemo kuhisi kuwa ili mtu awe kiongozi anapaswa kutoa fedha kabla na hatimae aweze kuchaguliwa.

 

Nae Shadida Omar kutoka shirikia linalojihusisha na changamoto zinazowakabili vijana (ZAFAYCO) alisema zipo chanagamoto nyengine zinazowakabili wanawake kushindwa kushika nafasi za uongozi.

 

Akitaja chanagmoto hizo alisema ni pale wanawake  wanapotaka kufanya kampeni za usiku nyumba kwa nyumba wanakosa kuungwa mkono na waume zao na badala yake wanawake walio wengi hushindwa kufanya kampeni nyakati za usiku ambazo ni sehemu muhimu ya kutengeneza ushindi kwa kuwa wapiga kura wengi tayari huwepo majumbani.

 

Mshiriki mwengine ambae ni Huzaima Ally Hamdani alisema ili wanawake wafikie malengo yao lazima demokrasia iheshimike vyenginevyo wanawake wengi hawatajitokeza tena katika nafasi za kugombea.

Alitolea mfano uchaguzi mkuu uliopita yeye na wagombea wengine wa nafasi mbali mbali kwa kuwa ni wanawake walikosa nafasi za kusimamia kura zao kutokana na kukosa vitambulisho ambavyo vingewawezesha kusimamia kura zao.

 

Alisema kutokana na mazingira hayo hwend akinamama wengi wakashindwa kujitokeza kugombea katika nafasi mbali mbali uchaguzi ujao wa mwaka 2025.

 

Awali akiwasilisha mada Bi Salma Sadati alisema wakati umefika jamii kujitambua na kuwaunga mkono wanawake kwenye maeneo yao kwa kuwa wanawake wengi wana uwezo mkubwa kushika nafasi za uongozi.

 

Alisema Zanzibar kama sehemu ya Jamuhuri ya Muungano wanawake ni zaiid ya asilimia 50 ya wapiga kura hivyo ni wazi kuwa iwapo wanawake watawaunga mkono wanawake wenzao wataweza kufanikiwa.

 

Sambamba na hilo alisema ni lazima katiba za vyama vya siasa zibadilike na ziweke asilimia ya wagombea kwa kila nafasi za uongozi.

 

‘’Nafikiri hili ndio jambo la muhimu zaidi kufanyika na naamini kupitia mfumo huu wanawake walio wengi watakua viongozi kinyume na ilivyo sasa’’aliongezea.

 

Akifunga mafunzo hayo ya siku moja  Afisa utafiti na tathmini kutoka TAMWA-Zanzibar Mohamed Khatib alisema ipo haja wanawake kupewa fursa sawa za uongozi kwenye jamii.

 

Alisema wanawake ni watu kama walivyo wengine na kwamba wanastahili haki zote kwa mujibu wa katiba ikiwemo ya kushika nafasi za uongozi.

 

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.