Habari za Punde

Wazazi wanaowalazimisha watoto wao wa kike kufeli mitihani yao kisa ndoa kuchukuliwa hatua

Na Hamida Kamchalla, HANDENI.

BAADHI ya wazazi wilayani Handeni mkoani Tanga, wamedaiwa kuhusika katika kuwazuia watoto wao wa kike wasifanye vizuri kwenye masomo yao pamoja na mitihani ya mwisho ili wasiendelee na masomo na baadae wafungishwe ndoa, hali ambayo inachangia kuongezeka kwa utoro shule mbalimbali.

Hayo yalibainishwa juzi na Mwenyekiti kamati ya elimu, afya na maendeleo ya jamii baraza la madiwani halmashauri ya wilaya Handeni Nurdin Semnangwa wakati akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo kwenye baraza lililofanyika ambapo alisema kuwa, baadhi ya wazazi wanatakiwa kuchukuliwa hatua kali kwa tabia hizo.

Semnangwa alisema kuwa katika ufuatiliaji waliofanya wamebaini wapo baadhi ya wazazi ambao wanawashawishi watoto wao kufanya vibaya ili wafeli hasa wasichana, kitendo ambacho kinasababisha kushuka kwa ufaulu hasa shule za msingi na wale wanaotakiwa kwenda sekondari.

"Kwa hali hii inabidi tuwekeli mikakati ya kuthibiti utoro kama huu kwa wanafunzi wote na kwa upande wa wazazi watakaobainika kuwashawishi au kuwalazimisha watoto kufanya vibaya kuchukuliwa hatua za kinidhamu ili kuweza kukomeshwa kwa tabia hizo" alisema.

Kwa upande wake Diwani kata ya Kiva Valentino Mbuji akichangia mada hiyo alisema kuwa licha ya wanafunzi kutofanya vizuri na kufeli pia wapo walimu ambao wana umri wa kufananishwa na watoto shuleni na wao pia husababisha kushuka kwa ufaulu kwani hawafuati taratibu za kiutendaji.

Alisema wapo walimu hawaishi kwenye maeneo wanayofundishia hivyo hali hiyo inasababisha washindwe kufika kazini kwa muda unaotakiwa, jambo ambalo linaathiri ratiba za ufundishaji, hivyo kushauri ofisi ya mkurugenzi kuliona suala hilo na kulifanyiakazi kwa haraka ili kunusuru taaluma mashuleni.

"Miundombinu yetu ni mibovu lakini walimu wanaishi nje ya vituo vya kazi hivyo ikitokea dharula aidha mvua na masuala mengine ya kifamilia wanashindwa kuhudhuria darasani na kuathiri ratiba za ufundishaji, mkurugenzi alione hili kwani pia linasababisha kushuka kwa ufaulu", alisema Mbuji.

Mkurugenzi halmashauri ya wilaya Handeni William Makufwe alisema wameshafanya vikao na wataalam pamoja na wadau kuhusu kupandisha ufaulu kwa halmashauri hiyo kwa msimu wa masomo ujao na kuongeza kuwa mpaka sasa ufaulu wao umepanda kutoka asilimia 87 kwa mwaka 2019 mpaka 88.7 kwa mwaka jana na mwaka huu mpango wa halmashauri ni kuongeza ufaulu zaidi ya huo wa sasa.

Hata hivyo Makufwe aliagiza walimu wote watoro wachukuliwe hatua za kinidhamu haraka kwani amebaini asilimia 50 ya walimu, wanachukua ruhusa ambazo zipo nje ya utaratibu wa utumishi wa umma ambao unatakiwa kufuatwa.

"Tumeboreshaji suala la chakula kwa shule za msingi wanafunzi wanapata chakuka kwa asilimia 90 huku sekondari wakifikia asilimia 100, hivyo hili suala la walimu idara husika iwachukulie hatua walimu husika kwani kuna kamati yangu inafuatilia asimilia 50 ya walimu hawapo kwenye vituo vyao," alisema Makufwe.

Katika matokeo ya mwaka jana halmashauri ya wilaya Handeni imeshika nafasi ya tatu kimkoa baada ya Tanga jiji kushika nafasi ya kwanza, Handeni mji kushika nafasi ya pili.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.