Na Eleuteri Mangi-WHUSM, Dodoma.
Kifo cha Dkt. John Pombe
Joseph Magufuli ambaye alikuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania si pigo tu kwa nchi, bali ni pigo katika tasnia ya Sanaa nchini.
Akitoa hotuba yake wakati wa
mazishi ya Kitaifa ya Hayati, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan aliwashukuru Watanzania kwa
kuonesha umoja, mshikamano na upendo kwa kujitoa kwa moyo wakati wote tangu
msiba utokee.
“Asanteni sana wananchi kwa
kujitokeza kwa wingi kumuaga kipenzi chetu, watu wametandaza nguo barabarani hii
ni namna ya kuenzi utu wake, kazi zake alizofanya, uzalendo wake kwa taifa,
maisha yake yote aliitanguliza Tanzania. Vizazi na vizazi watasimulia hadithi
nzuri” alisema Rais Samia.
Kwa upande wake Waziri Mkuu
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa ambaye pia ni Mwenyekiti wa
Kamati ya Mazishi ya Viongozi wa Kitaifa aliwashukuru wasanii kwa kuendelea kuimba
nyimbo za maombolezo ambayo yatadumu kwa siku 21 tangu kutokea kifo cha mpendwa wetu Hayati
Dkt. Magufuli.
“Wasanii endeleeni kutoa faraja
kwa kipindi chote kwa kutoa hisia zenu na kuwashirikisha Watanzania kufarijiana
wakati wa kipindi chote cha kumuaga kipenzi chetu Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Baba wa Taifa Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere Rais wa Awamu ya Kwanza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitambua
umuhimu wa Sanaa na utamaduni katika taifa kwa kusema, “Utamaduni ni kiini cha taifa lolote, nchi
isiyo na utamaduni wake ni sawa na mkusanyiko wa watu wasio na roho ambayo
inayofanya taifa.”
Sekta ya Sanaa ni nguvu laini (soft power) ya kuhamasisha jamii
kushiriki katika shughuli zote za kijamii ambapo sekta hiyo inasimamiwa na Wizara
ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Ni dhahiri Dkt. Magufuli
amekuwa Rais wa kwanza kuunda wizara yenye sekta ya sanaa inayojitegemea na
kuwafanya wasanii watembee kifua mbele kwa kushiriki kazi mbalimbali za
Serikali ikiwemo matamasha na dhifa za kitaifa.
Aidha, Hayati Dkt. Magufuli
alijipambanua kwa kupenda kazi za Sanaa ambapo wakati wa uhai wake alipokuwa
akitekeleza majukumu yake aliwatumia wasanii na kila mara alisikika akisema “Ni
lazima wasanii wetu wanufaike na matunda ya kazi zao za Sanaa.”
Tangu kutangazwa msiba wa
Hayati Dkt. Magufuli Machi 17, 2021, tumeshudia wasanii mbalimbali wakiandaa na
kuimba nyimbo za maombolezo zinazosadifu utendaji kazi wake ambazo wanaendelea
kuziwasilisha kwa jamii kwa umahiri mkubwa kwa kuwapa familia na Watanzania
faraja.
Enzi za uhai wake akiwa
kiongozi Mkuu wa nchi, katika moja ya hotuba zake Dkt. Magufuli akihitimisha
Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jijini Dodoma, Juni 16, 2020
alisema Sanaa ni sekta ambayo ina mchango mkubwa katika uchumi wa nchi.
“Sekta nyingine, ambayo
haijasemwa sana lakini kwa sasa ina mchango mkubwa kwenye uchumi wetu ni sanaa
na utamaduni. Kwa mujibu wa Taarifa ya Hali ya Uchumi ya mwaka 2018, shughuli
za Sanaa na Burudani ziliongoza kwa ukuaji mwaka 2018 ambapo ilikua kwa
asilimia 13.7 na mwaka 2019 ilishika nafasi ya tatu kwa ukuaji wa asilimia
11.2, hongereni sana wasanii wetu mbalimbali, hususan wa Bongo Fleva na Filamu.
Kazi zenu sio tu zinaburudisha na kuchangia ukuaji uchumi, lakini pia zinaitangaza
nchi yetu kimataifa”, Hayati Dkt. Magufuli.
Katika maombolezo ya msiba
huu, wasanii kupitia tungo zao wameonesha jinsi walivyoguswa wakisema Dkt.
Magufuli amewaachia Watanzania majonzi, simanzi kwenye mioyo yao.
Moja ya wimbo waliotunga
wasanii umebainisha kuwa kazi aliyoitiwa duniani Dkt. Magufuli ameimaliza,
ametumika kikamilifu utumishi wake hautasahaulika nchini, nenda salama
tutakukumbuka daima buriani Mwanamageuzi mahiri.
Wakati wa mazishi ya kitaifa
yaliyofanyika Machi 22, 2021 Wasanii “Tanzania all-stars” waliimba wimbo maalum usemao “Tusihuzunike
bado tumaini lipo”, tutakukumbuka daima maana tulikupenda sana, pumzika kwa amani.”
Ujumbe wa wasanii hao unaonesha
umahiri wa jinsi Dkt. Magufuli alivyoongoza nchi na kuheshimu kazi yake ya kishujaa,
kijasiri na uhodari katika kufanya mapinduzi ya kweli katika sekta mbalimbali
ikiwemo sanaa na kusema Watanzania wataikumbuka kaulimbiu yake ya ‘Hapa Kazi Tu.’
Naye Katibu Mkuu wa Wizara
ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hasaan Abbasi
amesema “Katika uhai wake kama kuna kitu Hayati Dkt. John Pombe Magufuli
alikipigania na kukipangia kukipigania zaidi kikue zaidi ni sekta ya sanaa.
Katika kampeni zake wakati
wa Uchaguzi Mkuu mwaka 2020, neno wasanii lilikuwa kinywani mwake sana, kiasi
cha kuambatana nao kwenye kampeni zake. Taswira hiyo ilianza kuonekana tangu mwaka
2015 ambapo amekuwa Rais wa kwanza kuunda wizara yenye sekta ya sanaa kama
sekta inayojitegemea.
“Leo hatuko naye mtu huyu
Dkt. John Pombe Magufuli, bingwa katika kuipigania sekta ya sanaa, anapaswa
kuimbiwa, nyimbo za maombolezo, nyimbo za kumwombea pumziko la amani na la
milele. Hivyo Machi 25 kuanzia saa 10 kamili jioni hadi saa moja katika uwanja
wa Magufuli hapa Chato tumewapa nafasi wasanii wote watakaoweza kufika Chato na
waliokwishafika Chato kumuimbia Magufuli kwa nyimbo mbalimbali za maombolezo
walizozitunga mmoja mmoja na kama makundi,” alisema Dkt. Hasaan Abbasi
Kwa kutambua na kuthamini
kazi ya Hayati Rais Dkt. John Pombe Magufuli, baadhi ya wasanii wameshiriki
kuimba kwa pamoja wimbo maalum wa maombolezo chini ya usimamizi wa Wizara ya
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).
Wasanii hao ni pamoja na
Nandy, Marioo, Dogo Janja, Young Lunya, GoodLuck Gozbeth, Christina Shusho,
Majid, JayMelody, Khadija Kopa, Mzee Yusuph, Mrisho Mpoto, Jesca Mshama, Linah,
Hamadai, Whozu, Stamina, Merissa, Meja Kunta, Mzee Kalala na Ndelah.
No comments:
Post a Comment