Habari za Punde

Mjue Mwanariadha Chipukizi Mtumwa Ali Haji



 NA MWAJUMA JUMA

HAKUNA kitu ambacho kimeletwa duniani kikakosa kutambulika kilipoanzia na mwisho wa kumalizia kwake.

Nasema hivi kwa sababu ya kile ambacho ninachoamini hakuna marefu yanayokosa mapana yake. 

Na kwa mantiki hiyo naweza kusema kuwa hata mbuyu nao ulianza kama mchicha na kukua hadi kufikia kutambulika na kutajikana dunia nzima kwa ukubwa wake.

Hivyo katika makala haya nilizungumza na mwanariadha chipukizi wa timu ya Mafunzo ambae alitambulika kwa jina la Mtumwa Ali Haji.

Mtumwa ambae katika timu hiyo anarusha mkuki anasema kuwa amechaguwa kurusha mkuki kwa sasabu ni anaupenda na umshamletea mafanikio kwa kuipatia ubingwa timu yake mara moja. 

Alisema kuwa pamoja na kuwa amejiunga na timu hiyo kwa muda mchache lakini michezo alianza kushiriki tokea akiwa anasoma skuli.

Mtumwa ambae alizaliwa Febuari 21/2001 alisema kuwa alijiunga na timu ya Mafunzo akiwa anasona kidato cha pili mnamo mwaka 2018 lakini fani ambayo anaipenda ni kurusha mkuki.

“Narusha Mkuki, Tufe na Kisahani lakini mkuki ndio napenda sana na hii ishanipatia medali ya dhahabu mara moja”, alisema.

Hata hivyo alisema kuwa wakati anaanza kushiriki michezo hakushawishiwa na mtu na aliamuwa tu mwenyewe kwa kile ambacho anaamini kwamba michezo ni afya.

“Sikushawishiwa na mtu kushiriki michezo kwa sababu najuwa kwamba unaposhiriki michezo unajenga mwili na kuepukana na homa za mara kwa mara”, alisema.

Hata hivyo alisema kuwa kitu ambacho kilimsukuma kushiriki michezo ni kuona kwamba atapata fursa mbali mbali ikiwemo kutembea na kuongeza idadi ya marafiki.

Alisema tokea kuanza kushiriki michezo hajatembea sana kutokana na muda mchache lakini ametembea Mtwara katika mashindano ya Umiseta yaliyofanyika mwaka juzi pamoja na Pemba katika klabu bingwa.

Alisema akiwa Mtwara timu yao ilifanikiwa kupata kikombe na medali za dhahabu na fedha.

“Sikumbuki tulitokea mshindi wa ngapi Pemba n ahata huko Mtwara lakini ninachokijuwa ni kwamba tulipata kikombe na medali”, alisema.

Alifahamisha kwamba katika mashindano hayo kwa upande wao yalikuwa ni magumu sana kutokana na maandalizi ya timu ambazo walizocheza nazo.

Alieleza kuwa wenzao walikuwa na maandalizi mazuri tofauti na wao hali ambayo iliwapa wakatyi mgumu wakati wanapokutana nazo.

“Tulikuwa katika wakati mgumu lakini tulipambana na kufikia ambapo tulifika”, alisema.

Hata hivyo alisema kwamba mafanikio ambayo ameyapata ni pamoja na kupata medali ya dhahabu na kusafiri pamopja na kuongeza idadi ya marafiki.

“Sina mafanikio makubwa ambayo nimeyapata mpaka lakini kwa hapa nilipofikia nashukuru mungu”, alisema.

Aidha mchezaji huyo ambae ni mzaliwa Mpapa wilaya ya Kati Unguja na ndio sehemu anayoishi alisema matarajio yake ni kutaka kufika mbali na kuwa mchezaji wa kulipwa.

Mbali na kuwa mchezaji wa kulipwa lakini kupitia michezo hiyo anatarajia sana kupata ajira ili aweze kujiendesha yeye na familia yake.

Kwa upande wa changamoto ambazo anapitia ni suala zima la vifaa pamoja na nauli kutokana na kuwa yeye pamoja na kuwa anachezea timu ya taasisi lakini bado sio muajiri rasmi.

Hivyo anategemea sana nauli ya kuja na kurudia Mpapa kila siku anapokuja mazoezi utoka kwa waalimu wao ambao ndio wanaomsaidia.

“Sina changamoto nyingi ambazo ninakumbana nazo isipokuwa suala la nauli maana tunapata nauli kutoka kwa waalimu wetu jambo ambalo nahisi kuna siku na wao kama binadamu wanaweza kukosa”, alisema.

Hivyo aliwaomba viongozi wakuu wa Mafunzo kuliangalia hilo kwa kuwajaalia angalau posho ya mwisho mwezi ili waweze kujikimu.

Alisema changamoto nyengine anaipata lakini kutokana na msimamo wake anaichukulia ni kawaida ni kufatwa fatwa na baadhi ya wachezaji wa kiume kumtaka kimapenzi.

Alisema kwa kuwa anajuwa lengo ambalo limemfikisha hapo anawapuuzia na kufanya lile ambalo ameliendea hapo.

Sambamba na hayo alisema kuwa michezo ni sehehmu ya starehe na ni furaha ambayo inawaleta watu kuwa karibu hivyo aliwataka wanawake na vijana kuipenda michezo.

“Nawasihi wanawake wenzangu na vijana kwa ujumla waipende michezo na wasibweteke kukaa tu nyumbani, waje washiriki michezo ili kuwaweka karibu zaidi na watu wengine”, alisema.

Aidha aliwataka wanafunzi kuondoa dhana kwamba kushiriki michezo kunaondoa akili ya kimasomo bali inategemea na jitihada za mwanafunzi mwenyewe katika michezo.

Alisema kuwa yeye alishiriki michezo akiwa kidato cha pili kuelekea kufanya mitihani ya kuingia kidato cha tatu, alifaulu na kuingia mpaka kidato cha nne.

Alisema katika kidato cha nne ndio alishindwa kuendelea na masomo na hakupata cheti kizuri lakini haikuwa kwa sababu ya kushiriki michezo.

Alisema kuwa alimaliza masomo kidato cha nne na kushindwa kuendelea kutokana na familia yake kutokuwa na uwezo wa kumuendeleza.

Hata hivyo aliishauri Serikali kuwekeza zaidi katika michezo na kuwaunga mkono vijana ambao wamejitolea ili kuzidi kuimarisha michezo zaidi.

Alifahamisha kwamba kitu ambacho anakichukia katika maisha yake ni kukatazwa kitu ambacho anakifanya kwa kujuwa kama kina maslahi kwake ikiwemo suala zima la kwenda kwenye mazoezi.

“Kwa kweli mtu akinikataza kwenda mazoezi nachukia sana kwa sababu haya mazoezi ndio ambayo yananijenga mimi na kuonekana kuwa na afya nzuri kila wakati”, alisema.

Aidha alisema kuwa mchezaji ambae anamvutia katika riadha kwa Zanzibar ni Ali Gulamu.

Mtumwa ni mtoto wa tatu kuzaliwa katika familia ya watoto saba ya bibi Asha Jimbo Shaka na bwana Ali Haji wanaoishi Mpapa.

Mtumwa alisema kuwa anawashukuru sana wazazi wake kwa kumruhusu kushiriki michezo na kusema kuwa wamekuwa wakimpa mashirikiano mazuri kila wakati.

Alisema kuwa wazazi wake pamoja na kuwa wanaishi kijijini lakini wamekuwa wakimuunga mkono sana katika suala zima la kushiriki kwenye michezo tokea akiwa mdogo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.