Habari za Punde

Ukosefu wa elimu ya uongozi na utawala bora changamoto kwa vikundi vya ujasiriamali

Afisa sheria kutoka Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, utumishi wa Umma na Utawala bora Zanzibar,  Bakar Omar Ali akitoa mafunzo kwa viongozi wa vikundi vya ushirika wakati wa mafunzo kupitia mradi wa VIUNGO.
Viongozi wa vikundi kisiwani Pemba wakiendelea na mafunzo ya uongozi na utawala bora kupitia mradi wa VIUNGO
 

IMEELEZWA kwamba ukosefu wa elimu ya uongozi na utawala bora kwenye vikundi vya ujasiriamali hupelekea vikundi vingi kukumbwa na migogoro mbalimbali inayopelekea kushindwa kufikia malengo yake.

Hayo yameelezwa na Bakar Omar Ali, afisa sheria kutoka Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, utumishi wa Umma na Utawala bora wakati wa mafunzo ya uongozi na utawala bora kwa wakulima na viongozi wa vikundi kisiwani Pemba kupitia mradi wa Viungo, Mboga na Matunda unaotekelezwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ), People’s Development Forums (PDF), na Community Forests Pemba (CFP) kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU).

Alisema licha ya wadau kujitahidi kuchukua juhudi kubwa kuhamasisha wananchi kujiunga na vikundi kwaajili ya kujikwamua kiuchumi lakini bado vikundi hivyo vimekuwa vikikabiliwa na migogoro ya hapa na pale ambayo chanzo chake kikubwa ni ukosefu wa misingi ya utawala bora ndani ya vikundi hivyo.

Alieleza suala la uongozi bora kwenye vikundi ni muhimu katika usitawi wa maendeleo ya wanawake hasa wanachama wa vikundi hivyo ili kutimiza malengo ya uanzishwaji wa vikundi.

“Vikundi vingi vinaanzishwa kila siku lakini havidumu kutokana na kukosekana kwa misingi hii ya utawala bora, na ukifuatilia migogoro mingi inayojitokeza kwenye vikundi chanzo chake utakuta ni ukosefu wa viongozi bora,” alisema.

Aliongeza kutokana na hali hiyo kuna haja kwa wadau wa maendeleo kuongeza nguvu katika utoaji wa taaluma ya uongozi na utawala bora kwenye vikundi hivyo ili viweze kufikia malengo ya kuwasaidia wananchi kujiendeleza kiuchumi kupitia shughuli mbalimbali katika jamii.

Alisema, “ tuwapongeze wasimamizi wa mradi huu wa Viungo kwa kuliona hili na kuamua kuja na mafunzo haya kwa wanufaika wa mradi huu kwani hii itasaidia kuondoa migogoro ndani ya vikundi inayopelekea vikundi kufa na kushindwa kufikia malengo ya kuanzishwa kwake.”

Alibainisha kwamba ujio wa mradi huo utasaidia kutatua changamoto zinazowakabili wakulima hasa wanawake kupitia vikundi vya ujasiriamali na hatimaye kuvifanya vikundi hivyo kuwa ni mkombozi kwao.

“Wanawake wengi ambao kwa kiwango kikubwa ndio wanajishughulisha na vikundi wamekuwa wakishindwa kupata mafanikio sahihi ya kujikwamua kiuchumi kupitia vikundi vyao kutokana na vikundi vingi kukosa misingi imara ya uongozi katika kusimamia shughuli zao hivyo mbinu hii ya mradi huu itarejesha matuamini ya wanawake katika vikundi vyao,” alisema.

Afisa uwezeshaji wanawake kiuchumi wa mradi huo, Asha Mussa Omar alisema mafunzo hayo yamekuja baada ya mradi kugundua kwamba vikundi vinashindwa kudumu na kufikia malengo kutokana na ukosefu wa uongozi imara na hivyo taaluma hiyo itawasaidia kutambua misingi ya utawala bora katika uendeshaji wa vikundi vyao.

Alibainisha malengo ya mradi ni kuwawezesha wanawake kujiinua kiuchumi kupitia shughuli za kilimo cha mboga, viungo na matunda hasa kupitia bustani ya nyumbani pamoja na uwekaji wa hisa na kwa asilimia 55%.

“Mradi huu unawalenga zaidi wanawake kwa asilimia 55% ambapo watanufaika kupitia kujihushisha na shughuli za kilimo cha Viungo, Mboga na Matunda, ikiwa ni pamoja na kujiunga na vikundi vya kuweka na kukopa ambavyo vitawasaidia kuongeza vipato vyao,” alisema.

Mshiriki wa mafunzo hayo, Fatma Shaame alipongeza uamuzi wa mradi kutoa taaluma hiyo kwani tatizo hilo limekuwa kilio chao kwa muda mrefu jambo linalopelekea wananchi wengi kukata tamaa ya kujiunga na vikundi hivyo.

 “Tatizo la kuvunjika kwa vikundi chanzo chake ni viongozi kukosa uwajibikaji na hii inatokana kwamba kwenye vikundi tunachaguana bila kujali misingi ya utawala bora. Tunashukuru mradi kuja na fursa hii kwani sasa itaenda kuimarisha vikundi vyetu, alisema.

Mafunzo hayo ya siku mbili ambayo yamejumuisha wakulima na viongozi wa vikundi 104 kutoka shehia zote 24 za Pemba ambazo mradi wa Viungo unatekelezwa ni mwendelezo wa utekelezaji wa mradi huo ambao unalenga kuongeza uzalishaji wa mazao ya Viungo, mboga na matunda sambamba na kipato kwa wakulima wa mazao hayo.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.