Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi Azungumza na Katibu Mkuu Kiongozi Ikulu Zanzibar.

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk, Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Katibu Mkuu Kiongozi wa Jamuhri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally, alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo na kujitambulisha leo 10-3-2021 na (kushoto kwa Rais) Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said, mazungumzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akisalimiana na Katibu Mkuu Kiongozi Mhe.Balozi Dkt. Bashiru Ally, alipowasili katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo na kujitambulisha

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la MapinduziDk. Hussein Ali Mwinyi amemuahidi kumpa mashirikiano makubwa Balozi Dk. Bashiru Ally Kakurwa, Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili aendelee kutekeleza vyema majukumu yake.

Ahadi hiyo aliitoa leo alipofanya mazungumzo na Balozi Dk. Bashiru Ally Kakurwa, Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzaniawakati alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa lengo la kujitambulisha kwa Rais kufuatia kuteuliwa kushika wadhifa huo.

Katika maelezo yake, Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba yeye mwenyewe pamoja na viongozi wote wa Serikaliya Mapinduzi ya Zanzibar wataendelea kumpa mashirikiano makubwa Balozi Dk. Kakurwa kwa azma ya kufanikisha majukumu yake ipasavyo.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa mashirikiano ya pamoja yanahitajika ili kufikia malengo yaliyokusudiwa katika kuwatumikia wananchi wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili wazidi kupata maendeleo endelevu.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alimpongeza Balozi Dk. Bashiru Ally Kakurwa, Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo na kueleza matumaini yake makubwa kwa kiongozi huyo kutokana na kuutambua uchapakazi wake mahiri alionao.

Nae Balozi Dk. Bashiru Ally Kakurwa, Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alieleza kwamba ana mategemeo makubwa kwamba ataendelea kupata mashirikiano kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na viongozi wake wote.

Balozi Kakurwa alimuahidi Rais Dk. Mwinyi kwamba atahakikisha mashirikiano yanaimarika zaidi kati yake na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Muhandisi Zena Ahmed Said ili shughuli zao ziende sambamba.

Aidha, Balozi Dk. Kakurwa alitoa shukurani kwa pongezi alizozipata kutoka kwa Rais Dk. Mwinyi baada ya kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Joseph Magufuli kuwa Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzaniakuchukua nafasi ya Balozi John Kijazi aliyefariki dunia Februari 17,2021.

Mapema Balozi Dk. Bashiru Ally Kakurwa, Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alikutana na kufanya mazungumzo na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Muhandisi Zena Ahmed Said hapo ofisini kwake Ikulu Jijini Zanzibar.

Katika mazungumzo hayo viongozi hao kwa pamoja waliahidi kuimarisha mashirikiano yaliopo sambamba na kuendelea kuratibu shughuli zao kwa mashirikiano ya pamoja ili waweze kutekeleza vyema majukumu yao.

Balozi Dk. Bashiru Ally Kakurwa, Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli mnamo Februari 26,2021 kushika wadhifa huo pamoja na kumteua kuwa Balozi na hatimae kuapishwa Februari 27, 2021 Jijini Dar-es-Salaam.

Balozi Dk. Kakurwa ambaye mnamo Mei, 2018 aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa CCM akichukua nafasi ya Abdulrahman Kinana ambapo kabla ya uteuzi wake huo ndani ya CCM, Balozi Dk. Bashiru alikuwa Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam(UDSM) katika Idara ya Sayansiya Siasa ambapo pia, alikuwa akiongoza Kurugenzi ya Mijadala na Makongamano.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.