Habari za Punde

Wanafunzi wa Skuli za Maandalizi Watakiwa Kuchukua Tahadhari Kipindi Cha Mvua za Masika

Na Maulid Yussuf.  WEMA Zanzibar

Wanafuzi wa elimu ya maandalizi  na msingi wametakiwa kuchukua tahadhari katika kipindi cha mvua za masika zinazotarajiwa kuanza mwezi wa machi hadi ili kuepuka majanga yanayoweza kutokea.

Afisa upimaji wa Afya za wanafunzi kutoka kitengo cha Elimu mjumuisho na stadi za maisha  bwana Mohammed Idarous Mohammed, ametoa wito huo wakati alipotoa elimu kwa Wanafunzi wa Skuli ya msingi Kisiwandui juu ya namna ya kuchukua tahadhari pamoja na mambo ya kufanya katika kipindi hicho cha mvua.

Amewataka wanafunzi hao kutotupa taka ovyo na badala yake watupe katika maeneo maalum yaliyowekwa, pamoja na kuacha tabia ya kujisaidia ovyo ili kuepuka kuenea kwa taka au uchafu ambao unaweza kusababisha maradhi mbalimbali yakiwemo ya kuharisha pamoja na maradhi ya miripuko.

Pia amewataka wanafunzi hao kutokubali kunywa maji yaisiokuwa salama, na badala yake wawashajiishe wazazi au walezi wao kuchemsha maji ya kunywa au kuyatia dawa, kwani msimu wa mvua ardhi inakuwa na unyevunyevu na hivyo visima vinauwezekano wa kuchanganyika na uchafu.

Aidha Afisa Mohammed amewataka wanafunzi hao kutochezea maji yaliyotuwama kwani yanaweza kuwasababishia majanga yakiwemo ya kuzama na kusababisha vifo au kupata maradhi mbalimbali yakiwemo ya ngozi.

Hata hivyo amewaomba wazazi na walezi kuwa karibu zaidi na watoto wao hasa wenye mahitaji maalum katika kuwalinda na kuwasaidia hasa katika kipindi hicho cha mvua zitakapoanza kunyesha ili kuwaepusha na majanga mbalimbali.

Kwa upande wake Msaidizi mwalimu Mkuu wa Skuli ya Msingi Kisiwandui na msimamizi wa kituo cha masuala ya elimu mjumuisho , mwalimu Kawthar Abdallah Mohammed ameishukuru kitengo hichocha Elimu mjumuisho kwa kuamua kuwapatia elimu wanafunzi wake kwani wamekiwa ndio miongoni mwa waathirika wa mvua za masika zinaponyesha kutokana na kujaa maji ndani ya Skuli yao.

Kitengo cha Elimu Mjumuisho kinatoa elimu hiyo kwa Wanafunzi wa Skuli mbalimbali za msingi kutokana na kutolewa dondoo muhimu na mamlaka ya hali ya hewa juu ya Msimu wa mvua za masika, ili kuweza kuwaelimisha wanafunzi kujikinga na athari mbalimbali zinazoweza kujitokeza.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.