Habari za Punde

Serikali ya Ummoja wa Kitaifa ni Ishara ya Matumaini ya Faraja Kubwa Kwa Jamii.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe.Othman Masoud Othman akisalimiana watoto katika kijiji cha Basra wilaya magharibi A Unguja akiwa katika ziara yake ya kuwatembelea wagonjwa Kisiwani Unguja.

Na.Talib Ussi -Zanzibar.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Othman Masoud Othman amesema uwepo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa hapa visiwani ni ishara ya matumaini na faraja kubwa kwa jamii na pia muendelezo wa utamaduni wa  kusaidiana kutembeleana miongoni mwa wakaazi wa asili wa visiwa hivyo.

Makamu  aliyasema hayo katika ziara iliyoandaliwa na chama cha ACT wazalendo kwa minaajili  ya kuwatembelea na kuwafariji wagonjwa, katika mitaa na vijiji vya Wilaya Magharibi A na B katika  kisiwa cha Unguja akiwa amembatana na ujumbe wa uongozi wa chama hicho kwa upande wa Zanzibar.

Mhe.Othman alisema Zanzibar ya sasa inashuhudia faraja hiyo ikiwa ni pamoja na ziara za Viongozi wakuu wa nchi kuwasogelea, kuwajulia hali na ikibidi kuwasaidia watu wa namna tofauti hasa katika Mwezi mtukufu wa Ramadhanlitaja

Faraja hii ni maendelezo wa utamaduni wetu wa asili na zama tangu mababu na mabibi zetu na hatuwezi kuupoteza", alisema Othman.

Makamu wa kwanza katika ziara hiyo akiwa pamoja  na ujumbe wake walitembelea wagonjwa katika mitaa ya Mfenesini Maryam Miraji , Said Juma Suleiman wa Kihinani, Said Ali Hamadi wa Bububu, Omar Abdalla Malik wa Sharifumsa, Sada Mwinyi Omari wa Basra, Aziza Said Ali wa Welezo.

Wengine ni Mbarouk Juma Juma wa Mwera, Salim Ali Said wa kinuni, Said Abdalla Said wa Pangawe Ameir Abdalla wa Fuoni Migombani ,Khatibu Khamis wa  Kwarara, Hamadi Said wa  Mshelishelini . na Abdalla Khator wa Kiembesamaki.

Katika shehia ya Sharifu Msa, Mtaa wa Beitras alimtembelea Mzee Omar Abdallah Maliki ambaye anasumbuliwa na maradhi ya baridi kwa muda mrefu.

Pia Makamu katika ziara yake hiyo alimtembelea kijana Mbarouk Juma Juma miaka 20 katika kijiji cha Mwera Magetini  ambaye inadaiwa kupata majeraha muilini kutokana na vurugu za uchaguzi mwaka jana.

Kiujumla katika ziara yake hiyo Makamu wa Kwanza wa Rais aliwatembelea wagonjwa pamoja wazee 13 kwa wilaya zote.

Akiwa katika kuwangalia wagonjwa hao aliwaomba kuwa na subra na yeye amefika hapo kuwafariji kutokana maradhi ambayo yamewakuta.

Akifafanua zaidi alisema kuwa mwenendo huo ni wa kuenziwa na wenye thamani ya pekee katika kubaini na kukabili moja kwa moja baadhi ya changamoto na matatizo ya wananchi.

makamu Othman ameahidi kufuata nyayo za mtangulizi wake, Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad ambaye ataendelea kukumbukwa daima katika kupigania faraja ya watu wa nchi hii.

“Tunashukuru wazee wetu kutuachia urithi huu wa kutembelea na kujuana hali zetu na mimi naahidi kuendeleza na yanayofanana na hayo”

Sambamba na hilo makamu huyo alisema jambo la kuwatembelea wagonjwa kwa mujibu wa kiongozi mkuu wa Uislamu Duniani Mtume Muhammad swalallah Alaihi wasalam (S.A.W) ni ibada kubwa na kuwamba Viongozi na wenye uwezo kufanya hivyo hasa katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani bila kujali uwezo wao au vyeo vyao.

Alisema kuwa kiongozi wa kweli ni Yule anayewafanya wananchi kuwa na furaha na amani ya moyo na taifa kwa ujumla na kudai hilo linapatikana katika kuwatembelea na kujua shida zao.

Alisema itakuwa vyema kwa viongozi na wale wenye uwezo wa kipato kuendeleza utamaduni huoo huku wakitoa sadaka kwa wale wanaowatembelea ili kuwapa faraja.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.