Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe Hemed Suleiman Amejumuika na Wananchi wa Mikoa Miwili ya Pemba Katika Futari

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla akijumuika na Wananchi wa Mikoa Miwili ya Pemba katika futari aliyoandaa katika ukumbi wa kiwanda cha makonyo Wawi Chakechake Pemba
Baadhi ya Viongozi na Wananchi wa Mikoa Miwili ya Pemba wakijipatia chakula kwenye Futari ya pamoja mwishoni mwa Kumi la kwanza la Rehma hapo Ukumbi wa Makonyo Wawi.

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na Waumini wa Dini ya Kiislamu baada ya Sala ya Tarawehe katika Msikiti wa Mkoroshoni.

Picha na – OMPR – ZNZ.
Na.Othman Khamis.OMPR.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla alisema Taifa linahitaji kuendeshwa  katika misingi ya ushirikiano kati ya Viongozi na Wananchi ili lijielewe kule linalokusudia kuelekea katika kuihudumia Jamii.

Akizungumza na Waumini wa Dini ya Kiislamu mara baada ya kukamilika kwa Ibada ya Sala ya Ishaa na Tarawehe ndani ya Msikiti wa Ijumaa wa Mtaa wa Mkoroshoni Chake Chake Pemba Mh. Hemed alisema hivi sasa tayari Wananchi wameshaunganishwa pamoja katika mfumo huo.

Alisema Mtoto lazima asimamiwe kwa nguvu za Mzee wake tabia itakayosaidia kupata nguvu za pamoja katika uchungaji wa malezi yatayochangia kurejesha Maadili ya Taifa yaliyotetereka kutokana na mchanganyiko wa Silka na Tamaduni za Kigeni.

Aliwakumbusha Wazazi na Wazee wa Mtaa huo wa Mkoroshoni ambao yeye binafsi aliwahi kuishi kurejesha mfumo wa zamani wa kuwa na vikundi vya Polisi Jamii vinavyosaidia kuondosha vitendo viovu ikiwemo wizi, matumizi ya Dawa za kulevya pamoja na vitendo vha Udhalilishaji.

Mheshimiwa Hemed aliwaeleza Waumini na Wananchi hao kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane imejikita kwa nguvu zake kuwaondoshea changamoto zinazowakabili Wananchi katika maeneo yao akizitaja kuwa ni pamoja na upatikanaji wa huduma za Maji Safi, Afya Miundombinu ya Mawasiliano ya Bara bara.

Mapema magharibi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman aliwapongeza na kuwashukuru Wawakilishi wa Wananchi wa Mikoa Miwili ya Pemba kwa ushiriki wao wa Futari ya pamoja aliyoiandaa na waliamua kuacha Familia zao ikionyesha ni ishara ya upendo.

Mheshimiwa Hemed alisema hayo katika salamu zilizotolewa kwa niaba yake na Msaidizi Katibu wa Mufti Mkuu wa Zanzibar Ofisi ya Pemba Sheikh Said Ahmad Moh’d  baada ya kukamilika kwa futari hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Kiwanda cha Makonyo Wawi Chake Chake Pemba.

Alisema muitiko ni wajibu katika mfumo wa mwenendo wa Dini ya Kiislamu unaopaswa kuendelezwa ili uzidishe ushirikiano kama ni jambo la msingi linalostahiki kufanywa sera ya kuunganisha nyoyo za waumini  na hasa Wananchi Mitaani.

Mheshimiwa Hemed Suleiman yuko Kisiwani Pemba kuungana na Waumini wa Dini ya Kiislamu na Wananchi katika matukio tofauti ya Ibada yanayoendelea kutekelezwa ndani ya Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani unaoingia Kumi la Pili sasa la Maghfira.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.