Habari za Punde

NMB yaendesha semina ya walimu kuwapa elimu ya fedha

Mkuu wa kitengo cha biashara ya kadi Benki ya NMB, Bw. Philbert Casmir akihutubia katika shughuli hiyo.
Meneja wa  wateja binafsi Benki ya NMB, Bi.Nyamisinda Manyonyi akitoa elimu ya Mikopo kwa walimu wakuu wa shule za msingi na sekondari Mkoa wa Arusha.
Washiriki wa Semina ya walimu wakuu wa Shule za msingi na wakuu wa Shule za Sekondari zilizopo Mkoa wa Arusha, wakisikiliza hotuba ya mgeni rasimi kwenye uzinduzi wa semina ya  mafunzo ya bidhaa za NMB. Semina hiyo yenye lengo la kutoa elimu ya fedha na bidhaa mbalimbali za NMB ilifanyika leo jijini Arusha na kuhudhuriwa na walimu zaidi ya 300.

Walimu wametakiwa kujiendeleza kwa kukopa mikopo nafuu, yenye tija na kuwawezesha kutatua  changamoto zinazowakabili ili kuweza kunufaika na kufurahia kazi wanayoifanya.

Akizungumza wakati wa mafunzo ya walimu wa mkoani Arusha yaliyoandaliwa na Benki ya NMB, Afisa elimu sekondari wa mkoa huo, Khalifani Omary alisema mafunzo hayo yatawajenga walimu katika kujiwekea kipato na kufahamu fursa mbalimbali zilizoko benki ili kuweza kujiendeleza kimaisha.

 

"Mafunzo haya yatawasaidia katika kuwaongezea ufahamu namna wanavyoweza kunufaika na benki ya NMB ikiwa jitihada hizi zitaleta matokeo chanya nakuleta faraja kwa jamii,"alisema Omary.

 

Afisa elimu alisema jitihada hizo ni nzuri na  zinaunga mkono juhudi za serikali katika kuhakikisha watanzania walio wengi wanajumuhishwa katika mfumo rasmi wa kifedha ili kuinua  vipato vyao hivyo ametoa rai kwa taasisi nyingine za kifedha nchini kufanya jitihada hizo kama NMB.

 

Alisema anashukuru huduma za kibenki zimeboreshwa na kusogezwa karibu na wateja wake kwani hapo awali walimu walipata taabu kutembea umbali mrefu hivyo benki ya NMB imekuwa chachu ya maendeleo katika jamii kwa kuwanufaisha wateja wake.

 

Kwa upande wake Mkuu wa biashara ya Kadi wa benki ya NMB, Philbert Casmir  alisema  wameandaa mafunzo yanayoitwa siku ya walimu ambapo wameanza mkoani Arusha kwa kutambua mchango wa mwalimu katika jamii na kutoa suluhisho ya changamoto zao katika kujikwamua kimaisha ikiwemo mikopo nafuu na bima mbalimbali.

 

"Tunatambua mwalimu ni mwezeshaji katika jamii hivyo NMB tumekuja na suluhisho mahususi kwa walimu ikiwemo mikopo nafuu ya kujenga au kununua nyumba,"alisema Mkuu huyo.

 

Casmir alisema pia kuna bima za walimu na watanzania kwa ujumla zinazoweza kuwasaidia kupata nafuu wakati wa majanga mbali mbali.

 

Baadhi ya walimu hao walisema wanashukuru benki ya NMB kwa kuwapa mafunzo hayo ambayo yatawasaidia katika kuwekeza fedha nakutumia katika matumizi sahihi ya kujiendeleza kiuchumi na kuwaletea maendeleo.


Mwalimu  mkuu wa shule ya msingi Daraja mbili, Zukra Kalunde alisema mafunzo hayo yatawasaidia katika kufahamu umuhimu wa kadi pamoja na kujifunza namna ya kupata mikopo nafuu ya benki hiyo itakayowasadia kujiendeleza kiuchumi kama ujenzi wa nyumba zao za kuishi na biashara.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.