Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi Amejumuika na Wananchi wa Mkoa wa Kusini Pemba Katika Futari Maalum Aliyowaandalia Katika Ukumbi wa Kiwanja cha Watoto Tibirinzi Chakechake.

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Wananchi wa makundi mbalimbali wa Mkoa wa Kusini Pemba wakati wa hafla ya futari maalum aliyowaandalia katika kiwanja cha Watoto Tibirinzi Chakechake Pemba

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi amefutari pamoja na wananchi wa Mkoa wa Kusini Pemba na kuwataka kuendelea kuiombea nchi amani.

Hafla hiyo ya futari iliyoandaliwa na Rais Dk. Mwinyi kwa ajili ya wananchi wa Mkoa  Kusini Pemba ilifanyika katika ukumbi wa kiwanja cha kufurahishia watoto Tibirinzi, Chake Chake , Mkoa wa Kusini Pemba ambayo ilihudhuriwa na baadhi ya viongozi wa Serikali, dini, vyama vya siasa pamoja na makundi maalum ya wananchi wa Mkoa huo.

Katika maelezo yake, Alhaj Dk. Mwinyi aliwasisitiza wananchi wa Zanzibar kuendelea kuiombea nchi amani sambamba na mshikamano ili nchi iweze kujiletea maendeleo zaidi.

Alhaj Dk. Mwinyi aliwapongeza wananchi wa mkoa huo kwa kukubali mualiko wake na kuweza kuhudhuria kwa wingi katika hafla ya futari aliyowaandalia wananchi wa mkoa huo ambao waliwakilishwa na wenzao katika makundi maalum.

Aidha, Alhaj Dk. Miwnyi alieleza kwamba ameona haja ya kuandaa furari hiyo ili aweze kuungana na wananchi wa Mkoa huo katika mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani.

Katika shukrani zake hizo, Alhaj Dk. Mwinyi alieleza utaratibu wake ambao ameuanza wa kufutari na wananchi wa  mikoa ya Unguja na Pemba ambapo kesho Alhamis ya Machi 06.2021 anatarajia  kufutari pamoja na wananchi wa Mkoa wa Mjini Magharibi huko katika ukumbi wa Michenzani Mall.

Nao wananchi wa Mkoa wa Kusini Pemba wakitoa neno la shukurani lililotolewa na Sheikh Omar Khamis Othman kwa niaba yao alieleza jinsi walivyofarajika na mwaliko huo waliopewa na Alhaj Dk. Mwinyi kwa niaba ya wenzao wa Mkoa huo na kuahidi kuendelea kumuunga mkono ili azidi kuiongoza vyema Zanzibar.

Wananchi hao waliipongeza hatua hiyo ya Alhaj Dk. Mwinyi kwa lengo lake la kuwaunganisha wananchi wa Zanzibar  ambapo mkusanyiko huo unaonesha dhahiri nia yake hiyo njema.

Aidha, wananchi hao walitoa shukrani kwa Mama Mariam Mwinyi kwa kuungana na wananchi wa Mkoa huo katika futari hiyo maalum aliyoiandaa Alhaj Dk. Mwinyi.

Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Matar Zahor Massoud kwa upande wake alieleza kwamba jambo alilolifanya Alhaj Dk. Mwinyi ni jambo kubwa na kumuombea dua kwa moyo wake huo wa kuwafutarisha wananchi wa mkoa huo.

Matar alimuahidi Alhaj Dk. Mwinyi kuwa wananchi wa Mkoa huo wataendelea kumuuunga mkono katika kuhakikisha Zanzibar inapata maendeleo huku akitoa shukurani kwa imani yake kwa wananchi wa Pemba na Wazanzibari wote kwa jumla.

Nae Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi kwa upande wake aliungana na viongozi wanawake wa kitaifa pamoja na wananchi wa Mkoa huo wa Kusini Pemba katika futari hiyo maalum aliyoianda  Alhaj Dk. Mwinyi hapo katika ukumbi wa Uwanja wa Kufurahishia watoto Tibirinzi, Pemba.

Wakati huo huo, Alhaj Dk. Mwinyi aliungana na waumini wa dini ya Kiislamu wa Mkoa huo wa Kusini Pemba katika sala ya Taraweh katika Masjid Al Rahmaan Gombani Chake Chake Pemba ambapo mara baada ya sala hiyo alipata fursa ya kuwasalimia wananchi na kuwaeleza kwamba Zanzibar iko katika hali ya amani na umoja.

Alhaj Dk. Mwinyi alimuomba Mwenyezi Mungu aendelee kuipa Zanzibar amani, umoja na maendeleo huku akieleza furaha yake kwa kufika Pemba na kukutana na waumini pamoja na wananchi mbali mbali katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani kwa kufutari pamoja sanjari na kufanya ibada nao.

Sambamba na hayo, alitoa shukurani kwa wananchi wote wa Zanzibar kwa mapokezi wanayompa popote pale anapokwenda ambapo wananchi wamekuwa wakimpa mapokezi makubwa Unguja na Pemba na kuwataka kwa kila mmoja kumuombea dua ili aweze kutekeleza vyema majukumu yake.

Alhaj Dk. Mwinyi amemaliza ziara yake ya siku mbili kisiwani Pemba ambapo alipata fursa ya kufutari pamoja na wananchi wa makundi mbali mbali wa mikoa ya Kusini na Kaskazini Pemba akiwa amefuatana na mkewe Mama Mariam Mwinyi.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.