Habari za Punde

Waziri Mhe. Jafo Yamkera Machinjio ya Tabora.

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo akipata maeleo ya namna ya mkaa mbadala unavyozalishwa kutoka kwa Bw. Leonard Kushoka Mkurugenzi wa Kampuni ya ‘Kuja na Kushoka’. Waziri Jafo amefanya ziara ya kikazi Mkoani Tabora leo tarehe 12/05/2021 kwa lengo la kukagua uzingatiaji wa Sheria ya Mazingira.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo akikagua machinjio katika Manispaa ya Tabora ambapo ametoa maelekezo ya kukarabati mfumo wa maji taka ndani ya mwezi mmoja na kutoa siku saba za usafi wa kina katika eneo hilo ambalo limekithiri kwa uchafu.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo leo tarehe 12/5/2021 amekutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa waTabora Dkt. Philemon Sengati  kwa lengo la kuendeleza agenda ya Uhifadhi wa Mazingira nchini. 

Na Lulu Mussa.Tabora

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo amemuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Tabora Bw. Bosco Ndunguru katika kipindi cha siku saba kuhakikisha machinjio katika Manispaa yake yanafanyiwa usafi madhubuti.

Agizo hilo limetolewa leo na Waziri Jafo mara baada ya kufanya ziara ya kikazi ya kukagua usimamizi na uzingatiaji wa Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 Mkoani Tabora. Akiwa katika machinjio hayo Waziri Jafo ameshuhudia kukithiri kwa uchafu ndani na nje ya jengo hilo jambo ambalo linahatarisha afya za wakazi wa Tabora.

“Mazingira ya hapa ni machafu sana, natoa muda wa wiki moja marekebisho yafanyike na nipate taarifa ya utekelezaji mapema iwezekanavyo pia natoa mwezi mmoja wa ukarabati wa mfereji wa maji taka” Jafo alisisitiza.

Waziri Jafo pia ametembea Kampuni ya kuzalisha mkaa mbadala ya “Kuja na Kushoka” na kutoa rai kwa taasisi za Umma na Binafsi kupunguza matumizi ya kuni na mkaa na kuhamasisha matumizi ya mkaa mbadala unaozalishwa kutokana na taka.

“Azma ya Serikali ni kuhakikisha tunatunza mazingira yetu kwa kupunguza matumizi ya kuni na mkaa, natoa rai kwa Shule za Binafsi na za Serikali kununua hizi mashine za kuzalisha mkaa badala ili zitumike kuzalisha mkaa katika Shule zao pia kama chanzo cha mapato kwa kutengeza mkaa na kuuzia wengine” Jafo alisisitiza.

Akiwasilisha taarifa ya Kampuni ya kuzalisha mkaa mbadala Bw. Leonard Kushoka amesema anatumia teknojia ya kuchakata taka na kuzalisha mkaa mbadala ambao umekuwa wa manufaa kwa wakazi wa Tabora na Tanzania kwa ujumla kwa kutoa ajira kwa vijana kunusuru mazingira.

Waziri Jafo yuko Mkoani Tabora kukagua shughuli za uhifadhi na usimamizi wa Mazingira ambapo kwa siku ya kwanza amekagua Machinjio ya Manispaa ya Tabora, Kampuni ya kuzalisha Mkaa mbadala na ukaguzi wa mabwawa ya maji taka.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.