Habari za Punde

Waziri Mkuu Majaliwa : Tumieni Urithi wa Ukombozi Kujikomboa Kiuchumi.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiongea wakati wa Ufunguzi wa  Kongamano  la Kutambua na Kuenzi Mchango Anuai wa Historia ya Tanzania katika Ukombozi wa Bara la Afrika na Kikao Kazi cha Maafisa Utamaduni na Michezo, katika kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Mei 21, 2021 Jijini Dar es Salaam.


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameitaka jamii kuutumia urithi wa ukombozi uliopo nchini kujikomboa kiuchumi na kifikra
Amesema kuwa ni vyema jamii ambazo zinatumia au zina miliki maeneo au miundombinu ya urithi wa ukombozi wa Afrika ikavitunza na kupata ushauri wa kitaalamu wa kuanzisha makumbusho na kuvutia utalii katika eneo hilo ili kujiongezea kipato.

Ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Mei 21, 2021) wakati wa Ufunguzi wa  Kongamano la kutambua na kuenzi mchango anuai wa historia ya Tanzania katika Ukombozi wa bara la Afrika na Kikao Kazi cha Maafisa Utamaduni na Michezo, kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.

“Nimeambiwa yapo maeneo zaidi ya 225 ya urithi wa ukombozi nchini, maeneo hayo ni fursa kwetu iwapo tutayatumia vyema. Urithi huu wa ukombozi ukiondoka umeondoka, haurudi mara ya pili. Hivyo, ni matarajio yangu kuwa mikoa ya Lindi, Ruvuma (Songea), Mtwara na Mbeya itakuwa mikoa ya kwanza kunufaika na zao jipya hili la utalii wa kiukombozi”

Aidha, Waziri Mkuu amesisitiza kuwa jukumu la kuhifadhi na kulinda urithi wa ukombozi tulionao ni la kila mmoja ili vizazi vijavyo viweze kujifunza na kuendeleza.

Amesema kuwa makundi yote au mtu yoyote ambaye ana mali za urithi wa ukombozi aviwasilishe katika Makumbusho ya Urithi wa Ukombozi wa Afrika iliyopo Dar es Salaam ili vihifadhiwe kitaalamu visije vikapotea

“Niwaahidi kuwa siyo kuwa vitu hivyo vitakuwa mali ya Serikali la hasha vitaendelea kuwa mali yako, kikundi au Taasisi husika, bali Serikali itavitunza katika hali ya usalama Zaidi”

Akizungumzia kuhusu ufundishwaji wa somo la historia, Waziri Mkuu amewaasa washiriki wa kongamano hilo kuhakikisha ndoto za hayati Dkt. John Magufuli ya kuona somo la historia linafundishwa katika ngazi zote za elimu inatimia. 

Kadhalika, Waziri Mkuu ametoa wito wa Watanzania kuweka utaratibu wa kufanya ziara za kwenda kujifunza kwenye maeneo ya ukombozi, “ni wakati muhimu wa kutambua maeneo yenye kumbukumbu muhimu yaliyokomboa nchi yetu na bara la Afrika”

Waziri Mkuu pia ameiagiza Programu ya Urithi wa Ukombozi ianze kutoa elimu mashuleni na kufungua klabu za ujifunzaji wa somo la historia kwa kushirikiana na TAMISEMI na Wizara ya Elimu.

Naye, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Innocent Bashungwa amesema kuwa lengo la kongamano hilo ni kuelimisha umma umuhimu wa kujikomboa kiuchumi na kifikra kupitia uhifadhi na utangazaji wa zao la utalii wa kiukombozi.

Pia kuhamasisha jamii kuwa na utangamano wa kitaifa ambao huzaa uzalendo, mshikamano na upendo.

Kaulimbiu ya Kingamano hilo ni “Urithi wa Ukombozi, Fahari ya Afrika”
 
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 - DODOMA,                      
IJUMAA, MEI 21, 2021.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.