Habari za Punde

RC Malima Amewataka Wafugaji Kujiunga Kwenye Vyama vya Ushirika wa Ufungaji.

Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania Dkt. George Msalya kushoto akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Adam Malima wakinywa maziwa wakati wa uzinduzi huo.
MKUU wa Mkoa wa Tanga Adamu Malima akizungumza  wakati akizundua wiki ya unywaji maziwa iliyofanyika kwenye viwanja vya Tangamano mjini Tanga

MKUU wa Mkoa wa Tanga Adam Malima amewataka wafugaji kujiunga kwenye vyama vya ushirika vya ufugaji ili serikali na taasisi mbalimbali ziweze kuwafikia kirahisi kwa kuwapatia huduma zikiwemo za kifedha ili kuweza kujikwamua kiuchumi.


Malima aliyasema hayo wakati akizundua wiki ya unywaji maziwa iliyofanyika kwenye viwanja vya Tangamano mjini Tanga ambapo alisema wakihimizana kupitia vyama vya ushirikia wanaweza kuwa na mikakati ya makusudi kwa ajili ya kuendeleza sekta hiyo.

Alisema sekta hiyo ina mchango mkubwa sana hivyo upo umuhimu wa wafugaji hao kuona namna nzuri ya kuweza kujiunga kupitia vyama vya ushirika ili waweze kupata mafanikio mbalimbali ikiwemo ya kuweza kupata fursa za mikopo kupitia taasisi za kifedha zilizopo nchini.

 “Ndugu zangu wafugaji lazima tubadilike na kuona umuhimu wa kujiunga na vyama vya ushirika badala ya kuwa pekee yenu kwani kujiunga huko kutawasaidia na kuwa rahisi kwa serikali kuwafikia sambamba na taasisi mbalimbali za kifedha kwa lengo la kuweza kujikwamua kiuchumi” Alisema

Hata hivyo aliwataka wazalishaji hao waongeze uzalishaji wa maziwa kutokana na kwamba wadau wakubwa ni watoto na lazima wawe na idadi kubwa ya watumiaji huku akitoa wito kwa wazazi na walezi kutambua kwamba suala la maziwa ni muhimu kwa watoto kama anavyokula chakula.

 Mkuu huyo wa Mkoa aliwataka wafugaji na wazalishaji wa maziwa wawe na uratatibu wa kupunguza bei ya maziwa na kuongeza uzalishaji wenye tija ili bei ya maziwa ishuke.

Hata hivyo alimuagiza Afisa uzalishaji Mkoa wa Tanga kukutana na wazalishaji wa mkoa na hao wazalishaji wakafanye hesabu juu ya namna Tanga inawezeje kuwa mzalishaji mkubwa wa maziwa kwa kuwa kuna mwamko mkubwa wa uzalishaji wa ng'ombe kutokana na kwamba sekta ya maziwa bado ina nafasi kubwa sana.

Awali akizungumza wakati wa uzinduzi huo Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania Dkt. George Msalya alisema lengo la bodi ya maziwa ni kusimamia na kuratibu tasnia ya maziwa nchini kutokana na kwamba ni muhimu kwa maendeleo haya kiuchumi kwa sababu ni biashara na lishe.

Alisema bodi hiyo inaratibu shughuli zote ambapo alisema kuhusu wiki ya unywaji maziwa dunia kote inapofika June 1 nchi nyingi zinahamasisha watu kunywa maziwa hivyo wanaungana na hapa nchini watu wanakunywa maziwa kidogo sana

Alisema takwimu za Tanzania mwaka jana kwa mtanzania mmoja anakunywa maziwa lita 54 kwa mwaka lakini shirika la afya la umoja wa mataifa wanapendekeza kwamba ili angalau uweze kupata virutubisho vya kutosha ni angalau ukanywa maziwa lita 200 kwa mwaka

Aliongeza kwamba uzalishaji wa maziwa kwa sasa ni lita bilioni 3.4 takwimu za mwaka jana ukichukua kiasi hicho cha maziwa na idadi ya watanzania milioni 60 utagundua watanzania wanakunywa maziwa kidogo

Hata hivyo kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika wa Wafugaji wa Ng'ombe wa  Maziwa Mkoa wa Tanga (TDCU) Shamte Saidi alisema unywaji wa maziwa upo chini lakini uzalishaji bado hawajafikia kiwango ambacho kitaweza kuhakikisha watanzania wanaweza kupata lita mbili kwa wananchi na ndio maana kauli mbiu ikasema tuongoze uzalishaji.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.