Dodoma, 28 Julai 2021
Tarehe
21 Julai, 2021 kulikuwa na tukio la vifo vya samaki ambao walionekana wakiwa
wamezagaa katika ufukwe uliopo kati ya Hospitali ya Aghakhan na Ocean Road, Dar
es Salaam.
Pamoja
na hatua zilizochukuliwa za kuzuia wananchi kuchukua samaki hao kama kitoweo na
kuzuia uingizaji wa samaki hao katika Soko la Magogoni Feri, sampuli za samaki hao zilichukuliwa kwa ajili
ya chunguzi za kimaabara na kilogramu 156 zilizobaki kuteketezwa na Afisa Uvuvi
wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.
Ili
kubaini chanzo cha vifo vya samaki hao, uchunguzi ulifanyika katika maeneo
makuu matatu:
i)
Utambuzi wa aina za samaki waliokufa, ukubwa
wao, aina ya vyakula ndani ya matumbo na muonekano wa hali ya nje ya samaki vilifanyika kwenye maabara ya Taasisi
ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI).
ii)
Uchunguzi wa maji kuangalia vimelea vyenye
sumu ulifanywa kwenye maabara ya Taifa ya Uvuvi, Dar es Salaam.
iii)
Uchunguzi wa viuatilifu, sumu zitokanazo na
mimea na kemikali nyingine za viwandani ilifanywa katika Maabara ya Mkemia Mkuu
wa Serikali.
MATOKEO
i) Aina
tisa za samaki zilitambuliwa ambazo ni kui,
mkizi, janja, tambanji, chaa, kuku bahari, kolekole pandu, kaa, kambamiti na kambakochi. Aidha, samaki jamii ya kui ilichukua sehemu kubwa ya samaki hao kwa asilimia 36 ikifuatiwa na jamii ya
mkizi iliyokuwa na asilimia 29. Kwa
ujumla, samaki hawa hupatikana kwenye kina kifupi cha maji. Pia, wengi wa
samaki hao walikuwa wachanga. Sehemu kubwa ya matumbo ya samaki hayakuwa na
chakula, ingawaje aina tatu za samaki (kui, mkizi na tambanji) walikutwa na
dagaa, kaa na uduvi katika matumbo yao. Samaki waliochunguzwa walikuwa na hali
nzuri, ngozi ilikuwa haikutatuka na ikiwa na rangi angavu, macho yao yalionekana
meusi na angavu, na mapezi yalikuwa angavu bila utelezi, walikuwa na nyama
imara na hakukuwa na harufu mbaya. Hali hii inaondoa uwezekano kuwa vifo hivi
vinaweza kuwa vimetokana na sumu au vilipuzi. Hata hivyo, samaki wengi
walionekana kuwa na midomo wazi kuashiria kuwa walikosa hewa au walikufa
wakitafuta hewa.
ii) Uchunguzi
wa sampuli za maji yaliyochukuliwa katika eneo haukubaini vimeamaji vinavyohusishwa
na sumu Mf. Kundi la Microcystis,
dianoflagelates, pseudonitchia, na Gambierdiscus
spp. Aidha, uchunguzi wa matumbo ya samaki haukubaini uwepo wa vimeamaji hivi hali
inayoondoa uwezekano wa kuwa samaki hao walikufa kutokana na sumu itokanayo na
vimeamaji hivyo.
iii) Vilevile,
uchunguzi wa kitaalamu kuhusu uwepo wa viuatilifu, sumu zitokanazo na mimea na
kemikali nyingine za viwandani uliofanywa na Mkemia Mkuu wa Serikali umeonyesha
kuwa hakukuwa na sumu katika samaki hao; hivyo kuhitimisha kuwa vifo vya samaki havikutokana na uwepo wa sumu ya
aina yoyote ile kwenye maji eneo la tukio.
Kutokana
na samaki wengi kuwa na midomo wazi na wengine kuwa na matamvua wazi, uwezekano
ni mkubwa kuwa samaki hao walikufa kwa kukosa hewa ya oksijeni.
Imetolewa:
Edward
Kondela
Kny: Mkuu wa Kitengo
cha Mawasiliano Serikalini
Kiambatisho
Na. 1
No comments:
Post a Comment