Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi Amekutana na Kuzungumza na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe.Balozi Mulamula.

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na mgeni wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata R. Mulamula, alipofika Ikuli Jijini Zanzibar kwa mazungumzo na kujitambulisha 
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akimsikiliza Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata  R. Mulamula, alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo na kujitambulisha na (kulia kwake) Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe Balozi. Mbarouk Nassor Mbarouk, mazungumzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesisitiza haja kwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuiimarisha Sera ya Diplomasia ya Uchumi ili  Zanzibar nayo iweze kupata fursa zaidi katika kuimarisha uchumi wake.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ukiongozwa na Waziri wake Balozi Liberata Rutageruka Mulamula

Katika maelezo yake, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa uchumi wa Zanzibar unategemea sana kazi zitakazofanywa na Mabalozi wanayoiwakilisha Tanzania  nje ya nchi hasa ikizingatiwa kwamba Zanzibar ina bidhaa nyingi za kuuza nje ya nchi zikiwemo viungo.

Alieleza kwamba kwa kipindi kirefu Zanzibar imekuwa ikiingiza bidhaa nyingi kutoka nje ya nchi na kutokuwa na bidhaa nyingi ambazo zinazotoka Zanzibar na kuweza kuuzwa nje ya nchi.

Hivyo, Rais Dk. Miwnyi alisisitiza haja kwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuiimarisha Sera ya Diplomasia ya Uchumi ili iweze kuleta tija zaidi hasa kwa upande wa Zanzibar kwa azma ya kuweza kupata soko kwa bidhaa zake inazozalisha.

Alisema kuwa kuna nchi kadha zikiwemo zile za Jumuiya ya Nchi za Falme za Kiarabu (UAE), Oman na nchi nyenginezo zinahitaji bidhaa za Zanzibar hivyo, juhudi za makusudi zikichukuliwa mafanikio yanaweza kupatikana katika nyanja hiyo hasa ikizingatiwa kwamba fursa ipo.

Rais Dk. Mwinyi alieleza haja ya kutilia mkazo suala zima la kuunganishwa kwa wafanyabiashara wa Zanzibar na wale wa nje ya nchi zikiwemo nchi hizo za Jumuiya ya Falme za Kiarabu (UAE) na nyenginezo.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alitoa shukurani kwa uongozi wa Wizara hiyo ukiongozwa na Waziri wake Balozi Mulamula kwa kuja Ikulu kujitambulisha kwake  na kueleza kwamba utaratibu wa kukutana mara kwa mara ni mzuri kwani unajenga zaidi mahusiano.

Rais Dk. Mwinyi pia, alipongeza hatua zinazochukuliwa na Wizara hiyo katika kuziweka katika mazingira mazuri ofisi za Wizara hiyo zilizopo hapa Zanzibar.

Sambamba na hayo, akieleza suala zima la  Diaspora, Rais Dk. Mwinyi alisisitiza haja ya Wanadiaspora kuangaliwa uwezekano wa kuanza kupewa baadhi ya haki za raia za nchini mwao ili waweze kufanya shughuli mbali mbali za maendeleo nchini mwao zikiwemo zile za uwekezaji huku hatua nyengine zikiendelea kufanyiwa kazi.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi aliueleza uongozi huo mwelekeo na Sera ya Zanzibar katika kujikita na Uchumi wa Buluu hiyo ni kutokana na mazingira ya Zanzibar ambayo visiwa vyake vimezungukwa na bahari.

Mapema Balozi Liberata Rutageruka Mulamula alimueleza Rais Dk. Mwinyi azma ya uongozi wa Wizara hiyo kuja kujitambulisha kwake sambamba na kuja kumpongeza kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kishindo.

Balozi Mulamula alieleza lengo kuu la Wizara yake ya kufanya kazi kwa karibu na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar huku akitoa shukurani za dhati kwa mashirikiano mazuri inayopata Wizara hiyo kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. 

Aidha, Balozi Mulamula alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa uwamuzi wake wa kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo imeleta mafanikio makubwa na imekuwa msaada mkubwa kwa Wizara yake katika kutekeleza majukumu yao.

Balozi Mulamula alisema kuwa kuwepo kwa maridhiano ya kisiasa hapa Zanzibar kumeweza kuwavutia watu wengi ambao wameonesha nia ya kuja kufanya kazi hapa Zanzibar.

Sambamba na hayo, Balozi Mulamula alimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa teuzi zake anazozifanya na alizozifanya ambazo zimekuwa zikizingatia jinsia.

Katika mazungumzo hayo pia,   Balozi Mulamula alieleza kwamba ofisi za Wizara yake zilizopo Zanzibar zimekuwa zikifanya kazi vizuri na kuweza kutoa mashirikiano mazuri kwa Serikali.

Kwa upande wa Diaspora, Waziri Mulamula alieleza azma ya Wizara hiyo katika  kuhakikisha inalipa kipaumbele suala la Wanadiaspora hasa ikizingatiwa hivi sasa Wizara yake inaipitia Sera yake ya mwaka 2001.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.