Habari za Punde

SMZ Itaendelea Kutowa Ushirikiano Katika Kufanikisha Diplomasia na Mataifa Mbalimbali Ili Kujenga Uhusiano.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Leberata Mulamula akiongozana na Uongozi wa Wizara yake walipokwa kwa mazungumzo na kujitambulisha , mazungumzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Makamu Vuga Jijini Zanzibar.

Na.Kassim Abdi OMPR.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amemuhakikishia Waziri wa Mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea kutoa ushirikano katika kufanikisha Diplomasia na Mataifa mbali mbali Ulimwenguni ili kutoa fursa ya kujenga Uhusiano mwema na Nchi izo.

Mhe. Hemed alisema hayo alipokutana kwa mazungumzo na Uongozi wa Wizara hiyo walipofika kujitambulisha Afisini kwake Vuga Jijini Zanzibar.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaamini kuwa kutambuliwa kwa Zanzibar katika sera ya mambo ya Nje kutaweza kusaidia kukuza imani ya wananchi juu ya kudumisha dhana ya Muungano waTanganyika na Zanzibar ulioasisiwa tangu 1964.

Mhe.Hemed alieleza kutokana na sera hiyo kutambua umuhimu wa Uchumi wa Buluu kwa taifa itaweza kutanua wigo katika kukuza sekta hiyo ambayo kwa kiasi kikubwa Tanzania itakuwa kiuchumi na kupelekea kutoa ajira nyingi kwa wananchi wake.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema kuwa mbali na Sekta ya Uchumi wa buluu, amefarijika kuona Sekta ya Utalii inapewa kipaumbele katika sera hiyo, jambo ambalo litasaidia kuitangaza nchi kwa mataifa mbali mbali duniani.

Nae Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Leberata Mula Mula alimpongeza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa kuendelea kuongoza vyema katika kumsaidia Mhe. Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa kuhakikisha wananchi wa Zanzibar wanapata maendeleo ya haraka.

Alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Wizara anayoisimamia itajenga uhusiano mwema sambamba na kufanya ushawishi kwa Nchi mbali mbali kufungua Ofisi za kibalozi Zanzibar ili kukuza uhusiano na ushirikiano na Tanzania.

Pamoja na mengine Mhe. Balozi Mula Mula alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa Ofisi zote za kibalozi za Tanzania zilizopo nje ya Nchi zina jukumu la kukuza Diplomasia ya Uchumi pamoja na kukuza utalii kwa lengo la kuvutia uwekezaji kwa maendeleo ya Taifa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.