Mkurugenzi wa Mazingira, Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Andrew
Komba akifungua Kongamano kuhusu Mchango wa Taifa katika Upunguzaji wa Uzalishaji wa Gesi joto
(NDC) Julai
23, 2021 jijini Dodoma kwa niaba ya Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Mary
Maganga.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mary Maganga amesema Tanzania imekamilisha rasimu ya Mchango wa Kitaifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (Nationally Determined Contributions -NDCs).
Bi. Maganga amesema
hayo Julai 23, 2021 jijini Dodoma katika hotuba ya ufunguzi wa Kongamano kuhusu
Mchango wa Taifa katika Upunguzaji wa Uzalishaji wa Gesijoto (NDC) iliyosomwa
kwa niaba yake na Mkurugenzi wa Mazingira, Dkt. Andrew Komba.
Alisema kuwa mchango wa
NDC umetokana na Mpango wa Ahadi za Kitaifa (Intended Nationally Determined Contributions-INDCs) za kukabiliana
na Mabadiliko ya Tabianchi uliowasilishwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
katika Sekretarieti ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi Septemba
2015.
“Kama mnavyofahamu, nchi
zinazoendelea ikiwemo Tanzania zinaathirika sana na mabadiliko ya tabianchi
kutokana na uwezo mdogo kifedha na kiteknolojia wa kuweza kuhimili athari za
mabadiliko ya tabianchi. Kutokana na ukweli huo kuhimili mabadiliko ya
tabianchi ndio kipaumbele cha nchi hizi,” alisema.
Bi. Maganga aliongeza
kuwa nchi zinazoendelea kutokana na kutokuwa na viwanda vingi, hazijachangia au
zimechangia kidogo katika uzalishaji wa gesijoto ambazo zinasababisha au zimesababisha
mabadiliko ya tabianchi lakini kwa muktadha wa Makubaliano ya Paris nchi hizi
zinatakiwa kutoa mchango katika kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi na
upunguzaji wa gesijoto kwa kuzingatia hali halisi ya nchi na uwezo wa kiuchumi
kwa maendeleo endelevu.
Kwa mujibu wa
Makubaliano ya Paris, kila nchi itaamua kiwango cha mchango wake katika
kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Kiwango hicho kitategemea uchumi wa
nchi husika na pia kiasi cha uzalishaji wa gesijoto.
Akizungumzia Rasimu
ya NDC alisema kuwa imeainisha hatua za kuchukuliwa kwenye eneo la kuhimili
athari na pia kupunguza uzalishalishaji wa gesijoto na katika kuhimili athari
za mabadiliko ya tabianchi kwenye sekta za Kilimo, Mifugo, Misitu, Nishati,
Mazingira ya Pwani na Bahari na Uvuvi, Rasilimali za Maji, Utalii, Makazi ya
Binadamu, Afya, Miundombinu, na Upunguzaji
Majanga.
Alisema shabaha ni
kupunguza vihatarishi vya majanga yatokanayo na mabadiliko ya tabianchi. Kwa
mfano sekta ya maji inatarajia kuongeza upatikananji wa maji safi na salama
mjini na vijijini kutokaasilimia 60 hadi 90 ifikapo mwaka 2030.
Ili kuchangia katika
upunguzaji wa gesijoto, shabaha ni kupunguza uzalishaji gesijoto kutegemeana na
uwezo kiuchumi kuanzia asilimia 10 hadi 20 ya uzalishaji wa gesijoto nchini.
Sekta za kipaumbele zitakazohusika na upunguzaji uzalishaji gesijoto ni nishati, usafirishaji, misitu na taka. Sekta
hizi ndiyo zinachangia kwa kiasi kikubwa katika uzalishaji wa gesijoto kwa sasa
na zina fursa kubwa ya kuchochea na kuchangia maendeeleo ya kiuchumi .
“Suala muhimu la
kutambua ni kuwa michango ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi
iliyobainishwa katika NDCs itatekelezwa kwa kuzingatia Kanuni ambazo NDCs
imeweka. Kanuni hizo ni kuwa utekelezaji wa NDCs utategemea upatikanaji wa
fedha na teknolojia kutoka Jumuiya ya Kimataifa na mifuko ya Kimataifa
inayofadhili masuala ya mabadiliko ya tabianch,” alisisitiza.
Mpango wa Utekelezaji
wa NDC umeandaliwa ukibainisha kwa kina shughuli zitakazotekelezwa kwa kila
kusudio lililoainisha katika NDC na kiasi cha fedha kitakachohitajika.
Kulingana na Mpango wa Utekelezaji wa NDC ulioandaliwa kiasi cha Dola za
Marekani Bilioni 14,071,670,000 zitahitajika kwa kipindi cha miaka mitano
kuanzia mwaka 2020.
Fedha kwa ajili ya
utekelezaji wa NDC zinategemea zaidi Mifuko ya Fedha iliyo chini ya Mkataba wa
Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi na vyanzo vingine kimataifa. Ofisi
zenye dhamana ya mazingira kwa Tanzania Bara na Visiwani yaani Ofisi ya Makamu
wa Rais na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar zitafanya kazi kwa pamoja
na sekta husika kutafuta fedha kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli
zilizoainishwa katika NDC.
Kongamano hilo lilihusisha Wadau kutoka Wizara za kisekta, Idara za Serikali Wadau wa Maendeleo binafsi, Taasisi za Utafiiti na Elimu pamoja na Asasi za kiraia.
No comments:
Post a Comment