Habari za Punde

Wasanii wa Ngoma Za Asili Watakiwa kujisajili Kupata Fedha Za Mfuko Wa Sanaa

 

Na.Adeladius Makwega  CHAMWINO-WHUSM
Serikali imesema kuwa  wasanii wa ngoma za asili wanatakiwa   kujisajili  kwa  maafisa Utamaduni wa Wilaya  ili waweze kupata  fedha za Mfuko wa Utamaduni na Sanaa ambapo kwa  mwaka wa fedha 2021/2022 mfuko huo umetengewa  bilioni 1.5.

Kauli hiyo imesemwa  Julai 24, 2021 na Mkurugenzi Msaidizi wa Maendeleo ya Sanaa wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bi Leah Kihimbi katika Tamasha la Cigogo linalofanyika Chamwino mkoani Dodoma.

“Pesa hizo zinatolewa kwa vikundi  vilivyofanya usajili  na siyo sandakalawe nendeni kwa maafisa utamaduni wa wilaya ili muwe na sifa ya kupata  pesa hizo vinginevyo  pesa  hizo zitapangiwa matumizi mengine.” Amesema Bi Kihimbi.

“Utamaduni wetu  lazima tuulinde kama  Mheshimiwa Rais  Samia Suluhu anavyosisitiza  ili  uwepo katika jamii  yetu   milele na milele.” Ameongeza Mkurugenzi huyo Msaidizi.

Naye Mkurugenzi wa Maendeleo ua Utamaduni wa Wizara hiyo Dkt  Emmanuel Temu  amesema kuwa  matamasha  ya utamaduni yanapofanyika ni vizuri  kuwashirikisha watu kutoka  kila rika ili  kuhakikisha  mila na tamaduni za kitanzania zinarithiwa kwa  haraka  kutoka kizazi kimoja kwenda kingine.

Pia katika tamasha hilo tahadhari dhidi ya ugonjwa Uviko 19 umesisitizwa kwani ugonjwa huo ni hatari sana kwa afya  ya binadamu na washiriki wote wameomba kufuata kanuni za afya.

Tamasha hilo  la kitamaduni linafanyika kwa siku mbili tarehe 24 na 25, 2021

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.