Habari za Punde

Watendaji Watakiwa Waende Wakatatue Kero za Ardhi Kwa Wananchi - Naibu Waziri Mhe. Mabula.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akisalimiana na viongozi wa wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma alipowasili kwa ziara ya kusikiliza na kuzitafutia ufumbuzi kero za ardhi katika wilaya hiyo 
Mkazi wa Kibaigwa wilayani Kongwa mkoa wa Dodoma akiwasilisha kero yake ya ardhi kwa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula wakati wa ziara ya kusikiliza na kuzitafutia ufumbuzi kero za ardhi katika wilaya hiyo 
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiungumza na wananchi wa Mji mdogo wa Kibaigwa wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma wakati wa ziara ya kusikiliza na kuzitafutia ufumbuzi kero za ardhi katika wilaya hiyo jana. Wa pili kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Kongwa Remidius Mwema
Sehemu ya wananchi wa Mji mdogo wa Kibaigwa wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma waliojitokeza katika mkutano wa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula kusikiliza na kuzitafutia ufumbuzi kero za ardhi katika wilaya hiyo jana.

Na Munir Shemweta, KONGWA

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amewataka watendaji wa sekta ya ardhi kutoka ofisini na kwenda kusikiliza kero za ardhi katika halmashauri zao ili kuondoa migogoro ya ardhi.

Dkt Mabula alisema hayo jana wakati akizungumza na wananchi wa Kibaigwa katika wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma akiwa katika ziara ya kusikiliza na kuzitafutia ufumbuzi kero za ardhi kwenye mikoa ya Morogoro na Dodoma ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Alisema, kero nyingi za ardhi katika halmashauri nchini hazihitaji Waziri ama ngazi ya Wizara kwenda kuzitafutia ufumbuzi bali zinaweza kutatuliwa na maafisa ardhi waliopo kwenye halmashauri husika.

‘’Ninachotaka kuona mnatoka kwenda kufanya vikao vya kusikiliza changamoto za ardhi katika halmashauri zenu na hata kama hakuna kero katoeni elimu watu wajue, maana wananchi  wanauza ardhi hovyo na hawajui hata mipango ya matumizi ya ardhi na pia hawajui faida za kupimiwa na kumilikishwa.’’ Alisema Dkt Mabula

Alimtaka Kamishna wa Ardhi Msaidzi mkoa wa Dodoma Thadei Kabonge kuhakikisha anasimamia watendaji wa sekta ya ardhi kwenye mkoa wake kutoa elimu ya masuala ya ardhi  badala ya kusubiri wananchi kufika ofisi za ardhi kuwasilisha malalamiko.

Wananchi wa Mji Mdogo wa Kibaigwa wilayani Kongwa waliwasilisha malalamiko yao kwa Naibu Waziri  wa Ardhi Dkt Mabula na kumtaka awasaidie kupata ufumbuzi wa changamoto zao baada ya kukwama kutatuliwa kwa muda mrefu na Maafisa Ardhi katika halmashauri ya Wilaya ya Kongwa.

Malalamiko mengi yaliyowasilishwa mbele ya Naibu Waziri wa Ardhi katika mkutano huo yalikuwa ni kuhusiana na kudhulumiwa maeneo kwa baadhi ya wananchi, udaiji fidia, uingizaji mifugo kwenye mashamba ya wakulima, ucheleweshaji kesi za ardhi katika mabaraza ya ardhi pamoja na kutokamalika kwa zoezi la urasimishaji kwa baadhi ya maeneo.

Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Dodoma Thadei Kabonge alisema  kupitia mkutano huo wa hadhara wa Naibu Waziri wa Ardhi kuwa, kutokana na kukua kwa mji wa Kibwaigwa ofisi yake ina mpango wa kuandaa Mpango Kabambe wa Mji wa Kibaigwa..

Sambamba na hilo aliongeza kuwa, kutokana na kuibuka kwa kero nyingi za ardhi katika mji huo sasa ofisi yake itaakwenda katika mji huo na timu ya wataalamu wa sekta ya ardhi na Msajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ili kusikiliza migogoro ya ardhi na kuipatia ufumbuzi.

‘’Sisi tutakuja kama mkoa kusikiliza migogoro mingine midogomidogo pamoja na kutoa hati  na tutakuja na maafisa ardhi, wapima ardhi na msajili wa hati pamoja na msajili msaidzii wa mabaraz ya ardhi maana masuala mengi yaliyoelezwa yanahusu mabaraza walau ajaribu kuelimisha wananchikutoa’’ Alisema Kabonge.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.