Habari za Punde

Wizara wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar yapokea msaada wa vitabu vya kusomeshea kutoka Uingereza

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe, Simai Mohammed Said Akipokea Msaada wa Vitabu mbalimbali vya Sayansi na hesabu, kutoka Skuli ya LANCLEY ACADEMY SECONDARY, ya BERKSHIRE, ENGLAND UK, kwa ajili ya Wanafunzi wa Skuli za Zanzibar. Wa pili kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini Profesa Hamed Rashid Hikimany.
Baadhi ya wafanyakazi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, wakibeba vitabu vya Sayansi na Hesabu, vilivyoletwa kutoka Skuli ya LANCLEY ACADEMY SECONDARY iliyoko BERSHIRE nchini ENGLAND kwa ajili ya msaada kwa Wanafunzi mbalimbali wa Zanzibar.
 Picha na  Maulid Yussuf WEMA

Na Maulid Yussuf WEMA

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe, Simai Mohammed Said amesema Mataifa mbali mbali yapo tayari kuisaidia Zanzibar kimaendeleo  ili izidi kupiga hatua ya kufikia malengo ya uchumi wa buluu hasa katika sekta ya Elimu.
   
Ameyasema hayo wakati wa hafla ya  kukabidhiwa Msaada wa vitabu vya  Sayansi katika ukumbi wa Wizara hiyo Mazizini Mjini Unguja amesema, ili kufikia haraka malengo hayo ni vyema kuitumia misaada inayotolewa na wahisani kama ilivyokusudiwa.
    
Amesema nchi yeyote ili ifikie malengo ni lazima iwe na misingi imara ya Elimu kwani ndio mama wa maendeleo katika kila Taifa.

Aidha ameeleza kuwa Zanzibar ipo tayari kutoa mashirikiano na nchi mbali mbali  Duniani ikiwa  lengo ni kuendana na kasi ya maendeleo ya uchumi wa buluu.

Aidha amewaomba Wazanzibari wanaoishi nje ya nchi kuhakikisha wanaisaidia Zanzibar katika nyanja zote za maendeleo.

Amesema msaada vitabu hivyo watavigawanya zaidi katika Skuli zenye uhaba wa vitabu kwani kuna baadhi ya Wanafunzi wanatumia kitabu kimoja watu wawili kutokana na tatizo hilo. 
   
Kwa upande wake   Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini Profesa Hamad Rashid Hikimany amesema  wametoa vitabu ili  kuunga mkono masomo mbalimbali hasa ya sayansi hali ambayo inaweza kupelekea  Wanafunzi kuweza  kufaulu vyema katika masomo hayo .

Aidha amesema  malengo yao ni kuhakikisha wanatoa misaada katika kuleta maendeleo ya Taifa lao hasa Sekta ya Elimu kwani vitabu vya dini Zote vimetilia mkazo juu ya suala la kupata na kutoa elimu.

Zaidi ya vitabu  Elfu Moja kutoka Skuli ya LANGLEY ACADEMY SEKONDARY  iliopo mji wa BERKSHIRE, ENGLAND UK, vimekabidhiwa  vikiwemo vitabu vya Hesabu, Vitabu vya Kemia, Fizikia na kiengereza.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.