Naibu Waziri wa
Nishati Mhe. Stephen Byabato akizungumza na wanakijiji wa Katambike (Hawamo
pichani) tarehe 12 Julai, 2021, alipotembelea kijiji hicho kilichopo katika Kata
ya Ugalla, wilaya ya Mpanda, Halmashauri ya Nsimbo, Mkoa wa Katavi akiwa katika
ziara ya kikazi mkoani humo.
Naibu Waziri wa
Katiba na Sheria Mhe. Geophrey Mizengo Pinda (Mb.) akizungumza na wanakijiji wa
Katambike (Hawamo pichani) tarehe 12 Julai, 2021, alipoungana na Naibu Waziri
wa Nishati, Mhe. Byabato katika ziara ya kikazi katika kijiji cha Katambike,
kilichopo katika Kata ya Ugalla, wilaya ya Mpanda, Halmashauri ya Nsimbo, Mkoa
wa Katavi.
Wanakijiji cha kijiji
Katambike, Kata ya Ugalla, wilaya ya Mpanda, Halmashauri ya Nsimbo, Mkoa wa
Katavi wakimsikiliza Naibu Waziri Byabato (Hayumo pichani) alipokuwa
akizungumza nao kufuatia ziara yake ya kikazi kijijini hapo tarehe 12 Julai, 2021.
Na Dorina Makaya - Katavi
Serikali itatumia zaidi
ya shilingi bilioni 24.7 kuunganisha umeme kwenye vijiji 53 ambavyo bado
havijaunganishiwa umeme mkoani Katavi katika Mradi Kabambe wa kupeleka umeme
vijijini Awamu ya III Mzunguko wa pili.
Hayo yameelezwa na
Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Stephen Byabato tarehe 12 Julai, 2021,
alipotembelea kijiji cha Katambike, Kata ya Ugalla, wilaya ya Mpanda,
Halmashauri ya Nsimbo, Mkoa wa Katavi akiwa katika ziara ya kikazi mkoani humo.
Amesema, Serikali
inatambua, umuhimu wa upatikanaji wa umeme wa uhakika mkoani Katavi na kuwa MW
5.3 zinazozalishwa katika kituo cha Mpanda bado hazitoshelezi mahitaji ya umeme
hususan katika kuwezesha shughuli za kiuchumi na maendeleo ya viwanda na
biashara hapa nchini.
Naibu Waziri Byabato
ameeleza kuwa, Serikali imeamua kuleta grid ya Taifa mkoani Katavi ili kuwa na
umeme wa uhakika mkoani humo na tayari ujenzi wa majengo ya vituo vya umeme kuleta
grid ya Taifa mkoani Katavi umefikia zaidi ya asilimia 90.
Amevitaja vituo hivyo
kuwa ni Ipole, Inyonga na Mpanda.
Ameongeza kuwa, pesa
kwa ajili ya kuleta umeme mkoani Katavi ipo, na zitawekwa Transfomer mbili zenye ukubwa wa 15MVA kila moja sawa na 12MW, zitakazowekwa
kwenye kituo cha Inyonga na nyingine katika kituo cha Ipole ili kuhakikisha
kila kituo kinatoa umeme wa kutosha na wa uhakika.
Naibu Waziri Byabato
amesema, mradi wa Grid ya Taifa kwa mkoa wa Katavi utakamilika ifikapo Agosti,
2023.
Amewaeleza wananchi
wa kijiji cha Katambike kuwa, umeme utakuwa umefika kijijini hapo ifikapo mwezi
Octoba mwaka 2021, na kuwa hakuna kijiji kitakachoachwa kuunganishiwa umeme.
Amewaasa wanakijiji
cha Katambike kuanza kufanya maandalizi ya kupokea umeme kwa kuanza kutandaza
nyaya kwenye nyumba zao (Wiring) na kulipia shilingi elfu 27,000 tu ili waweze
kuunganishiwa umeme utakapofika kijijini hapo.
Aidha, amewaomba
wanakijiji hao kutoa ushirikiano kwa Serikali katika kuhakikisha miundo mbinu
inatunzwa na kutoharibiwa kwa nguzo na kuonya kuwa atakayebainika kuiharibu
miundombinu ya umeme atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Akizungumza wakati wa
mkutano huo Mbunge wa jimbo la Nsimbo, Mhe. Anna Lupembe amemshukuru Naibu
Waziri Byabato kwa kufika mkoani Katavi, kujionea hali halisi ya umeme mkoani
humo na kutoa ahadi ya kuvipelekea umeme vijiji 53 ambavyo bado
havijaunganishwa umeme na kuahidi kufikisha umeme kijijini Katambike ifikapo
mwezi Octoba 2021.
Mhe. Lupembe,
amesema, kupatikana kwa umeme katika kata ya Ugalla kutasaidia sana katika
kuinua kilimo cha mpunga na kuwezesha mazingira ya uanzishaji wa viwanda vidogo
vidogo vitakavyoboresha bidhaa ya mchele katika viwango vya juu zaidi na
kuwaongezea kipato wananchi wa Ugalla.
Awali Naibu Waziri
Byabato alitembelea vituo vipya vinavyojengwa vya Ipole, Inyonga na Mpanda na
kuridhishwa na kasi ya ujenzi wa vituo hivyo.
Mara baada ya
kuwasili katika wilaya ya Mlele tarehe 11 Julai, 2021 Naibu Waziri Byabato
alikutana na Mkuu wa Wilaya ya Mlele Filiberto Sanga na kupata taarifa kuhusu
upatikanaji wa umeme Wilayani Mlele.
No comments:
Post a Comment