Habari za Punde

WAANDISHI wa habari Pemba wametakiwa kujikita katika uandishi wenye kuibua na kusaidia kutatua matatizo ya kijamii ili kuchochea upatikanaji wa dhana ya utawala bora,

Na Gaspary Charles- TAMWA ZNZ

WAANDISHI wa habari Pemba wametakiwa kujikita katika uandishi wenye kuibua na kusaidia kutatua matatizo ya kijamii ili kuchochea upatikanaji wa dhana ya utawala bora, ushirikishwaji na uwajibikaji wa kila mmoja katika jamii.

Dkt. Mzee Mustafa Mzee kutoka Chuo kikuu cha Taifa (SUZA) aliyasema hayo katika mafunzo ya uwajibikaji kwa waandishi wa habari Pemba yaliyoandaliwa na Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa kuwajengea uwezo wanawake kudai haki zao za demokrasia, siasa na uongozi unaofadhiliwa na Ubalozi wa Norway Nchini.

Alisema kufanya hivyo kutasaidia kuwafanya viongozi na wanajamii kuwa wawajibikaji kwa nafasi zao na kupelekea upatikanaji wa maendeleo ya haraka katika jamii.

Alibainisha kwamba wandishi wa habari kwa hivi karibuni wameshindwa kuwajibika ipasavyo katika uchambuzi wa taarifa kwa kina na badala yake huishia kuandika habari katika hatua za awali jambo ambalo linapelekea kucheleweshwa kwa upatikanaji wa haki na uchukuaji wa maamuzi katika mambo mbalimbali.

Akizungumzia kuhusu ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi na demokrasia alisema ili lengo la mradi la kushajihisha ushiriki wa wanawake katika masuala ya uongozi na demokrasia kufikiwa ni lazima waandishi kuongeza nguvu zaidi kuandika habari za uchambuzi ili kusaidia wanawake kuwa na uwezo wa kudai haki zao za kidemokrasia na uongozi katika nafasi mbalimbali.

“Waandishi mnatakiwa kusaidia wananchi kuelewa kwamba kumchagua mwanamke kuwa kiongozi si suala la hisani bali ni wajibu na ni haki yao ya msingi. Jukumu la mwandishi wa habari ni kutoa elimu kwa jamii ili kuwa na ufahamu wa kutosha juu ya haki zao za msingi,” alisema.

Mratibu mradi huo, Salma Lusangi aliwataka waandishi kutumia taaluma ya mafunzo hayo kubadilika kutoka kwenye uandishi wa kuripoti matukio na kujikita katika uandishi wa habari za uchambuzi kuhusu ushiriki wa wanawake katika demokrasia, siasa na uongozi.

Alisema, “Mafunzo haya tuyatumie kama ni chachu ya kubadilika katika kazi zaetu za uandishi kwa kuandika habari ambazo zinalenga kubadili mitazamo hasi ya wanajamii na kuwaelezea kwanini wanawake wanatakiwa kupewa fursa sawa katika demokrasia, siasa na uongozi.”

Akizungumzia kuhusu mradi huo unaofadhiliwa na ubalozi wa Norway alisema mradi unalenga kuwawezesha wandishi wa habari sitini Unguja na Pemba kuandika habari za uchambuzi kuhusu masuala ya kidemokrasia na uongozi kwa wanawake.

"Mradi huu unalenga kuwawezesha waandishi 60 kuwa na uwezo wa kuandika habari za kuwahamasisha wanawake kuwa na uwezo wa kudai haki zao katika masuala ya kidemokrasia, siasa na uongozi katika kila nyanja,"alisema Salma Lusangi.

Mmoja kati ya washiriki wa mafunzo hayo kutoka Shirika la Utangazaji Zanzibar ‘ZBC’ Mchanga Haroub Shehe, alisema changamoto inayowakwaza waandishi kushindwa kuandika habari za uchambuzi ni baadhi ya sera za vyombo vya habari kuwabana kwa kuchagua aina ya taarifa za kutolewa.

Alisema, “wandishi wengi wanahitaji sana kuandika habari zenye kuchambua masuala mbalimbali lakini changamoto kubwa iliyopo si kila chombo cha habari kipo tayari kutangaza aina hizo za taarifa.”

Nae Amina Ahmed mshiriki wa mafunzo hayo alibainisha, “waandishi wa habari tunatakiwa tubadili mwelekeo wa uandishi wetu, tujikite katika kuandika habari zenye kuchambua mazuri ya viongozi wanawake ili wawe ni mifano kwa wengine.” Alisema.

Mradi wa kuwajengea uwezo wanawake kudai haki zao za demokrasia, siasa na uongozi unaofadhiliwa na Ubalozi wa Norway unatekelezwa na TAMWA ZNZ kwa kushirikiana na Chama cha Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) pamoja na  PEGAO. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.