Habari za Punde

Wazanzibarin Watakiwa Kuendeleza Umoja na Mshikamano Kufikia Malengo ya Serikali. - Mhe. Hemed.

Na,Kassim Abdi - OMPR.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amewataka Wazanzibar kuendeleza umoja na mshikamano miongoni mwao ili kufikia malengo ya serikali ya awamu ya nane ya kuwaletea maendeleo wananchi wake.

Mhe. Hemed alieleza hayo mara baada ya kutekeleza ibada ya sala ya Ijumaa katika Msikiti wa Ijumaa matemwe mnazi mrefu Wilaya ya Kaskazini “A” Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Amesema Rais DK. Mwinyi ni muumini wa umoja na mshikamano siku zote ataendelea kuhubiri juu ya suala hilo kwa lengo la kuwaunganisha wananchi waweze kushikamana na kushirikiana katika kuijenga Zanzibar Mpya.

Akigusia juu ya Maradhi ya Covid-19 Makamu wa Pili wa Rais aliwaomba waumini waliosali mskitini hapo na wananchi kwa ujumla kuendelea kifatilia vyombo vya habari juu ya taarifa sahihi kuhusu ugonjwa huo na kuwasihi kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo kwa kufuata maelekezo ya Wataalamu wa Afya.

Akizungumzia kuhusu mporomoko wa maadili Mhe. Hemed amewakumbusha wananchi kuendelea kupiga vita juu ya uingizaji, utumiaji wa dawa za kulevya nchini kutokana na athari zake kwa vijana.

Amesema kukithiri kwa watumiaji wa madawa hayo ikihusisha watumiaji na wasambazaji wenyeji kutoka Zanzibar  kunapelekea kupoteza nguvu kazi ya taifa ambao ni tegemeo la Taifa katika kuleta maendeleo ya Nchi.

Nae, Khatibu aliehutubu katika mskiti huo Sheikh Kundi Chum Haji amewasihi waumini kuyatumia vyema masiku matukufu ya mwezi wa Muharram kwa kufanya ibada ili kupata radhi kutoka kwa  Allah (SW).

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.