Habari za Punde

Waziri wa Habari Mhe. Bashungwa Awasilisha Taarifa ya Ukimwi kwa Kamati ya Bunge.

Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo  Mhe. Innocent Lugha Bashungwa imewasilisha taarifa kuhusu hali ya VVU/UKIMWI, Kifua Kikuu na magonjwa yasiyo ambukiza leo Agosti 12, 2021 kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi Jijini Dodoma.


Na Richard Mwamakafu, WHUSM

Menejimenti ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ikiongozwa na Waziri wake, Mhe. Innocent Lugha Bashungwa imewasilisha taarifa kuhusu hali ya VVU/UKIMWI, Kifua Kikuu na magonjwa yasiyo ambukiza leo Agosti 12, 2021 kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi Jijini Dodoma.

 

Taarifa hiyo imeainisha hali halisi ya magonjwa hayo pamoja na mafanikio, changamoto na mikakati inayochukuliwa na Wizara katika kudhibiti maambukizi mapya ambapo Wajumbe wa Kamati hiyo wameshauri Wizara kuweka mikakati mahususi ya kuhamasisha jamii kujikinga na magonjwa hayo.

 

Miongoni mwa mkakati iliyopendekezwa kutumika kudhibiti magojwa yasiyoambukiza kuwa ni pamoja na kuanzisha vikundi vya mazoezi ya pamoja maarufu kama Jogging clubs kuanzia kwenye ngazi za vijiji  hadi taifa  ili kuwafanya wananchi kuimarisha afya zao.

 

Aidha, Kamati imeishauri Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kukaa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ili kuona namna bora ya kuimarisha michezo katika ngazi mbalimbali kuanzia shule ya msingi hadi sekondari kama ilivyokuwa awali kabla ya kuondolewa.

 

Wameitaka Wizara kuwahamasisha Wasanii kupitia kazi zao kuelimisha jamii ambapo wamewapongeza baadhi ya Wasanii wa muziki wa kizazi kipya kwa kutoa nyimbo zenye tungo nzuri za kuelimisha jamii kuhusu ugonjwa wa UKIMWI.

 

Baadhi ya wasanii hao na nyimbo zao kwenye mabano ni pamoja na Feruz (Starehe), Matola (Kosa la Marehemu) na Mwana FA (Alikufa kwa ngoma).

 

Kwa upande wake, Wizara imedhamiria kuanzisha kampeni kupitia Vyombo vya Habari kuhimiza Waandishi wa Habari kuandika na kutangaza habari mbalimbali kuhusu afya na lishe ili jamii iweze kujikinga na magonjwa yasiyoambuza kama Saratani na Kisukari.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.