Habari za Punde

Kikao cha pamoja kati ya Ofisi ya Makamo wa kwanza wa Rais na Ujumbe kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu

Katibu Mkuu OMKR Dkt Omar D. Shajak akiwa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Profesa Jamal walipokutana katika kikao cha mashauriano ya pamoja kati ya Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kupitia Baraza la Taifa la Watu wenye Ulemavu na ujumbe kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu 

 KATIBU Mkuu Ofisi yq Makamo wqa kwanza wa Rais,  Dkt OMAR D. SHAJAK akitoa maelezo kwa Ujumbe kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Tanzania Bara pamoja na watendaji wakuu wa OMKR

Raya Hamad Suleiman – OMKR                                                   05/09/2021

 

Katibu kuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Dkt Omar Dadi Shajak amesema uwepo wa sera na sheria zinazoendana kati ya Tanzania bara na Zanzibar ni fursa ya kuongeza ufanisi na kufikia malengo ya taasisi hizo. 

Ameyasema hayo katika kikao cha mashauriano ya pamoja kati ya Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kupitia Baraza la Taifa la Watu wenye Ulemavu na ujumbe kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu wenye lengo la kukuza ushirikiano na kubadilishana uzoefu hasa katika sekta ya Watuwenye Ulemavu. 

Dkt Shajak amesema katika kukuza ufanisi ni vyema kuimarisha uhusiano wa karibu uliokuwepo wa taasisi zote mbili kuzungumza lugha moja ya kiutendaji kwa vile kila upande una mafanikio na changamoto za kiutendaji lakini mwisho wa siku tunazungumzia mafanikio na maslahi ya Watanzania ya Watu wenye Ulemavu. 

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Profesa Jamal Adam amesema lengo la ujio wao ni kujifunza kutoka pande zote mbili kwa kubadilishana uzowefu na kuangalia miongozo wapi panahitaji maboresho pamoja na kupeana mawazo ya kiutendaji 

“leo tumejifunza utaratibu mzuri uliopo wa kukusanya takwimu za Watu wenye Ulemavu ambazo zinakwenda mpaka kwenye Shehia hili tunaondoka nalo na wenzetu wa Zanzibar tumeona wao bado hawajawa na vyuo katika stadi za kazi na marekebisho kwa Watu wenye Ulemavu hapa tunaona kuwa tumepata kitu kizuri kwa pande zote mbili na tutafanya kazi kwa pamoja “alisisitiza Profesa Jamal 

Mkurugenzi wa Baraza la taifa la Tatu la Watu wenye Ulemavu ndugu Ussi Khamis Debe amesema Baraza la Taifa la Watu wenye Ulemavu na Sekretarieti yake wanashughuli kubwa ya kuratibu masuala ya Watu wenye Ulemavu kwa Serikali na kijamii kwa ujumla 

Nae Mkurugenzi anaeshughulikia masuala ya Watu wenye Ulemavu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu ndugu Jacob Mwinula amesifu uwepo wa mfumo wa kielekroniki ambao unarahisisha kupata taaarifa sahihi kwa ajili ya ustawi wa haki za watu wenye ulemavu, pamoja na suala la miundo mbinu ambapo amesema Zanzibar imepiga hatua kubwa hivyo watahakikisha miongozo hio wanaifanyia kazi kwa manufaa ya kiutendaji. 

Aidha Jacob amesema Watu wenye Ulemavu wanayo haki na nafasi ya kujiendeleza na kupata huduma kwa jamii sawa na watu wasio na ulemavu na kuongeza kuwa ushiriki wao katika maisha ya kila siku ndani ya jamii hauna budi kulenga katika kupunguza au kuondosha maisha tegemezi. 

Katika kikao hicho mapendekezo kadhaa yametolewa ya kukuza ushirikiano ikiwemo kuwepo ushiriki wa pamoja kati ya Zanzibar na Tanzania Bara kwenye ushiriki wa mikutano ya kimataifa na kikanda. 

Kuimarishwa mashirikiano juu ya utekelezaji wa mikataba ya kimataifa juu ya haki za Watu wenye Ulemavu pamoja na kuangaliwa suala la Watu wenye Ulemavu kama ni suala la haki za kibinaadamu Tanzania nzima. 

Vikao hivyo ni muendelezo wa mikakati ya serikali katika kuimarisha utendaji kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania kwa mambo yasiyokuwa ya Muungano kwa sekta ya Watu wenye Ulemavu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.