Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapiunduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi Ameupongeza Kwa Dhati Uongozi wa Maalim Seif Foundation Kutenga Siku Maalum ya Kumbukumbu Yake.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na kuhutubia wakati wa hafla ya mkutano wa ufunguzi wa Kongamano la Maadhimisho na Kumbukumbu ya Maisha ya Maalim Seif Sharif Hamad, lililofanyika katika ukumbi wa Hotel ya Golden Tulip Zanzibar
 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameupongeza kwa dhati uongozi wa Maalim Seif Foundation kwa kuja na wazo la kutenga siku maalum kwa ajili ya kumbukumbu na kusherehekea maisha ya Hayati Maalim Seif Sharif Hamad.

Pongezi hizo amezitoa leo katika Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Maisha ya Maalim Seif Sharif Hamad, huko katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip, iliyopo Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Zanzibar, Mkoa wa Mjini Magharibi ambapo mgeni rasmi ya hafla hiyo alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.

Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Hayati Maalim Seif Sharif Hamad ana historia ndefu sana katika medani ya siasa ndani na nje ya Tanzania ambapo amekuwa sehemu ya siasa na uongozi nchini kwa zaidi ya miaka 45 na kuweza kutumikia nafasi mbali mbali za uongozi.

Alizitaja nafasi hizo ni pamoja  na kuwa kiongozi katika Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chama cha CUF, chama cha ACT Wazalendo pamoja na kuwa Waziri wa Elimu Zanzibar, Waziri Kiongozi na kufanya kazi kwa Awamu mbili tofauti akiwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.

“Mimi binafsi, nimebahatika kufanya kazi kwa karibu sana na hayati Maalim Seif Sharif Hamad akiwa ni Makamu wangu wa Kwanza wa Rais katika hii Awamu ya Nane ya Uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa”.

“Bahati mbaya sana kutokana na kudra na uwezo wa Mwenyezi Mungu hatukubahatika kuwa nae kwa kipindi kirefu sana ndani ya uongozi wa Serikali hii na Mwenyezi Mungu kumpenda zaidi na kumchukua, hakika pengo lake haliwezi kuzibika ndani ya Serikali na katika Jamii ya Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla”,alisema Rais Dk. Mwinyi.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Maalim Seif atakumbukwa kwa mengi mazuri aliyoifanyia nchini hii na hasa suala la kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha Amani, Mshikamano na Upendo unaimarika na kudumu hapa nchini kwani alikuwa mwana maridhiano wa kweli.

Alisema kuwa kielelezo halisi ni juhudi zake katika kuhakikisha kwamba nchi inabakia kuwa na amani na utulivu baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Maalim Seif hakuwa ni mtu mwenye kujikweza, kiburi au majivuno daima alikuwa ni mtu alieweka maslahi ya Zanzibar kwanza na hakuwa mbinafsi wala mchoyo katika kushauri au kutoa hekima na nasaha zake kwa viongozi vijana wao.

Aliongeza kuwa katika kipindi alichofanya kazi nae aliweza kuvuna na kujifunza kwake mambo mengi yenye lengo la kufunza na kuthamini mshikamano, maelewano na maendeleo ya nchi kwa jumla.

Kitengo cha Habari

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.